Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaajiri wahitimu wa kada ya mazingira waliomaliza katika vyuo vikuu nchini?

Supplementary Question 1

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kuweza kuwavutia wawekezaji.

Je, nini mpango wa Serikali katika kuajiri watumishi wa kada ya mazingira katika miradi yote mikubwa ambayo inatekelezwa na Serikali?

Swali langu la pili; je, kwa kuwa nchi yetu kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya tabia nchi, kwa mwaka huu wa fedha, Serikali imepanga ajira ngapi?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa amekuwa hodari sana kufuatilia masuala mbalimbali ya ajira za kada mbalimbali ambazo zinahusu mkoa wake na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza la je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri watu kwenye miradi hii mikubwa; Niseme tu kwamba Serikali inaajiri kwa kuzingatia ukomo wa bajeti kama ambavyo inaidhinishwa na Bunge lako hili Tukufu. Kwa hiyo, tutaendelea kuzitenga kwenye bajeti na kuleta hapa Bungeni kuona namna gani nafsi hizi zitaongezwa Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili:Je, Serikali ilitenga jumla ya ajira ngapi? Kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya ajira 30,000 kwa kada zote na taasisi mbalimbali za Serikali nchini na hiyo pia kama nilivyojibu katika jibu langu la nyongeza la kwanza kwamba ni kutokana ukomo wa bajeti ambao tulipatiwa. Hata hivyo tutaendelea kutenga na kuona namna gani tunaweza kuangalia hizi kada zote zikapata watumishi wa kutosha.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kwenye jibu lako unasema ajira ambazo Serikali ilitoa vibali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ajira 223 utekelezaji bado unaendelea. Ni kwamba wale waombaji hakuna, au yaani mwaka ule uliopita kipindi kile mpaka sasa hivi bado mnaendelea au kuna changamoto kwenye sekretarieti ya ajira?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, Hapana, siyo kwamba kuna changamoto kwenye sekretarieti ya ajira, lakini hizi nafasi zote 223 zinatokana na taasisi mbalimbali za Serikali. Kwa hiyo, sekretarieti ya ajira inaanza mchakato pale tu zile taasisi zilizoidhinishiwa vibali vyao vya kuajiri zinapoanza mchakato wao kupeleka sekretarieti ya ajira. (Makofi)