Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga shule mpya za msingi katika maeneo ya Mbirani, Makibo, Kiyombo na Tutuo – Sikonge?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na pia napongeza majibu mazuri ya Serikali hasa hiyo tathmini ambayo inaenda kufanyika ni tathmini nzuri ya school mapping.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili. Swali la kwanza, hivi karibuni kuanzia miaka ya 2017 kumekuwa na ujenzi wa madarasa, mabweni na kadhali na hiyo ni miundombinu ya shule. Je, tuna uhakika gani kama hizi Shilingi Bilioni 230 nazo zitaendeleza tu utaratibu huo wa kujenga madarasa badala ya shule mpya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye taarifa ya jana ya sensa, katika Wilaya ya Sikonge, wananchi wameongezeka mara mbili, maana yake ni kwamba hata idadi ya wanafunzi imeongezeka mara mbili.

Je, kwa nini Serikali isiweke kipaumbele ya kujenga shule mpya Nne katika Wilaya ya Sikonge kwenye hayo maeneo ambayo nimeyataja kwa mwaka huu wa fedha? Ahsante sana. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba katika tathmini tunayoifanya ya ujenzi wa shule mpya za msingi na katika fedha ambayo imetengwa sehemu ya hiyo fedha itakwenda kujenga shule mpya sehemu nyingine tutakwenda kukarabati maboma ya madarasa ambayo yamekwisha muda wake, na maeneo mengine tutabomoa kabisa na kuanza upya ujenzi katika mabwawa ambayo yamekwisha kabisa. Kwa hiyo, huo ndiyo mpango wa Serikali ambao upo, kwa hiyo nimuondoe hofu kwenye hilo.

Mheshimiwa Spika, suala lake kuhusu shule nne mpya za msingi, nikuhakikishie tu fedha ipo kwa sababu mradi peke yake wa BOOST ambao tunautekeleza kwa miaka mitano, thamani yake ni trilioni 1.15. Kwa hiyo ni fedha ipo ya kutosha ambayo tutahakikisha changamoto ya elimu msingi tunazimaliza nchini. Ahsante.