Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Primary Question

MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kujenga Vituo vya Afya katika Kata ya Lyamugungwe na Kihanga?

Supplementary Question 1

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini mpango wake wa 2024/2025 ni mbali sana. Ione uwezekano wa kurudisha kati 2023/2024. Maswali mawili ya nyongeza ni haya: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Mgama, kipo kituo cha afya na wananchi walishajenga msingi wa wodi, sasa uwezo wao wa kuendelea kujenga ni mdogo: Je, ni lini Serikali itatusaidia kuleta fedha ili tujenge wodi ili wananchi wa vijiji 12 wanaohudumiwa hapo wapate huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Pamoja na kwamba umesema Halmashauri itatenga Shilingi milioni 400, uwezo wa Halmashauri yetu bado siyo mkubwa hivyo. Aliyetangulia, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, aliahidi kuleta Shilingi milioni 300. Ni lini fedha hizo zitakuja Magulilwa ili tukamilishe hiki kituo cha afya?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jackson Gideon Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Kata ya Mgama kwa kutoa nguvu zao kujenga kituo cha afya na kujenga msingi kwa ajili ya wodi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, afanye tathmini ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa wodi hiyo ili Serikali ione namna ya kutafuta fedha kwa kushirikiana Halmashauri kwa maana ya mapato ya ndani kukamilisha ujenzi wa wodi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kweli kwamba Mheshimiwa Waziri wa Nchi, aliahidi kupeleka Shilingi milioni 300 fedha ya Serikali kwa ajili ya kujenga kituo cha afya pale Magulilwa. Katika jibu la msingi tumetenga Shilingi milioni 400 kupitia mapato ambayo ndiyo fedha ya Serikali hiyo hiyo kwa kwa jili ya ujenzi wa kituo cha afya hicho. Ahsante.

Name

Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Primary Question

MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kujenga Vituo vya Afya katika Kata ya Lyamugungwe na Kihanga?

Supplementary Question 2

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kule Magu Lutale, Wamanga na Igogo, kuna uhitaji mkubwa sana wa vituo vya afya: Je, Serikali ina mpango gani kuyaangalia maeneo yale ambayo yako mbali na huduma? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniventura Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Magu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge ikiwepo ya Mtalia na hizo nyingine mbili kwa kadri ya uhitaji wa vituo vya afya, Serikali ilishatoa maelekezo kwamba Halmashauri ziainishe kata za kimkakati kwa ajili ya kujenga vituo vya afya, kwa kuwa hatujengi kituo cha afya kila kata wala hatujengi zahanati kila Kijiji, bali tunajenga vituo vya afya kwenye kata za kimkakati ambazo zina vigezo ambavyo vinaelezea na pia zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba twende tukaainishe haya maeneo kama ni maeneo ya kimkakati na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Magu alete Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kwenda hatua inayofuata.

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kujenga Vituo vya Afya katika Kata ya Lyamugungwe na Kihanga?

Supplementary Question 3

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, Kata ya Korongwe na Kata ya Mkwamba kuna umbali wa kutosha kufika katika hospitali ya wilaya, na hizo kata zote mbili hazina vituo vya afya: Nataka kujua mkakati wa Serikali ili kuwaokoa wanawake ambao wamekuwa wanajifungulia njiani na kupewa penalty, wanalipa Shilingi 50,000?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Nkasi ni miongoni mwa Halmashauri ambazo bado zina kata ambazo hazina vituo vya afya, na tayari Mkurugenzi alishawasilisha kata za kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kata hizi mbili ni sehemu ya kata ambazo tutakwenda kutafuta fedha, kwa kushirikiana na Halmashauri, kwa maana ya mapato ya ndani na Serikali Kuu ili kuanza ujenzi wa vituo vya afya hivi kwa awamu.