Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali inaweza kutoa tathmini ya urejeshwaji wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa Vikundi vya Akinamama, Vijana, na Watu Wenye Ulemavu katika kipindi cha angalau miaka mitatu iliyopita?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Wizara, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza; je, Wizara haioni umuhimu wa kuwawezesha halmashauri kutenga maeneo mahususi kwa wajasiriamali na kuyawekea miundombinu stahiki ili wale wanaopokea mikopo waweze kuanzia miradi yao na shughuli zao kwenye maeneo haya ambayo yatakuwa kama incubation center na pia waweze kupewa ushauri nasaha?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa vile tunafahamu kwamba mikopo inayotolewa na NEDF chini ya SIDO inalipika, inarejeshwa kwa kiwango kikubwa cha zaidi ya aslilimia 90. Je, Wizara haioni umuhimu wa kushirikisha SIDO kwenye kutoa mikopo ya halmashauri?

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba halmashauri zetu lazima zitenge maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji na maeneo haya pia wanufaika vikundi ambavyo vinakopa asilimia zile 10 wawe ni moja ya wanufaika katika maeneo haya ambayo yanatengwa mahususi kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hili tumeboresha zaidi, tumeshakaa na Wizara ya Kilimo kuangalia hata makundi ya vijana wasomi ambao wanapata asilimia 10 kwenye Halmashauri zetu, Majiji na Manispaa, kuangalia namna bora ya kuweza kuwasaidia maeneo mahususi kama haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo hili tunalifanyia kazi na nitumie nafasi hii kuzielekeza Halmashauri zote nchini, kuhakikisha maagizo ya Serikali ya kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji yanashughulikiwa. Tunashirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kuweza kuliratibu hili vyema kwa sababu yapo masuala ya fidia. Halmashauri nyingine zimekuwa na nia ya kutenga maeneo, lakini wanakosa fedha kwa ajili ya fidia. Kwa hiyo, yote haya tunayaangalia ndani ya Serikali ili kuhakikisha tunaratibu vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu mikopo ya SIDO na mikopo kupokea, hili ni eneo lingine ambalo Wizara Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara tunaangalia namna ya ku-link pamoja ili zile asilimia 10 ambazo tunazitoa kwenye halmashauri na fedha kupitia Mifuko mengine ndani ya Serikali, tunakaa pamoja na kuangalia namna bora ya kuipeleka kwenye makundi ili iweze kuleta tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili kwenye suala la asilimia 10 mikopo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunafanya tathmini ya nchi nzima kuangalia namna bora tutakayoweza kutumia fedha hizi kwa sababu tumetathmini ni takriban zaidi bilioni 60 kila mwaka zinapatikana kupitia halmashauri kupitia vikundi.

Kwa hiyo, tungependa kuona mabilioni haya yanapokwenda kwenye vikundi yanaleta tija, yanasaidia vikundi, lakini vikundi hivi vinasaidia nchi katika kujenga uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tathmini hii kufanyika, tutaleta hapa Bungeni uchambuzi huo ili Waheshimiwa Wabunge waweze kushauri ili tuweze kwenda vizuri. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali inaweza kutoa tathmini ya urejeshwaji wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa Vikundi vya Akinamama, Vijana, na Watu Wenye Ulemavu katika kipindi cha angalau miaka mitatu iliyopita?

Supplementary Question 2

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa kanuni ya 10(3) ya kifungu 37A cha Sura ya 290 ya Fedha za Serikali za Mitaa inayohusu asilimia 10; imeitaka Mamlaka ya Serikali za Mitaa kukabiliana na mkopaji namna bora ya kurudisha fedha zile za mkopo. Je, Serikali haioni kwamba Kanuni hii inatoa loophole kwa Watendaji kuingiza mambo kinyume cha utaratibu na hawaoni haja kuweka muda wa marejesho kulingana na kiwango cha fedha ambacho kikundi kile kitakuwa kimekopa? Nashukuru sana.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kanuni ya Fedha ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Kanuni ile inayoelekeza mikopo ya asilimia 10 imeweka nafasi ya Watendaji katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kukubaliana na vikundi vya ujasiriamali kuhusu utaratibu na muda wa marejesho ya mikopo hiyo. Dhamira yake ilikuwa, kwa kuwa mazingira haya ya wakopaji yanatofautiana sehemu moja na nyingine, lakini pia uwezo wa vikundi kurejesha unatofautiana kutoka kikundi kimoja na kikundi kingine, kwa hiyo, tunapokea ushauri wake. Tutafanya tathmini kuona uwezekano wa kuweka standard ya muda wa marejesho kwa kiasi fulani na pia tutaboresha njia hiyo kuhakikisha kwamba zile fedha hazipotei. Ahsante. (Makofi)

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali inaweza kutoa tathmini ya urejeshwaji wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa Vikundi vya Akinamama, Vijana, na Watu Wenye Ulemavu katika kipindi cha angalau miaka mitatu iliyopita?

Supplementary Question 3

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba hizo pesa za 10% katika Halmashauri zote nchini Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo CAG ametoa ripoti ya upotevu wa fedha hizo; haoni sasa ni wakati wa Serikali kusimamia fedha hizo zinazokopeshwa kwa vikundi zinarudi kwenye Halmashauri na zinakopesha tena vikundi vingine vingine?Ahsante kwa kunisikiliza.

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba


kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, bondia mwenzangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Ndugange kwa namna anavyojibu maswali vizuri na kwa ufasaha. Niendelee kumshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kunipa Naibu Mawaziri ambao tunashirikiana vizuri katika kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunafanya tathmini nzima ya 10% ambazo zinaenda kwa vijana, akina mama na ndugu zetu, watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, concern ambayo Mheshimiwa Sophia Mwakagenda ameisema, zikiwemo hoja za CAG, ni sehemu ya uchambuzi huu. Kama nilivyosema, baada ya kufanya uchambuzi, tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge ili mwelekeo wa matumizi ya fedha za 10% uweze kuwa na tija na matarajio ambayo wananchi wetu pamoja na Bunge hili tutayapata. Nakushukuru. (Makofi)

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali inaweza kutoa tathmini ya urejeshwaji wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa Vikundi vya Akinamama, Vijana, na Watu Wenye Ulemavu katika kipindi cha angalau miaka mitatu iliyopita?

Supplementary Question 4

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, majibu yanatuonesha kwamba yapo malalamiko mengi sana ya fedha hizi takribani shilingi bilioni 60 ambazo zinarudi kila mwaka zinapatikana kutokea kwenye fungu hili la 10% na mifano imeoneshwa; Dar es Salaam kwenye Wilaya mojawapo tayari kuna ubadhirifu mkubwa sana wa fedha hizi: -

Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kupeleka ukaguzi maalum kwa nchi nzima ili tupate tathmini ya kweli? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya maeneo nchini kote kuhusiana na matumizi ya fedha za 10% na Serikali kama ambavyo Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Bashungwa ametoa maelezo mwanzoni, ni kwamba tunafanya tathmini ya kuona wapi kuna mafanikio, maeneo gani yana changamoto, na changamoto ni zipi; ili sasa baada ya tathmini hiyo, tuwe na direction ambayo itatuwezesha kuwa na fedha ambazo zinaleta tija kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na sababu ya kutazama uwezekano wa kufanya ukaguzi maalum tutalifanya kwa sababu kazi ya Serikali ni kudhibiti fedha hizo ili ziweze kuleta tija kwa watarajiwa. Kwa hiyo, tumelichukua wazo hilo na tutaendelea kulifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)