Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Primary Question

MHE. DEO K. SANGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kilomita sita ya barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Makambako?

Supplementary Question 1

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri ambayo imeifanya na hasa kwa barabara hizi kilomita sita na kilometa 3.5 kama alivyosema kwenye jibu la msingi zimejengwa. Kabla sijakwenda kwenda kwenye swali, nimshukuru Waziri wa TAMISEMI, Ndugu yetu Bashungwa alipopita kwenye kazi zake katika Mkoa wetu wa Njombe alikuta tuna maafa pale katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, akatoa fedha zake mfukoni kuwasaidia wahanga wale, namshukuru sana sana na wananchi wanakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, kwa kuwa kazi ni nzuri na kwa kuwa kilometa zilizobaki ni kilometa 2.5. Ni lini wataanza kuzijenga ili wananchi wa Makambako wawe na imani kubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini katika kilomita hizo zilizobaki zitamaliziwa kujengwa?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa moja ya jitihada kubwa ambayo Mheshimiwa Mbunge anaifanya ni kuhakikisha hii ahadi ya Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kilomita sita inakamilika na kilomita zilizobaki ni 2.5 ambazo sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tunapaswa kuzitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishazungumza na Mheshimiwa Mbunge, tulishazungumza na TARURA Mkoa wa Njombe kuwaambia kwamba barabara hizi ziwekwe katika mpango wa kila mwaka wa fedha ili hizi kilometa 2.5 tuzimalize kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025. Kwa hiyo, matarajio yetu kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 barabara hizi kilometa 2.5 zitakuwa zimeshakamika. Ahsante sana.

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEO K. SANGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kilomita sita ya barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Makambako?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo. Nauliza kuwa, je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga barabara ya kuanzia Gairo hadi Kata za Chagongwe na Nongwe kwa kiwango cha lami? Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa ahadi ambayo imeahidiwa katika Awamu ya Nne ya Serikali na anataka Awamu ya Sita tuikamilishe kwa wakati. Jibu moja kubwa la msingi ambalo Wabunge wote wanapaswa kufahamu ni kwamba Ahadi zote za Viongozi, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumeziainisha na zote zinathamani halisi ya fedha ambayo tumeziwekea kila ahadi, kama ni barabara, maji, Kituo cha Afya zote zipo katika vitabu vyetu na utekelezaji wake ni kwamba tumekuwa tukitenga fedha katika kila mwaka wa fedha. Kwa hiyo, hata hili la Awamu ya Nne na lenyewe lipo katika utekelezaji huo. Kwa hiyo, ninachoweza kukisema ni kwamba, litatekelezwa kulingana na fedha tunavyokuwa tunazipata kila wakati ili kuhakikisha tunamaliza ahadi zote za viongozi zilizopo. (Makofi)

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. DEO K. SANGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kilomita sita ya barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Makambako?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Kwa kuwa nimeshatoa machozi ya kutosha mbele ya viongozi wetu wakuu kuhusiana na uhitaji wa lami kwenye barabara zetu tatu fupi pale Vunjo ambazo ni Barabara ya Uchira-Kisomachi-Kolalie, Barabara ya Pofo-Mandaka-Kilema na Barabara ya Himo Sokoni- Lotima. Nataka nimwombe Waziri kama ataridhia kuambatana nami kwenda kutembelea barabara hizi ili aweze kuona uhalisia wa hadhi ya barabara hizi na kero ambazo wananchi wanapata? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu kwa kifupi swali la Mheshimiwa Dkt. Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari kuambatana na Mbunge kwenda kuziona hizo barabara ili tuhakikishe kwamba tunawapatia ufumbuzi wa kudumu. Ahsante. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEO K. SANGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kilomita sita ya barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Makambako?

Supplementary Question 4

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama unavyojua Mji wa Bunda unakua kwa kasi na Serikali ya Awamu ya Nne iliji-commit kujenga kilomita 10 katika mitaa ya Mji wa Bunda na hasa ukizingatia sasa kuna barabara moja tu ya lami kutoka pale Mjini kwenda Bomani. Nataka nijue ni lini Serikali itakamilisha ahadi hii ya kilomita 10 ili Mji wa Bunda ufanane na Miji mingine kwa lami? Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu awali kwamba ahadi zote viongozi zipo na tunachokifanya sasa hivi zote zimeshatengewa fedha yaani kwa maana thamani halisi. Kwa hiyo, tunavyopata fedha ndipo ambavyo tunatekeleza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nimwahidi najua Mji wa Bunda na bahati nzuri na mimi mwenyewe nimefika, kwa hiyo ninachokiahidi ni kwamba zile barabara zitajengwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hizo. Ahsante sana. (Makofi)