Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha kuvipatia umeme wa REA Vitongoji na Vijiji vilivyobaki katika Jimbo la Mbarali?

Supplementary Question 1

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa katika Wilaya ya Mbarali kuna uzalishaji mkubwa wa mpunga na viwanda vingi vya kuchakata mazao ya mpunga, lakini umeme ni hafifu kwa maana ni low voltage.

Je, Serikali iko tayari kufunga transformer kubwa ili kusudi kuwasaidia wananchi wa Mbarali ambao wana bidii katika kuzalisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kutokana na kwamba Serikali hivi karibuni ilitangaza bei mpya na bei hii ni kwa ajili ya maeneo ya mijini na maeneo ya vijijini bado bei itabaki ile ile ya shilingi 27,000/= kwa umeme unaosambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini; hata hivyo, sheria inayotumika kuamua kwamba hili ni eneo la mji, kwa maana ya Sheria ya Urban Planning Act. No. 8 ya Mwaka 2007, inasema kwamba eneo litahesabika kuwa ni mji ikiwa lina maduka kuanzia 20 na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo kama Mafinga Mjini, ambapo maeneo kama Vijiji Ndolezi, Makalala, katika Sheria hii ya Serikali za Mitaa inahesabika kwamba hilo ni eneo la mji, lakini maisha halisi ya wananchi ni ya kijijini. Kwa mfano, hapa Dodoma kuna Kata 41; Kata za mjini ni 15 tu, the rest maisha yao ni ya kijijini kabisa: Je, Serikali ina mpango gani kuangalia maisha halisi ya wananchi ambao pamoja na kuwa inasemekana wapo mjini kutokana sheria hii, lakini maisha yao ni ya kijijini ili nao waweze kulipa shilingi 27,000? (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cosato Chumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la kwanza, ni kweli tunalo tatizo la voltage katika maeneo mengi hapa nchini na tayari Serikali imechukua jitihada za makusudi kabisa za kufanya kitu kinachoitwa voltage improvement kwa kuongeza vituo vya kupooza umeme na kufunga mitambo inayoitwa Auto Voltage Regulators kwenye maeneo mbalimbali ili kuweza kufikisha umeme mwingi zaidi kwa wanaohitaji. Kwa hiyo, eneo la Mbarali ni mojawapo ambalo lipo katika mpango huo na hiyo kazi itafanyika. Namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvumilia kidogo na huduma nzuri itafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, kama alivyosema yeye mwenyewe, sheria inaeleza kama alivyosema; na sheria tulitunga sisi wenyewe hapa Bungeni; lakini uhalisia ni vyema ukaangaliwa na sisi kama tulivyosema siku zilizopita, jambo hili tumelichukua na tumewakabidhi wenzetu wa TANESCO waangalie upya uhalisia unavyosema ili pamoja na sheria kuwepo, tuone namna ambavyo sheria hii itawatumikia wananchi ambapo ndiyo hasa tuliitengeza ili iwalinde wao na kuwahakikishia huduma nzuri. Nashukuru. (Makofi)

Name

George Ranwell Mwenisongole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha kuvipatia umeme wa REA Vitongoji na Vijiji vilivyobaki katika Jimbo la Mbarali?

Supplementary Question 2

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuweka bayana bei ya umeme vijijini ni shilingi 27,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni hili; hapa katikati kuomeongezwa bei ya umeme mijini kutoka shilingi 177,000 mpaka shilingi 320,000.

Je, Serikali haini kama hiyo bei kwa watu wanaoishi mijiji nao bado ni kubwa sana? Kwa nini isirudi bei ya awali ya shilingi 177,000 ili wananchi wa mijini nao kwa wingi wapate nafasi ya kuunganishiwa umeme? (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanisongole kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu niliyoyatoa kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Cosato Chumi, kimsingi ndiyo yanayokwenda mpaka kwenye swali la Mheshimiwa Mwenisongole. Tunakwenda kuangalia kwa ujumla maeneo ni yapi na gharama ipi iweze kutumika katika maeneo hayo ili kuwahakikishia wananchi wote huduma hiyo kwa gharama nafuu ambayo wataiweza. (Makofi)

Name

Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha kuvipatia umeme wa REA Vitongoji na Vijiji vilivyobaki katika Jimbo la Mbarali?

Supplementary Question 3

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Temeke, hasa Jimbo la Temeke, naomba kuuliza: Je, ni lini sasa umeme utakamilika kwenye Jimbo letu la Temeke? Kwani hata kabla ya mgawo tulikuwa hatupati umeme; na sasa pia hatupati umeme kwa masaa mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Temeke wanataka kujua; je, ni lini sasa kutakuwa na ukamilifu wa umeme kwenye Jimbo letu la Temeke? Ahsante. (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa kuna outage kadhaa ndani ya Jimbo la Temeke. Sababu ya kukatika kwa umeme mojawapo ilikuwa inasababishwa na ujenzi wa barabara ya BRT ambapo tumekuwa tuna schedule ya kukata umeme katika siku ya Jumanne na Alhamisi kwa ajili ya kupisha uhamishaji wa nguzo kwa ajili ya utengenezaji wa barabara hii. Pia zoezi hilo limekuwa likiendana pamoja na kuhamisha ile miundombinu ya umeme kuipitisha chini ya ile barabara na kuweza kuweka mazingira mazuri ambayo yatakuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linakwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya umeme katika Jimbo la Temeke na mkoa mzima wa Dar es Salaam kwa kujenga vituo vya kupoozea umeme na kuviongeza nguvu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika muda mfupi ujao kama nilivyojibu juzi, kwamba tutakuwa tumeweka vizuri mazingira ya umeme kwenye Mkoa wetu wa Dar es Salaam na katika maeneo mengine kwa kurekebisha miundombinu mbalimbali. (Makofi)