Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuja na mpango mkakati wa kuwezesha NGOs kupata rasilimali fedha kupitia njia mbalimbali ikiwemo ruzuku katika maeneo mahsusi kama ambavyo inafanyika kwa Vyama vya Siasa, hasa baada ya uamuzi wa Serikali kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambayo inahusisha Asasi za Kiraia katika malengo yake?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nami niungane na Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya sekta ya Asasi za Kiraia, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Wizara hii mpya mahususi ambayo inalenga kusimamia masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, na kwa kuwa tunafahamu sisi waswahili tunasema anayemlipa mpiga zumali ndio anayechagua wimbo, sasa kwa mustakabali huo na kwa kutambua kwamba NGOs nyingi zinapata fedha ambazo zimetengwa na Serikali za nje; je, Serikali haioni ipo haja ya kuona namna gani ambavyo pia itatenga fedha kwa ajili ya NGOs za ndani ili kuepusha baadhi ya NGOs kwenda na kufanya kazi ambazo zinakwenda kinyume na maadili na malengo ya Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa hali ya sasa ipo changamoto kubwa sana kwa upande wa TRA na namna ambavyo inaangalia hizi NGOs. Pale ambapo inatokea NGO inapata rasilimali fedha na inakwenda kutekeleza mpango ule kutoka mwaka mmoja kwenda wa pili, TRA wanatoza kodi ya mapato kwenye hizi NGOs kwenye zile fedha ambazo zinakuwa zimebaki mwisho wa mwaka, lakini zinakwenda kutekeleza mradi mwaka unaofuata. Nwa kwa mantiki hiyo TRA inafanya hivyo kana kwamba NGOs zinafanya biashara wakati hazifanyi biashara, zinatoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali haioni haja ya kuleta hizi sheria, kanuni na haya maelezo mbalimbali ambayo yanatoa fursa kwa TRA kufanya hivyo ili iletwe Bungeni ifanyiwe maboresho ili kuimarisha mazingira wezeshi kwa hizi Asasi za Kiraia ili ziweze kuendelea kufanya kazi kwa tija na kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii ambayo kimsingi ili Wizara hii itekeleze malengo yake ni lazima ifanye kazi kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa nyingine niweze kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Neema Lugangira.

Mheshimwa Mwenyekiti, nianze na sehemu ya kwanza, kwamba Serikali ina mpango wa kutoa fedha kwa ajili ya Mashirika haya Yasiyo ya Kiserikali. Niseme kwamba Serikali imekuwa ikifanya hivyo tangu miaka ya nyuma kwenye baadhi ya taasisi chache ile zile NGOs ziweze kuchangia maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni CCBRT, ile ni hospitali yetu ambayo inawanufaisha akinamama na watoto na watu wengine wenye magonjwa mbalimbali ya ulemavu. Imekuwa ikipeleka fedha kule tangu miaka ya 2000 na
kikubwa katika mwelekeo huo, pamoja na hili andiko tunalolifanyia kazi, bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali inajielekeza kuanza kutekeleza mpango wa ruzuku kwenye baadhi ya hizo NGOs zitakazokuwa zimeonekana zina vigezo na tutawasilisha kwenye kipindi cha bajeti, mtaweza kuona mwelekeo huo wa Serikali.

Mheshimwa Mwenyekiti, aidha, katika kipengele kingine cha pili cha swali, maboresho ya kanuni na sheria ili kuzifanya hizi NGOs zetu ziweze kufanya kazi kwa kujiamini na kuwa na uendelevu baadaye. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu alishaelekeza, andiko limeanza kuandikwa lakini tayari tumeanza kutekeleza kupata maoni kutoka kwenye NGOs mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilifanyika kikao Arusha; Mashirika 200 yalikaa yakatoa maoni na tarehe 5, hapa Dodoma kinafanyika kikao kingine, NGOs nyingine zimealikwa, zitakuja kutoa maoni na baadaye tunakwenda Mwanza Kanda ya Ziwa, tunafunga. Yale maoni ndiyo tutayafanyia kazi na kuyachakata kuona tunaendaje katika suala zima la kuhakikisha sheria na kanuni zote zilizopo zilizopitwa na wakati ziweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo hatua tuliyonayo. Lengo kubwa la Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona NGOs hizi zilizo ndani yetu zinapunguza utegemezi, zinakaa vizuri na kushiriki kuwa wanufaika wa Serikali yao kupitia National Cake. Ahsante. (Makofi)

Name

Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuja na mpango mkakati wa kuwezesha NGOs kupata rasilimali fedha kupitia njia mbalimbali ikiwemo ruzuku katika maeneo mahsusi kama ambavyo inafanyika kwa Vyama vya Siasa, hasa baada ya uamuzi wa Serikali kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambayo inahusisha Asasi za Kiraia katika malengo yake?

Supplementary Question 2

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. kwa kunipa nafasi. Pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Waziri, moja ya changamoto kubwa anayoanza nayo kwenye Wizara hii ni mauaji ambayo yanaendelea katika jamii hasa katika yanayosababishwa na jinsia, ikiwepo wanawake kuwaua wanaume, wanaume kuwaua wanawake, watoto kuwaua wazazi wao kwa ajili ya kupata mali: -

Je, Wizara imejipangaje sasa kabla ya kufikia kwenye vyombo vya usalama kuhakikisha kwamba wanazuia hali hii inayoendelea katika jamii?

Name

Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, kuhusu vitendo vya ukatili vinavyoendelea kwenye jamii yetu. Ni kwamba tunao mkakati wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto mpango wa Taifa uliozinduliwa mwaka 2017/2018 na unakwenda mpaka mwaka 2021/2022, ambao umeandaa Kamati kwenye ngazi ya Kijiji zinazoongozwa na Wenyeviti wa Serikali za Kijiji, Mtaa, Kata, Halmashauri mpaka Taifa na mkoa ukiwemo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hizi tumeshazipelekea maelekezo na leo tunakwenda kuazimisha Siku ya Kupinga Ukeketaji tarehe 6 Februari, 2022. Hii ni Fursa ya kuziamsha hizi Kamati zote zifanye kazi yake. Zikitekeleza majukumu yake yaliyomo kwenye huo mwongozo, tutaweza kudhibiti ukatili huo unaotokea kwenye jamii kwa kuona viashiria husika na kuvitolea taarifa katika vyombo husika vinavyoshughulika na uhalifu.

Name

Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuja na mpango mkakati wa kuwezesha NGOs kupata rasilimali fedha kupitia njia mbalimbali ikiwemo ruzuku katika maeneo mahsusi kama ambavyo inafanyika kwa Vyama vya Siasa, hasa baada ya uamuzi wa Serikali kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambayo inahusisha Asasi za Kiraia katika malengo yake?

Supplementary Question 3

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii ya swali la nyongeza. Licha ya Serikali kuleta Wizara hii maalum kabisa ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, naomba kufahamu ni nini mpango wa Serikali kuajiri Afisa Maendeleo Jamii Kata na Afisa Maendeleo Jamii wa Vijiji ambao ni wachache sana ili wanawake wetu waweze kufikiwa na kuweza kukua kiuchumi? (Makofi)

Name

Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Ulenge. Serikali inatambua upungufu wa watumishi hawa, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii. Kadri ya asilimia 96 kwenye Kata zetu hazina hawa watu; na kwenye bajeti ya mwaka huu tutapanga kuanza kupunguza upungufu huo kwa kushirikiana na wadau wetu.