Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Primary Question

MHE. MRISHO S. GAMBO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanapata malipo kama Madiwani na Wabunge kutokana na majukumu mazito wanayoyafanya ikiwemo ufuatiliaji wa malipo ya Kodi ya Majengo?

Supplementary Question 1

MHE. MRISHO S. GAMBO: Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba, Wenyeviti wa Serikali za Vijiji ndio msingi wa Serikali za Mitaa katika nchi yetu, na kwamba, maelekezo mengi ya Serikali kutoka ngazi ya TAMISEMI, mikoa, wilaya na halmashauri yanapelekwa ngazi za chini na wao ndio wanazisimamia.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, Jiji letu la Arusha limeongoza kwa mapato kwenye hii robo ya kwanza. Na ukizingatia kwamba, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/ 2022 tulitenga fedha kwa ajili ya kulipa shilingi elfu 50 kwa kila Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na bado halmashauri yetu haifanyi hivyo. Je, ni nini kauli ya Serikali kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhusiana na changamoto hii ambayo inawakumba Wenyeviti wa halmashauri?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ukizingatia kwamba, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulifanyika mwaka 2019 na mpaka sasa Wenyeviti wa Serikali za mitaa hawajapatiwa semina, hawapewi stationaries zozote, hawajapewa vitambulisho na hata bendera kwenye maeneo yao pia hazijapatikana na hasa ukizingatia pia hawana hata ofisi. Inabidi wachangishe kwa watu waende wakaombe hela kwa wadau, ili mwisho wa siku waweze kulipia ofisi.

Mheshimiwa Spika, hatuoni kwa kufanya namna hiyo tunawaweka kwanye mazingira ya rushwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa? Je, nini kauli ya Serikali kwenye kutoa heshima kwenye ofisi za Serikali za mitaa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, viongozi hawa Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji wanafanya kazi kubwa sana katika kusukuma maendeleo ya nchi yetu. Na ndio maana katika jibu la msingi nimeeleza namna ambavyo Serikali imeendelea kutathmini na kuweka njia bora zaidi ya kuhakikisha tunawawezesha Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kupata posho zao kila mwezi, lakini kwa sababu halmashauri zetu hazijawa na uwezo wa kutosha tunaendelea kuona namna gani tutaboresha mfumo huu, ili waweze kupata posho hizo.

Mheshimiwa Spika, lakini Serikali ilitoa mwongozo kwamba, kila halmashauri itenge fedha kulingana na uwezo wa mapato yake na iweze kuwalipa posho hizo Wenyeviti wa Mitaa.

Kwa hiyo, naomba nitoe maelekezo kwa Halmashauri ya Arusha na halmashauri nyingi zote nchini, zile ambazo zimetenga bajeti na zina uwezo wa kukusanya fedha hizo ziendelee kuwalipa Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji kwa kadiri ya bajeti ambazo wamezitenga.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, Serikali imeendelea kutoa fedha ambazo ni fidia ya vyanzo vilivyofutwa (GPG), kwa maana ya asilimia 20 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa ofisi za vijiji na mitaa. Utaratibu huu unaendelea ili kuwezesha kuweza kununua shajara, lakini na matumizi mengine ya kila siku. Ahsante.