Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Tanzania ina idadi ya watu takribani milioni hamsini na tano wenye madaraja tofauti ya uchumi: - Je, katika idadi hiyo Tanzania ina mabilionea wangapi?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu haya ya Serikali ambayo kwa kweli yanaonyesha bado tuko nyuma sana, maana kati ya 140,000 kwa Afrika sisi tuna 5,000 sawa na asilimia 4.2: Sasa ni upi mkakati wa Serikali katika kuhuisha sera na sheria ambazo wakati mwingine ndiyo zinazokuwa kikwako katika ukuaji wa mitaji wa kibiashara na uwekezaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Mheshimiwa Waziri ametaja sekta mbalimbali ambazo mabilionea hawa aliowataja wanatoka, lakini kwa masikitiko makubwa hakuna hata mmoja anayetokana na Sekta ya Kilimo na Mifugo na Uvuvi. Haoni kwamba kwa stahili hiyo wakulima, wafugaji na wavuvi wataendelea kuwa wasindikizaji katika eneo zima hili la kiuwekezaji wa mitaji? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Shangazi kwa swali lake nzuri. Nampongeza kwa jana niliambiwa alikuwa anashabikia moja ya timu iliyoshinda kwa mbinde sana. Taarifa alizonipa Mkuchika anasema, basi timu yake isingeshinda, mpaka sasa mpira ule ungekuwa bado unaendelea kuchezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabilionea hawa tuliotaja, tumewataja tu kwa mfano. Tumetoa tu mifano ya baadhi ya sekta ambazo tumeweza kuziainisha, lakini haina maana kwamba kwenye Sekta ya Kilimo na Mifugo hakuna mabilionea. Hata Sekta ya Mifugo na Sekta ya Kilimo wapo mabilionea na takribani kila mkoa kwenye sekta hiyo ya kilimo mabilionea wapo kuanzia ngazi zote; kuanzia kwenye kulima kwenyewe wapo ambao wako ngazi ya processing ambazo ziko ngazi ya viwanda, lakini wapo pia wa ngazi ya export. Kwa hiyo, hii tulitolea tu mifano ya baadhi ya maeneo ambayo yapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta nyingine zipo ambazo hatujazitaja kwa kiwango kikubwa na zenyewe zina mabilionea ambao wako. Kwa mfano, King Musukuma pamoja na wengine ambao na wenyewe wapo katika makundi yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kwamba tuna sera gani? Serikali ina sera na moja ya maeneo ambayo tumeyapa uzito mkubwa ni kutengeneza mazingira bora kabisa ya ufanyaji biashara ambapo tunahamisha watu kutoka kundi moja la kipato kwenda kipato kingine na mkakati huo unaanza na biashara kuanzia zile zilizo ndogo kwenda biashara zilizo kubwa na zilizo kubwa kwenda kwenye ngazi ya mabilionea ili Tanzania iweze kuwa na mabilionea wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tamko lilitolewa siku siyo nyingi sana, hata Wabunge wanakaribishwa waungane na King Musukuma kwenye kundi lile la mabilionea ili waendelee kuongozwa kwa mfano kwa wananchi hao wanaowaongoza. (Kicheko/Makofi)

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Tanzania ina idadi ya watu takribani milioni hamsini na tano wenye madaraja tofauti ya uchumi: - Je, katika idadi hiyo Tanzania ina mabilionea wangapi?

Supplementary Question 2

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, ili mtu aweze kuwa bilionea, wengi wanaanza katika biashara ndogo ndogo. Kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema, unaanza na biashara ndogo ndogo, unafika kati na hatimaye unakuwa mkubwa ukiacha wale ambao wanarithi. Sasa imekuwa ni utamaduni wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwafukuza Wamachinga ambao wanatumia kipato chao kidogo kwenye maeneo yao ya biashara na kuwapeleka pembezoni na maeneo ambayo hayajaandaliwa na mazingira ambayo siyo wezeshi kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuthibitisha kwamba Serikali haijali kundi hili la wafanyabiashara wadogo wadogo, hapa kwenye mpango ambao Waziri ameusoma jana, hakuna maeneo ambayo anazungumza atawapanga vipi hawa vijana wetu? (Makofi)

Sasa nataka Waziri aniambie, kwa kuwa anatambua ili uweze kuwa milionea na hatimaye bilionea, lazima uanzie chini; na kwa kuwa anatambua...

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Halima.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuja, ninakuja. Serikali...

NAIBU SPIKA: Aah, uliza swali, kwa sababu umepewa nyongeza.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina uwezo wa kuajiri asilimia mbili tu: Je, sasa ana mpango gani rasmi wa kuingiza eneo hili muhimu katika Mpango wetu ambao tutakuja kuufanyia kazi Januari, kwa kundi hili kubwa la vijana ambalo sasa hivi wanahangaika mtaani?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Halima kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali inayowajali sana wafanyabiashara wadogo. Mfano na uthibitisho mmoja ni kwamba mabilionea wote walioko katika nchi hii, ni zao la Chama cha Mapinduzi kwa sababu hakuna chama kingine kimewahi kuongoza. Kwa hiyo, mabilionea wote unaowaona katika nchi hii na wengine wame-spill over mpaka nchi za SADC na nchi nyingine kwa ukombozi wa Chama cha Mapinduzi. Ni zao la Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hawa ambao wako hapa, amesema Mpango haujasema watapangwa vipi? Mpango wa nani akae wapi, ni suala la kisekta ambalo litafanywa na Serikali za Mitaa. Kwa upande wa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Rais ana mpango mzuri sana na kundi hili ambalo Mheshimiwa Halima amelisema la wafanyabiashara wadogo wadogo. Kwa sababu ndiyo kwanza bado tunaendelea kuchambua huu Mpango, tutawapa undani wake Waheshimiwa Wabunge, ni kwa sababu tu hatukusema kwa kuwa bado tuko kwenye mazungumzo ya awali. Hata hivi tunavyoongea, tunaendelea kuongea na wenzetu wa Benki ya Dunia, lakini pia tunaendelea kuongea ndani ya Serikali kutengeneza utaratibu ambalo lengo lake kubwa hasa ni kuwafanya hawa ambao tumewataja kwa jina la Wamachinga waweze ku- graduate, wapige hatua kwenda kwenye hatua nyingine inayofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema hii mtaiona katika Mpango huu na mtaona katika bajeti hii inayokuja na wenyewe Wamachinga watakuwa mashahidi kwamba kumbe kweli huu Mpango ulikuwa ni mwema ambapo umetufanya tu-graduate. Kwa sababu katika hali ya kawaida, hakuna Mmachinga anayetaka aendelee kuwa Machinga katika maisha yake yote. Hata wao wanataka siku moja wawe kama GSM wafanye mambo ya kweli na yanayoonekana katika nchi hii. Ahsante. (Makofi)