Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo sugu la soko la zao la tumbaku nchini?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni pale ambapo Serikali imesema kwamba mwaka huu kulikuwa na kampuni nane za wazawa zimeingia mikataba na wakulima. Hadi ninaposimama hapa Bungeni mwaka huu kumekuwa na kuvunja rekodi ya kuwakopa wakulima maana yake wameuza tumbaku yao mwezi wa Tano, lakini hadi ninaposimama Bungeni hapa asilimia zaidi ya 50 ya wakulima hasa waliouza tumbaku yao kwenye kampuni hizo za wazawa hawajalipwa. Hawajalipwa kwa sababu kampuni hizo ndogo zimepata shida na changamoto katika kuuza tumbaku hiyo kwenye soko la dunia. Walikuwa wanauza kupitia Zambia, wamefungiwa huko. Walikuwa wanauza kupitia Malawi, wamefungiwa huko. Sasa je, Serikali haioni hasa kama Waziri, haioni umuhimu wa kukutana na hizo kampuni nane ili kuona namna ya kuwasaidia ili hatimaye nayo yawalipe wakulima haraka iwezekanavyo? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa mujibu wa sheria, zao la tumbaku linaendelezwa na kusimamiwa na Bodi ya Tumbaku. Tangu mwaka jana Bodi ya Tumbaku imemaliza muda wake, hadi sasa hivi inafanya kazi zake kinyume cha sheria. Hivi Serikali haioni kwamba inatakiwa iteue Bodi ya Tumbaku kesho? Ahsante sana.

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, Wizara ya Kilimo imeshakutana na kampuni zote nane za Kitanzania zinazonunua tumbaku na ningeomba tu-acknowledge kazi iliyofanywa na kampuni hizi za Kitanzania katika kununua tumbaku. Tumbaku yote iliyonunuliwa mpaka msimu unakwisha ni jumla ya bilioni 86. Fedha zilizolipwa mpaka sasa ni bilioni 82, kwa hiyo, sio sahihi kwamba zaidi ya asilimia 50 kwamba wakulima hawajalipwa. Tuna-acknowledge fedha ambayo haijalipwa ya wakulima mpaka sasa imebaki shilingi bilioni nne.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwenye eneo hili tumbaku hii iliyonunuliwa na naomba Bunge lako Tukufu lifahamu kabla ya kuleta kampuni za Kitanzania katika mfumo wa ununuzi wa tumbaku pamoja na grade zaidi ya 60 za tumbaku, kulikuwa kuna tumbaku inaitwa reject inayotupwa ambayo mkulima anaitupa shambani. Ni kampuni hizi za Kitanzania ndiyo zimeenda kuinunua mpaka tumbaku inayoitwa reject na kwa mwaka huu hakuna tumbaku iliyobaki mikononi mwa wakulima. Kunapokuwa na success story, tu-acknowledge na hili ni jambo jema. Kwa miaka mingi sekta hii imekuwa kwenye dominance ya kampuni mbili tu. Tumeingiza kampuni za Kitanzania against all efforts za international market ambazo zilituzuia.

Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo yaliyobaki na tumbaku iliyoko Malawi na Zambia, Balozi Simba aliyeko Zambia ameshafanya jitihada kwa sababu walio-block tumbaku yetu isinunuliwe Zambia ni hizi hizi kampuni kubwa zilizoko ndani ya nchi, zimetumia subsidiary companies zao kule nchi kuzuia tumbaku yetu isinunuliwe. Tatizo hili tumeli- resolve, tuko kwenye hatua za mwisho. Tumeongea na Benki ya CRDB na NMB watatoa fedha ili kampuni hizi zimalizie bilioni nne iliyobaki ambayo haijalipwa kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie Bunge lako Tukufu kusema tutaendelea ku-support kampuni za Watanzania kununua green tobacco na kui-export kwa sababu tumbaku haiwezi kugeuka kuwa chapati.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kuhusu suala la Bodi. Bodi ya Tumbaku imemaliza muda wake, ni kweli. Sisi kama Wizara tumeshapeleka mapendekezo vetting inaendelea na tumeshaomba kwa Mheshimiwa Rais ili aweze kumteua Mwenyekiti. Iko kwenye hatua za mwisho na ni interest yetu sisi kama Wizara kuhakikisha Bodi ya Tumbaku inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria. Sasa hivi Bodi haipo, Mkurugenzi anafanya kazi chini ya Katibu Mkuu kwa mujibu wa sheria.

Kwa hiyo, Bodi ya Tumbaku inafanya kazi chini ya DG na anaripoti moja kwa moja kwa Katibu Mkuu. Tumeshapeleka mapendekezo na tunaendelea kufuatilia Serikalini.