Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: - Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu usalama wa Askari ambao wakati mwingine huvamiwa na kujeruhiwa pamoja na kuporwa silaha wakati wakiwa kazini?

Supplementary Question 1

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na yanaleta faida kwa Watanzania. Hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uvamizi katika vituo vya Polisi siyo jambo jema, lakini nashukuru Jeshi la Polisi wameweza kudhibiti, lakini suala kama hilo huenda likajirudia. Swali langu linasema hivi: Je, ikitokea wamevamiwa katika vituo vyao na kwa bahati mbaya askari kajeruhiwa au askari kauliwa; familia ile inayomtegemea yule askari ambapo ndio tegemeo lao kimaisha, Serikali inawaambia nini au itawasaidia nini ili waweze kuishi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wanapovamia vituo, lengo kuu ni kupata zile silaha na kuwaathiri Polisi wenyewe walioko kituoni. Je, wakati wanapozungumza au wakati taarifa tunapozipata, baadhi yao wanazipata silaha; wanapokuwa wamezipata zinakuwa katika hali gani? Katika hali ya ubora ule ule wa awali au tayari zimebadilishwa ili wasiweze kuzitambua? Ni hayo tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bi. Fakharia, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa Mjini Zanzibar, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeweka utaratibu maalumu wa askari wake watakapopata mitihani katika harakati za kulinda amani na utulivu wa nchi hii, lakini ni ikiwa imethibitika kwamba mtihani huo umemkuta ama ameupata akiwa katika harakati za kazi zake za kawaida za kiaskari. Kwa hiyo, kuna kanuni ya fidia ya pamoja ya Jeshi la Polisi na Magereza, hiyo hutumika. Katika kanuni hiyo imeelezwa viwango ambavyo huwa mtu anafidiwa kutokana na tatizo lililomkuta; kuna viwango akipata ulemavu, kuna viwango akikatika, na kuna viwango akifa. Kwa hiyo, Serikali kupitia Jeshi, imeweka utaratibu maalumu kupitia hii kanuni ambayo inawapa watu nafasi ya kuweza kupata fidia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine kwamba je, Silaha hizi tunakuwa tumezipata zikiwa zimeharibika au vipi? Silaha hizi zitakavyokuwa, zikiwa zimeharibika, zikiwa nzima, wajibu wetu tukizipata katika matukio ya kihalifu, maana yake ni kuzichukua. Kama itakuwa zimeharibika, maana yake tuna utaratibu wa kuzitengeneza. Ikiwa hazijaharibika, tunaiangalia; kama silaha ile ina kesi, tunaiacha kesi ile iendelee, ikimalizika, silaha ile inarudi Serikalini, inarudi jeshini, tunaendelea kuitumia kwa ajili ya Ulinzi na Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)