Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta Sera ya Ubunifu (Innovation Policy) ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia?

Supplementary Question 1

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba Sera yetu ya Sayansi na Teknolojia ni ya muda mrefu, ya miaka 25 nyuma, lakini vilevile kutokana na suala kwamba mapitio ya sera hii ili yaweze kuleta tija kwenye ubunifu yamekuwa yakichukua muda mrefu, tangu 2012, jambo linalosababisha programu za ubunifu chini ya COSTECH kutokutengewa fungu na kutegemea zaidi ufadhili na hivyo kukosesha vijana fursa nyingi zinazotokana na ubunifu: Je, Serikali haiwezi kutuambia ukomo wa muda wa mapitio haya ya sera ya kwamba yatakamilika lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu tumeambiwa maboresho yamekuwa yanafanyika toka 2012 lakini hadi leo hayajafanyiwa kazi. Tunaomba Wizara ituambie ukomo wa muda wa kufanyia maboresho ili programu za ubunifu ziweze kuwa na tija kwa vijana wa Tanzania. Ahsante. (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Wizara imekuwa ikitenga fedha katika kila bajeti kwa lengo la kuhakikisha kwamba eneo hili la ubunifu linafanyiwa kazi sawa sawa. Nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara imetengeneza mwongozo wa mwaka 2018. Vilevile mwongozo huu tunaendelea kuuboresha mwaka huu, tena tunaendelea kuupitia upya ili kuweka mwongozo huu sawa sawa, nimtoe wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, pia anataka kujua kwamba ni lini Serikali itakamilisha utungaji huu au mapitio haya ya sera? Ndani ya mwaka huu wa fedha tutalifanya hilo na kuhakikisha jambo hili linakaa sawa sawa. Ahsante. (Makofi)