Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali inaweza kuwahakikishia Wananchi wa Moshi Vijijini kuwa barabara za Himo – Kilema, Pofo –Mandaka, Uchira – Kisomachi na Mabogini – Kahe - Chekereni zitawekwa kwenye Bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa lakini kusema ukweli matengenezo yanayofanyika hayatoshelezi kitu. Unafanya matengezo mwezi huu, mwezi ujao mvua kubwa ikinyesha unarudia tena matengenezo. Kusema kweli ahadi ambazo zilitupa ushindi sisi wana-CCM ni ahadi hii ya barabara ya Mandaka – Kilema ambayo Mheshimiwa Rais aliitoa. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze ni lini au anafanya commitment gani kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna taswira kwamba kule Kilimanjaro kuna barabara nzuri. Nataka niwahakikishie wananchi kwamba Kilimanjaro hatuna barabara nzuri, barabara zilizokuwepo ni zile za zamani zilizojengwa na Ushirika na zingine zinaenda mpakani. Sasa namuomba Mheshimiwa anayehusika, Waziri wa TAMISEMI, hajawahi kufika kwenye jimbo langu akaona hali ya usafiri ilivyo ngumu, najua kwamba tumeshapewa hela lakini hazitoshi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Kimei uliza swali lako.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Je, Waziri atakubali kuongozana nami nikamtembeze aone hali ya barabara za Vunjo? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza Mheshimiwa Mbunge amesema anataka kujua commitment ya Serikali juu ya ahadi ya barabara ya Mandaka – Kilema itaanza kujengwa lini kwa kiwango cha lami. Niseme tu kwamba tumelipokea kwa sababu moja ya wajibu wetu ambao tulikuwa tunaufanya hapo awali ilikuwa ni kuchukua ahadi zote za viongozi ili tuziweke katika Mpango. Kwa sababu jana tumepitisha Bajeti Kuu na kuna ongezeko la fedha ambalo limetokea, naamini katika Mpango unaofuata tutakuwa tumeingiza na tutafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili kufika katika Jimbo lake, nimwambie tu hapa katika Bunge lako Tukufu kwamba niko tayari kwa sababu mara baada ya Bunge nitakuwa na ziara ya kuzunguka katika maeneo mbalimbali ikiwemo zile ahadi ambazo nimezitoa hapa kwa Wabunge mbalimbali kufika katika maeneo yao. Kwa hiyo, moja ya eneo ambalo nitafika ni pamoja na Vunjo. Ahsante sana.

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali inaweza kuwahakikishia Wananchi wa Moshi Vijijini kuwa barabara za Himo – Kilema, Pofo –Mandaka, Uchira – Kisomachi na Mabogini – Kahe - Chekereni zitawekwa kwenye Bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini barabara ya Mzumbe – Mgeta itajengwa kwa kiwango cha lami ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Awamu ya Nne? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, alichozungumza hapa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya utekelezaji wa Barabara ya Mzumbe mpaka Mgeta, niseme tu kama nilivyojibu katika jibu la msingi na la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kimei kwamba, na yenyewe tunaiingiza katika mpango, tutaizingatia. Barabara nyingi tutaziongeza katika mpango baada ya kupata ongezeko la fedha hii ambayo jana Bunge lako Tukufu lilipitisha. Ahsante.