Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Michael Constantino Mwakamo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watumishi waliostaafu kupata mafao yao kwa wakati?

Supplementary Question 1

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri yenye mikakati ya Serikali juu ya watumishi wao, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Jimbo la Kibaha na majimbo mengi nchini kuna watumishi ambao wamechelewa kulipwa mafao yao kutokana na waajiri kutokupeleka michango yao kwa wakati. Je, Serikali inawasaidiaje watumishi hao, kwani waajiri wao wamefanya kinyume na utaratibu wa sheria?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuanzia mwaka 2016 mpaka 2020, kulikuwa na maelekezo mbalimbali ya Serikali juu ya upandishwaji wa vyeo, kuna watumishi ambao wamestaafu wakiwa na barua mkononi lakini wameshindwa kulipwa kutokana na barua zao walizo nazo. Lakini pia kuna watumishi walichelewa kupandishwa vyeo kwa sababu ya waajiri kuwasahau kwenye kuingiza kwenye mfumo.

Je, Serikali inawasaidiaje watumishi hao ili waweze kupigiwa hesabu zao kulingana na haki na sheria ilivyo? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Costantino, kwa kufuatilia vizuri sana haki za wananchi wake katika Jimbo la Kibaha Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza ambalo ameuliza ni utaratibu gani tunaochukua kwa wale waajiri ambao wanachelewesha michango lakini pia wanaosababisha fedha zile zisiweze kulipwa kwa wakati, hasa hizi za pensheni. Tumekwisha kuchukua hatua mbalimbali kwa mameneja wa mikoa wa PSSSF, lakini pia hata kwa NSSF kwenye maeneo ambayo tunagundua kwamba kuna uzembe wa ukusanyaji wa michango. Tumekuwa tukichukua hatua kali kwa wakurugenzi wa PSSSF Mikoa, lakini pia complying officers ambao tumekuwa tukiwaagiza kwa wakati wote watoe taarifa ya wadaiwa sugu kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu waajiri wanapochelewesha michango ni pamoja na kukwepa kodi, kwa sababu kuna PAYE kwenye mshahara wa mfanyakazi, kuna fedha inayopaswa kuinia katika Mfuko wa WCF, kuna fedha inayopaswa kulipwa kama Skills Development Levy, lakini vilevile kuna fedha ambayo ni ya mafao ya mfanyakazi, anapomaliza wakati wake wa kazi itamsaidia kwenye maisha yake. Kwa hiyo tunachukua hatua kali, na sheria inaelekeza na tumekuwa tuna kesi mbalimbali ambazo zinaendeshwa kwenye mahakama mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuagiza kwamba mameneja wetu wa mikoa na complying officers waweze kufuatilia michango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kwa kifupi, ni kwamba swali hili liko Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, kwa wafanyakazi ambao ni wa Serikali. Nikuombe Mheshimiwa Mbunge, mimi pamoja na wewe tuweze kuiona ofisi ile na tuweze kufuatilia madai hayo ili waweze kupata haki na stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.