Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - (a) Je, ni Vijiji vingapi vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vimepata umeme wa REA II, Densification na REA III? (b) Je, ni lini vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa swali la nyongeza; lakini vile vile, naomba niishukuru sana Serikali kwa kweli kwa kazi kubwa iliyofanya ya kusambaza umeme vijijini. Ninashukuru sana ya kwamba vijiji 39 vya mwisho sasa navyo kazi imeshaanza ili kukamilisha vijiji vyote vya Wilaya yetu ya Mbeya, Halmashauri ya Mbeya Jimbo la Mbeya Vijijini kupata umeme, nashukuru sana kwa hilo; ingawaje mkandarasi alipewa vijiji 32 kwa hiyo nitamuomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia ili kuoanisha hayo mahesabu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa mradi mkubwa wa Tanzania Zambia Inter-Conector ambao unapita kwenye vijiji vya kata nane za Wilaya ya Mbeya Jimbo la Mbeya Vijijini. Inapita katika Kata za Ulenje, Inyala Maendeleo, Itewe, Swaya, Igale, Iwindi na Bonde la Songwe. Wananchi waliopisha ujenzi wa line hii waliahidiwa kupatiwa fidia tangu mwaka 2018, lakini mpaka leo hii wanasubiria hakuna kinachoendelea, na imekuwa kero kwa vile waliambiwa wasifanye ujenzi wala maendeleo yoyote. Sasa ni lini wananchi hawa watapata fidia yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama unavyojua kupeleka umeme vijijini ni kuchochea uchumi, lakini kumekuwa na mkanganyiko wa tozo kati ya wateja wa line ya three phase na wateja wa line ya single phase. Wateja wa line ya three phase wanatozwa na TANESCO Shilingi 918,000 ambapo REA wanawatoza 139,000.

Je, Serikali ina mpango wa kuoanisha hizo tozo mbili ili kuchochea huo uchumi vijijini na wananchi waweze kulipia laki moja na thelathini na tisa badala ya laki tisa na kumi na mbili? Nashukuru.

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Manase Oran Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake na shukrani alizozitoa kwa Serikali, na mimi kwa niaba yake nizipokee, kwamba Serikali imejitahidi sana kuhakikisha inapeleka umeme vijijini na katika maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji 39 ambavyo anavyo vyote vitapata umeme pamoja na kwamba inawezekana mkandarasi alipewa 32 vya kwanza. Pia niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba hata kama mkandarasi alipewa vijiji pungufu ya vile ambavyo uhalisia vimebaki, katika survey hii ambayo tumewatuma wakandarasi wafanye kwenye maeneo yetu watahakikisha na vile vijiji vingine ambavyo vilibaki au viliachwa vinachukuliwa katika kazi zao na katika adendum za nyongeza za kazi tutakazo wapatia, watavichukua vijiji vyote na kuvifanyia kazi. kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ufuatiliaji wake umefanikiwa na wengine pia umeme utapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la fidia itakayolipwa kwenye mradi mkubwa wa kuunganisha umeme wa grid kutoka Iringa kwenda Mbeya, Tunduma mpaka Sumbawanga, takribani kilomita kama 622, kazi hiyo ya umbembuzi yakinifu imefanyika imekamilika na sasa makabrasha ya ulipaji wa fidia ndiyo yanawasilishwa sasa kwenye ofisi zetu kwa ajili ya uhakiki na kuweza kulipa fidia hiyo. Kwa hiyo bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri aliwasilisha hapa juzi imetenga kiasi cha kuanzia, zaidi shilingi bilioni moja kwa ajili ya malipo ya fidia ya eneo hilo, na tutaanza kulipa fedha hiyo kuanzia kwenye mwezi wa kumi na kuendelea kwa ajili ya kupisha sasa ujenzi wa mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, niombe kutoa maelezo na maelekezo kwa watumishi wenzetu. Serikali imesikia kilio cha Watanzania na tayari ilielekeza kwamba umeme katika maeneo yote utaunganishwa kwa shilingi 27 kwa umeme mdogo. Kwenye maeneo yetu ya vijiji Serikali imetoa msamaha wa kuunganisha line ya nguvu kubwa three phase kwa gharama ya shilingi 139,000 tu. Kwa hiyo, ninawaelekeza watumishi wenzetu wa TANESCO kwamba maeneo yote ya vijijini ambapo either ni TANESCO kapeleka umeme au REA imepeleka umeme, gharama ya kuunganisha umeme wa three phase ni shilingi 139,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo shilingi 912,000/= ni kwenye maeneo mengine ya mijini ambapo mradi wa REA wowote ule haujafika. Kwa hiyo ieleweke wazi kabisa, waheshimiwa Wabunge tunaomba tusaidiane katika usimamizi wa hili. TANESCO akiwa analeta umeme au REA analeta umeme mkubwa gharama yake ni shilingi 132,000 kwenye maeneo yetu ya vijijini. Ahsante.