Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukaimu muda mrefu kwa watumishi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Sekretarieti za Mikoa?

Supplementary Question 1

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Swali la kwanza; kwa kuwa majibu ya Serikali yanathibitisha kuwepo kwa watumishi 332 kukaimu wakiwa na sifa lakini zaidi ya watumishi 1,164 wanakaimu bila sifa yaani hawana kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Sasa na ni ukweli kuwepo kwa viongozi wengi wanaokaimu kunazorotesha utendaji kazi na hivyo kutofikia malengo tarajiwa. Je, ni ipi sasa commitment ya Serikali kuwathibitisha au kuwaondoa watumishi wenye kukaimu zaidi ya miezi sita? (Makofi)

Swali la pili; kwa kuwa mchakato wa uteuzi unachukua muda mrefu sana hata zaidi ya miaka kumi na mfano upo, Katibu Tawala Msaidizi upande wa uchumi na uzalishaji Mkoa wa Kilimanjaro Ofisi ya Mkuu wa Mkoa anakaimu mwaka wa tisa toka 2012. Je, Serikali ipo tayari kutengeneza kanzidata au database ya wale watumishi waliofanyiwa vetting wengi kwa ujumla wao ili waweze kusaidia kupunguza muda ule wa watumishi kukaimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Mtemvu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la kwanza tumekuta kuna changamoto kubwa sana ya waajiri kukaimisha watu wasiokuwa na sifa bila ya kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi kama mwongozo unavyotaka, matokeo yake mtu anakaa kwenye nafasi muda mrefu anakuwa hafanyiwi upekuzi na hivyo kufanya mtu kukaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka mingi. Sasa tayari tulishawaagiza waajiri wote mapema mwaka huu kuleta majina yote ya watu wanaokamimu nafasi zao kwa zaidi ya miaka mitatu ili tuweze kupitia na kuangalia ni wapi wenye sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba tayari tumegundua kuna watumishi 1,164 wasiokuwa na sifa na tunazidi kuwaomba waajiri waweze kuhakikisha wanakaimisha watu wenye sifa lakini vilevile kwa kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Waache kukaimisha kwa sababu anamtaka fulani au fulani mimi naweza nikafanya nae kazi na kumburuza, bali wakaimishe mtu kwa sababu ndie anayetakiwa kuwepo kwenye nafasi hiyo na hiyo itasaidia sana katika upekuzi na kuweza kuwathibitisha watumishi ndani ya miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili la nyongeza Mheshimiwa ameuliza kama tuna kanzidata, sasa tayari tumeshaanza kukusanya taarifa na tumeshapeleka majina zaidi ya 2,300 kwa ajili ya upekuzi ili yawepo na wiki hii tunapeleka tena majina 2,400 kwa ajili ya upekuzi ili tuweze kuwa tuna watu katika kanzidata yetu wenye sifa. Tunapoona mwajiri amekuweka mtu asiye na sifa, Utumishi tutam-post moja kwa moja mwenye sifa ili akashike nafasi hiyo na aweze kuifanya kwa weledi na kuweza kufanya maamuzi. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Wabunge na watumishi wote wale wenye sifa muda si mrefu mtaanza kuwaona na tatizo hili la kukaimu litaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukaimu muda mrefu kwa watumishi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Sekretarieti za Mikoa?

Supplementary Question 2

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa tatizo hili limekuwa kubwa na kwa miaka sasa linazungumzwa na hoja ni hizi hizi na majibu ni haya haya, Serikali haioni umefika wakati wa kutunga sheria iwe ni kosa kumkaimisha mtu kwa muda mrefu. Kwamba tutunge sheria ifikie ukomo kwamba mwisho wa kukaimu ni hapa na baada ya hapa mtu akipitiliza tuchukue hatua ili tuondokane na hili mtu anakaimu miaka Tisa na hakuna mtu anachukuliwa hatua. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishasema awali tatizo hili tunalifahamu na tayari tukishakuwa na kanzidata ya watu wenye sifa hii changamoto inaenda kuisha kwa sababu tutaanza ku-post moja kwa moja watu kwenye nafasi hizi zilizo wazi. Commitment yetu ni kwamba tutaendelea kulifanyia kazi na kuhakikisha kwamba nafasi zote zinazokaimiwa zinakuwa na watu wenye sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilihakikishie Bunge lako kwamba muda si mrefu tutakuwa tayari tuna watu wenye sifa kwenye nafasi zao. Vilevile, nichukue fursa hii kuwaasa na kuwaagiza watumishi wote nchi nzima kuhakikisha ifikapo mwisho wa mwezi huu, walete majina yote ya watu ambao wanakaimu nafasi zao bila kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Vilevile, ifikapo tarehe 30 ya mwezi huu, walete majina ya wote wanaokaimu kwa vibali vya Katibu Mkuu Utumishi ili tuweze kuwafanyia upekuzi na kama wao wanafaa kuwa kwenye nafasi hizo, basi tuwaache hapohapo kwenye nafasi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.