Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: - Je, ni lini ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma utakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Uwanja wa Ndege wa Musoma ni uwanja wa kimkakati, kwa maana Mkoa wetu wa Mara umejaaliwa madini, mbuga za wanyama, makumbusho ya Baba wa Taifa, samaki na biashara mbalimbali,hivyo ungeweza kunufaisha taifa iwapo ungejengwa kwenye kiwango cha kimataifa ili ndege ziweze kutua moja kwa moja tofauti na ilivyosasa hivi watalii wanatua Nairobi au Arusha ndipo wanakuja kwenye mbuga ya Serengeti.

Ningependa kujua sasa, huu ujenzi na ukarabati ambao unaokadiriwa kukamilika ndani ya miezi 18, unatarajia kuwa na run ways pamoja na jengo la abiria la kiwango cha kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, pale Tarime tuna Uwanja mdogo wa Magena ambao hutumiwa na watalii na wale ambao wanakwenda migodi kwa kutua na ndege ndogondogo. Na sasa hivi upo chini ya halmashauri ambapo unaikosesha mapato Serikali, kwa maana imekodiswa kwa makampuni binafsi.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kuchukua uwanja ule ili uje kwenye Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwenye Serikali Kuu ili pia uweze kukarabatiwa na kuweza kutumika na kuongeza kipato cha taifa? (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uwanja wa ndege wa Musoma ni uwanja ambao ni wa kihistoria, ni uwanja ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa hili. Vilevile upo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na viongozi wetu wa mkoa wanausimama pamoja na Wabunge wote wa Mkoa wa Mara. Na mimi pia ni sehemu ya eneo hilo la mkoa huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuhakikishie kwamba uwanja tayari, kulikuwa na eneo limebaki, kama mita 105, ili kila aina ya ndege hata kama iwe kubwa iweze kutua pale. Tumeshalipa, fidia imekamilika. Kwa hiyo, ndege zote muhimu zitatua katika eneo hilo na watalii kutoka Kenya watatua Musoma watakwenda Serengeti kwenye shughuli zao, na uchumi wa Mkoa wa Mara na maeneo mengine utafunga.

Vilevile swali lake la pili linalohusu Uwanja wa Ndege mdogo pale Magena. Wiki iliyopita Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi alikuwa pale, amefungua mnada wetu pale wa Magena, maana yake itaongeza soko la kibiashara katika eneo hilo, kuna mifugo itauzwa katika eneo hilo. Uwanja huu upo chini ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalipokea wazo hili, tufanye tathmini, tuangalie uwezo wa Serikali, ikiwezekana upanuliwe na kusimamiwa ili ndege ndogo za watalii ziweze kutua pale, na hivyo itapunguza msongamano pia kuja Musoma na badala yake watakuja kule Tarime ambapo kimsingi watalala Tarime, watakula Tarime, watafanya kazi Tarime na uchumi wa Tarime utafunguka. Ahsante sana. (Makofi)