Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Primary Question

MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaruhusu tena usafirishaji wa vipepeo nje ya nchi ili kuongeza vipato vya wananchi wa Muheza?

Supplementary Question 1

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, na nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwamba, kwa vile imeshathibitika kwamba jambo hili halina madhara yoyote kimazingira na kwenye idadi ya vipepeo, na kwamba kwanza ukiachilia mbali kuongeza vipato vya wananchi lilikuwa linasaidia kwenye idadi ya vipepeo kwa vile kwa kawaida kipepeo anayetaga mayai mpaka 500 kwa njia zake za kwaida huweza kuzalisha vipepeo wawili, lakini kwa njia hii ya msaada wa wananchi huweza kuzalisha mpaka vipepeo 300.

Je, Serikali haioni kwamba, ilishauriwa tu vibaya kwenye suala hili kwa kutotenganisha kati ya wanyama wakubwa kama chui, twiga na swala na hawa vipepeo wetu na kwamba inatakiwa kurudi nyuma na kutenganisha sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa vile ni nchi chache sana duniani ambazo zinaweza kuzalisha vipepeo kama sisi, na ni biashara na utalii mkubwa duniani; Serikali haioni haja sasa ya kuwekeza kwenye kuanzisha utalii wa vipepeo, ili kuongeza vivutio vya utalii nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mwin’juma, Maarufu kama “Mwana FA”, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Hamis Mwin’juma, lakini pia nimpongeze sana kwa kuendelea kusimamia eneo hili la wanyamapori hai, lakini nimpongeze pia kwa kuendelea kupigania wananchi wa Muheza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo ameshauri Mheshimiwa Mwinjuma, kwamba Serikali inawezekana ilishauriwa vibaya. Nimtoe wasiwsi kwamba Serikali iko makini na Serikali iko kazini na ina wataalamu wa kutosha. Suala hili limekuwa likichunguzwa na wataalamu mbalimbali. Muhimu ni kuangalia kipi faida na hasara ambayo inaweza ikapata Serikali. Tunapoendelea kuhamisha wanyama mbalimbali kutoka ndani ya nchi kupeleka nje ya nchi ina maana tunazidi kuuwa utalii wa hapa Tanzania. Hata hivyo nimtoe wasiwasi, kwamba suala hili tunaendelea kulifanyia tathmini, tutachakata kuangalia faida na hasara ya eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze pia, kwa kuendelea kuhamasisha utalii kupitia vipepeo ambavyo amevitamka yeye mwenyewe. Kwa hiyo, kama kweli tutaanzisha utalii wa vipepeo haina haja sasa hata kuendelea kuvitoa hivi vipepeo viende nje ya nchi kwa sababu tunapoendelea kuvitoa tunauwa soko la utalii wa ndani.

Name

Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaruhusu tena usafirishaji wa vipepeo nje ya nchi ili kuongeza vipato vya wananchi wa Muheza?

Supplementary Question 2

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia wazawa katika kukuza utalii wetu hasa cultural tourism? Kwa mfano kutumia wazee wa kimila kama wazee wa kihehe ambao walianza kutunza Mbuga ya Ruaha wakati wa Chief Mkwawa na kutumia wazee wengine kama Wamasai, ili kuhakikisha kwamba utalii wetu unakua, kwa kuwa wao wenyewe wanakuwa tayari ni kivutio?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli sasa hivi Serikali ina mpango wa kutumia watu maarufu, wazee wa kimila kama ambavyo amewaainisha Mheshimiwa Mbunge na watu maarufu wakiwemo wasanii ambao tutawatumia kama mabalozi wa hiyari. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, suala hili Serikali inalishughulikia; na tulishukuru sana Bunge hili limetupitishia bajeti nzuri ambayo sasa mwaka wa fedha 2021/22 tunaenda kutekeleza maeneo yote haya. Ahsante.