Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - (a) Je, ni lini wananchi wa Ludewa ambao maeneo yao yamechukuliwa na Serikali kwa muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Liganga na Mchuchuma watalipwa fidia? (b) Je, ni lini Mradi wa Liganga na Mchuchuma utaanza kufanya kazi ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Njombe na Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; wananchi wa Ludewa wangependa kufahamu kwa kuwa wamesubiria fidia hizi kwa muda mrefu. Je, kwa nini Serikali isitenganishe majadiliano na mwekezaji na suala la fidia ili wananchi wa Jimbo la Ludewa waweze kulipwa fidia mapema?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ningependa kufahamu ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya kuandaa wananchi wanaoathirika na miradi ili waweze kunufaika na miradi hii? Ahsante.

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika mradi huu fidia kwa wananchi iliyothaminiwa jumla ya bilioni 11.037 katika majadiliano au katika mkataba ambao tuliingia na kampuni hii Situan Honda ilikuwa yeye kama mwekezaji atakuwa na wajibu wa kulipa fidia eneo hilo ambalo atakuwa analitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema baada ya majadiliano na mwekezaji huyu tutaangalia sasa kama tutafikia muafaka maana yake yeye atakubaliana kulipa fidia, lakini utekelezaji wa mradi huu lazima uanze mwaka 2021/2022, aidha tumekubaliana na mwekezaji huyu au hatujakubaliana lakini mradi huu lazima uanze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshaeleleza na ni utekelezaji ambao unaenda kufanyika katika mwaka wa fedha ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu katika eneo hili, ni kweli Serikali imekuwa ikiweka fedha kwa ajili ya kuelimisha wananchi namna ambavyo watashiriki katika ujenzi wa mradi huu kwa maana ya local content kwamba wao watafanya nini au watashiriki vipi katika mradi huu mkubwa wa Mchuchuma na Liganga. Kwa hiyo fedha zinatengwa kila mwaka na elimu inaendelea kutolewa kwamba sasa mradi huu ukianza naamini elimu zaidi itatolewa ili wananchi wa eneo hili waweze kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu kikamilifu.

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - (a) Je, ni lini wananchi wa Ludewa ambao maeneo yao yamechukuliwa na Serikali kwa muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Liganga na Mchuchuma watalipwa fidia? (b) Je, ni lini Mradi wa Liganga na Mchuchuma utaanza kufanya kazi ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Njombe na Taifa?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kuendelea kuzungumzia mradi wa Mchuchuma na Linganga kwenye Bunge letu bila utekelezaji dhabiti ni aibu, ni wa muda mrefu tangu enzi ya akinamama Mary Nagu wakiwa Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unasuasua kwa sababu mwekezaji hana mtaji wa kutosha, ndiyo maana ameshindwa kulipa fidia. Kwa nini Serikali inamkumbatia huyu mwekezaji, kwa nini isiachane naye kama mama Samia anataka mradi huu uendelee, ikamtafuta mwekezaji mwingine na Serikali ikawekeza vya kutosha?

Name

Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Answer

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nijibu swali nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi umechukua muda mrefu lakini lazima tukubaliane kwamba mwekezaji huyu Situan alikuwa na mkataba na Serikali kupitia NDC. Kwa hiyo mkataba wake lazima uhitimishwe kisheria, tukienda papara tutapata matatizo. Hata hivyo, nimpe taarifa kwamba leo hii wanakaa na tunaamini ndani ya mwezi huu mazungumzo yatakamilika. Baada ya hapo tuatajua ama twende naye au tuachane kisheria twende kwa mwekezaji mwingine, lakini tumesema kabisa kwamba kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais mradi huu lazima uanze ndani ya mwaka ujao wa fedha.