Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Primary Question

MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Tarafa ya Simbo na Manonga katika Jimbo la Manonga?

Supplementary Question 1

MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweka kumbukumbu vizuri naomba kurekebisha kidogo vijiji vya Ulaya, Nkinga na Barazani, kwamba viko Tarafa ya Manonga na si Tarafa ya Simbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza, kwasababu ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais na sasa ndiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni lini Serikali itapeleka maji ya Ziwa Victoria katika Tarafa ya Simbo hasa Makao Makuu ya Tarafa ya Simbo na Tarafa ya Manonga, hasa Makao Makuu ya Tarafa pale Choma cha Nkola kwa kuwa maeneo hayo yana idadi kubwa ya wananchi wanahitaji huduma hii ya maji? Ahsante.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Gulamali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti Tarafa hizi mbili, ya Simbo na Manonga zote zipo katika mpango mkakati wa kukamilisha utekelezaji wa kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria. Mwaka ujao wa fedha wa 2021/2022 kadiri tutakavyopata fedha tutafikia maeneo hayo yote muhimu. (Makofi)

Name

Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Tarafa ya Simbo na Manonga katika Jimbo la Manonga?

Supplementary Question 2

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza napenda kuipa shukrani Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi inavyofanya kazi zake katika Wizara hii ya Maji, inatekeleza kwa hali na mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sasa hivi ni mkazi wa Dodoma nakaa maeneo ya Mkalama. Eneo lile la Mkalama maji yapo mengi sana lakini mabomba yanakuwa yanapasuka sana maji yanatoka na hovyo. Mimi mwenyewe binafsi nakuwa nahisi huruma. Kwa hiyo nimwambie Mheshimiwa Waziri, kama Serikali imeliona suala hili kule sehemu ya Mkalama basi ifanye kazi zake kwenda kuyaziba yale mabomba ili maji yasitoke hovyo. Ahsante sana.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kupokea pongezi kwa namna ambavyo ameridhishwa na utekelezaji wetu. Sasa kuhusiana na tatizo la maji kumwagika baada ya mabomba kupasuka maeneo ya Mkalama nipende kusema kwamba Meneja wa Maji Mkoa wa Dodoma Engineer Aron anafanya kazi usiku na mchana. Lengo ni kuona anakwenda kufanyia kazi mapungufu yote haya yanayoendelea kujitokeza. Siyo tu eneo la Mkalama hata wale wenzetu wanaotoka Ilazo taarifa za matatizo ya maji pale tunazo na tunazifanyia kazi. Tayari tumempa mtu kazi ya kuweza ku-supply mabomba.

Kwa hiyo mabomba haya yakifika, tunatarajia wiki hii yatafika, tunakuja kufanya ukarabati na marekebisho maeneo yote ambayo yana matatizo ya kupasuka na kumwaga maji mitaani.