Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati barabara zilizoharibika hasa barabara za vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali; kwa kuwa tulishawahi kupata mafanikio katika kuunganisha baadhi ya shughuli za taasisi fulani kwa mfano tuliunganisha TRL pamoja na RAHCO, lakini pia kwa ufanisi kabisa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeweza kuunganishwa.

Je, Serikali haioni sasa kwamba imefika mahali kwamba tulete mabadiliko ya sheria ambayo tutaunganisha sasa TARURA pamoja na TANROADS ili waweze kufanya kazi pamoja tuweze kuondoa hii kero ambayo hii kila siku kunakuwa na mapungufu ya fedha?

Mheshimiwa Spika, Tabora Mjini ina kata 29 na vijiji visivyopungua 41, imeathirika sana pembezoni Kata za Tambuka Reli, Ntarikwa, Uyui, Ifucha na kata nyingi za pembezoni.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni muda muafaka pamoja na kwamba imetenga bajeti ya nyongeza kuweza kufanya haraka kutengeneza zile barabara kwa sababu nyingine hazipitiki? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme dhumuni la Serikali kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini ilikuwa ni kuiwezesha Mamlaka hii kuwa karibu zaidi na wananchi na barabara za vijijini na mijini ili tathmini ya kina na ya haraka iweze kufanyika na kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa mapema iwezekanavyo kuliko ilivyokuwa inasimamiwa na TANROADS kutokana na ukubwa wa nchi na majukumu ambayo TANROADS ilikuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TARURA inafanya kazi yake vizuri na kwa kushikirina kwa karibu sana na TANROADS tunaendelea kuhakikisha barabara zetu za mijini na vijijini zinapitika vizuri na changamoto ya fedha haitakuwa na suluhu kama tutaunganisha TANROADS na TARURA kwa sababu Serikali ni moja na vyanzo ni vilevile. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba TARURA inafanya kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na suala la barabara za Tabora Mjini; ni kweli nchini kote tumepata changamoto ya uharibifu wa barabara nyingi na nimhakikishie kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tayari fedha zimetengwa zaidi ya mara moja na nusu ya fedha za mwaka wa fedha uliopita ili kuhakikisha kwamba fedha zile zinatumika kurekebisha miuondombinu mingi ya barabara na katika Jimbo la Tabora Mjini barabara Mama Onyango, Kilimbika, Jobodo, Mkoani, Lubatuka, Manolelo, Inala, Shule ya Msingi Jamhuri na nyingine tayari kazi za mrekebisho zinaendelea na nimhakikishie zitaendelea kufanyiwa marekebisho, ahsante sana. (Makofi)

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati barabara zilizoharibika hasa barabara za vijijini?

Supplementary Question 2

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nilikuwa nasema kwa kuwa barabara nyingi za vijijini ambazo zinahudumiwa na TARURA zimeonekana kutokuwa na uteshelevu wa bajeti na angalau TANROADS kuonekana wana bajeti ya kutosha.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha barabara nyingi ambazo zipo vijijini zinazochelewa kupandishwa hadhi kwenda TANROADS ili angalau ziweze kusaidiwa kwa sababu barabara za vijijini tunapata shida sana na bajeti ya TARURA ni ndogo?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, bajeti ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Wakala wa Vijijini na Mijini imeendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi katika mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021 bajeti ilikuwa bilioni 275.034 lakini mwaka ujao wa fedha ni shilingi bilioni 400, ongezeko la zaidi ya shilingi bilioni 125. Jitihada hizi zote ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha uwezo wa TARURA kuhudumia barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Spika, na naomba nichukue hoja yako, tutaendelea kufanya tathmini kwenye barabara hizo ambazo zinahitaji kusajiliwa wa TARURA lakini zile ambazo zinahitaji kupandishwa hadhi kwenda TANROADS kuna utaratibu ambao Serikali imeelekeza naomba tuufuate huo ili tuweze kupata barabara zenye hadhi hiyo na kufanyiwa matengenezo kwa wakati, ahsante.