Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Primary Question

MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itafikisha umeme katika vijiji 28 ambavyo bado havijapata umeme kati ya vijiji 50 vya Jimbo la Singida Mashariki?

Supplementary Question 1

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kunipa majibu ambayo pia nahitaji nipate uhakika.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umeme ni chachu ya maendeleo na kwa kuwa ni asilimia 44 tu ya vijiji vya Singida Mashariki vina umeme, ninalotaka kujua na wananchi wa Singida Mashariki, hususan Tarafa ya Mungaa ambayo ina kata saba na ambayo haina umeme kabisa.

Ni lini mkandarasi atakwenda kuanza kazi kama alivyosema mwezi Machi mpaka sasa hajapatikana na tunataka tujue jina la mkandarasi huyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa, vijiji ambavyo amevitaja anasema vina umeme na kwa sababu kuna mradi wa ujazilishaji na mpaka tunavyoongea sasa ni unaenda taratibu mno. Hawaoni sababu ya kuongeza kasi ya kuweza kuweka umeme katika vitongoji vilivyobaki? (Makofi)

SPIKA: Yaani Mheshimiwa Mtaturu kuna tarafa ambayo haina umeme, tarafa nzima?

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, Tarafa nzima ya Mungai yenye Kata za Mungaa, Lighwa, Makiungu, Kata ya Ituntu, Mungaa na Kikiyo pamoja na Kata ya Msughaa zote hazina umeme ambazo ni mpakani mwa Chemba.

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtaturu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunakiri ni kweli kwamba mpaka sasa kuna baadhi ya vijiji Tanzania havijafikiwa na umeme. Kama tulivyosema tulianza tukiwa na vijiji 12,268 lakini tumepunguza mpaka sasa tuna vijiji 1,974 ndio havina umeme na mpango uliopo kwa sasa ni kuhakikisha kabla ya mwezi Disemba, 2022 vijiji vyote hivyo 1,974 vyote vinakuwa vimepata umeme na tuko tayari tumeshawapata wakandarasi wa kupeleka umeme kwa kila eneo katika REA III, Round II.

Mheshimiwa Spika, Jumanne ya wiki hii tulikuwa tuna kikao na wakandarasi hao ambao tuymewapa kazi hizo na tumewaagiza kabla ya Jumatatu inayokuja wawe wote wamewapigia simu Waheshimiwa Wabunge pamoja na viongozi wengine kwenye maeneo kuwaambia kwamba tumekuja na tumeripoti kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri juzi kuna maeneo wakandarasi wetu wameenda, lakini hawakuwa wametoa taarifa ya kutosha kwa Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, ili kuweza kujua kwamba wapo. Sasa mimi nimechukua jitihada ya kuwapatia wakandarasi namba za Waheshimiwa Wabunge na kuwaelekeza kabla ya Jumatatu nitakuwa nime-verify kwa Mbunge mmoja-mmoja kujua kama amepigiwa simu au kutumiwa message kuambiwa kwamba mimi ninaenda kuripoti katika eneo hilo. Kwa hiyo, niseme katika maeneo hayo ambayo Mheshimiwa Mtaturu ameyataja kazi inaendelea na tutafikisha umeme katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, lakini katika swali la pili, kwenye densification (ujazilizi); mkandarasi anayeendelea kufanya kazi katika Mkoa wetu wa Singida anaitwa Sengerema, ni mkandarasi mzuri, anafanya kazi yake vizuri na anakwenda hatua kwa hatua na tunatarajia kufikia mwezi Disemba mwaka huu atakuwa amemaliza vitongoji vyote. Kwenye kupeleka umeme kwenye vitongoji tunapaleka kupitia miradi yetu ya REA ambao wanapeleka kwenye vijiji wanashuka kwenye vitongoji, lakini tuna mradi maalum huu wa densification ambao wenyewe unalenga vitongoji, lakini pia na wenzetu wa TANESCO bado wanalenga vitongoji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kufikia mwaka 2022 tunatarajia kuwa tume-cover vijiji vyote, lakini tunakuwa tume-cover vitongoji vingi sana. Mpango wetu kuendelea kupeleka umeme katika vitongoji kwa sababu kupeleka umeme ni zoezi endelevu.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nipongeze majibu ya nyongeza ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika Jimbo la Mheshimiwa Mtaturu.

Mheshimiwa Spika, ni kweli jimbo la Mheshimiwa Mtaturu kimsingi ile tarafa ambayo haijapata umeme pamoja na tarafa nyingine zote wakandarasi wameondoka jana kwenda Singida kwenda kufanya kazi, pamoja na tarafa hiyo. Mheshimiwa Mtaturu alikuwa na vijiji 12 ambavyo havijaguswa kabisa pamoja na hiyo tarafa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mtaturu pamoja na Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa wananchi wa Singida katika jimbo lake wote watapata umeme ndani ya miezi 18 kuanzia jana walipoondoka wakandarasi. (Makofi)