Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Primary Question

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Maji kutoka Mto Rumakali katika Kata ya Lufilyo utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza naomba kwanza nikushukuru sana pamoja na Serikali kwa changamoto ambazo tulizipata Jimbo la Busokelo kwa mafuriko ambayo yalisababisha nyumba zaidi ya 30 pamoja na mtu mmoja kufariki, lakini wewe pamoja na timu yako mlikuja kutoa msaada. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu ya Serikali, huu Mradi wa Mto Rumakali upo katika halmashauri mbili kati ya Halmashauri ya Busokelo pamoja na Mkoa wa Njombe, lakini mradi huu katika utekelezaji wake inaonyesha kwamba licha ya kwamba megawati hizo zitazalishwa tunahitaji kujua wananchi wa Busokelo, je, ni kwa kiwango gani kupitia Corporate Social Responsibility ya mradi huu watanufaika wananchi wa Busokelo pamoja na Kata hii ya Lufilyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mradi huu utaanza kuzalishwa hivi karibuni na tunafahamu kwamba Halmashauri ya Busokelo ni halmashauri changa, je, ni kwa kiwango gani Serikali imejipanga kuboresha miundombinu kufikia sehemu ya uzalishaji wa mradi huu kupitia Halmashauri ya Busokelo hususani madaraja ya Mto Lufilyo pamoja na madaraja ya Mto Malisi? Ahsante.(Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Atupele, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotekeleza miradi mikubwa ya namna hii kipande cha Corporate Social Responsibility kwa maana ya manufaa ya mradi kwa umma ni kipande ambacho kinaongozwa na sheria tuliyokuwa nayo kwetu Tanzania na tunakiweka kwenye mkataba kwa ajili ya kukubaliana kwamba katika mapato na kazi utakayoifanya kiasi hiki basi kirudi kurudisha huduma katika jamii husika. Tunakwenda afya, tunakwenda kwenye maji, tunakwenda kwenye elimu na kwenye miundombinu kama hiyo ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni katika mradi wetu wa Mwalimu Nyerere, katika mradi wetu ule tunazo trilioni sita, lakini asilimia nne zimeenda kwenye CSR kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumeingia mkataba na mkandarasi wa kujenga mradi ule, lazima tuwe na kifungu cha Corporate Social Responsibility ambacho kitawanufaisha wananchi wa Busokelo, lakini pia na Makete ambapo ndiyo bwawa linapoanzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, umuhimu wa kufikia ile miundombinu itakayotengenezwa ndiyo itakayofanya miundombinu ya barabara iwepo, kwa sababu mradi kama mradi kwa maana ya ujenzi wa bwawa, lakini pia ujenzi wa ile power house, sehemu ambayo umeme utazalishwa, lazima tuwe tuna barabara nzuri zinazopitika kwa sababu tunayo mizigo mikubwa ambayo tunatakiwa kuisafirisha kuifikisha katika maeneo yale. Kwa hiyo tutajenga barabara hizo ikiwa ni faida kwa kuhudumia mradi, lakini pia na kuhudumia wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kufikika katika maeneo yote.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Maji kutoka Mto Rumakali katika Kata ya Lufilyo utaanza?

Supplementary Question 2

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, kwanza niipongeze Wizara ya Nishati kwa sababu mradi huu wa Bwawa la Rumakali, bwawa linajengwa Wilaya ya Makete, lakini power plant inajengwa Busokelo kwa ndugu yangu Mwakibete.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu dogo la nyongeza lilikuwa Waziri alipokuja Makete mwezi wa kwanza aliahidi kwamba mradi huu utaanza mwezi Machi kwa maana ya demarcation kuweka alama, lakini hadi sasa haujaanza. Je, ni lini Serikali itaanza kuweka alama (demarcation) kwenye mradi huu ili wananchi waendelee na shughuli za kijamii, waachane na hii changamoto waliyonayo sasa wanashindwa kuendelea na shughuli za kijamii kwa sababu, hawajui bwawa mipaka itaishia wapi? Naomba pia kujua kuhusu mambo ya fidia. Ahsante.

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mwezi Januari Mheshimiwa Waziri alitembelea mradi ule kuona maandalizi yake yamefikia wapi na sisi kama Serikali tumejipanga kuanzia tarehe Mosi, mwezi Juni, wataalam wa Wizara na TANESCO wataenda katika eneo la mradi kwa ajili ya kuhakiki mipaka na kuweka demarcation na kufanya maandalizi ya kulipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, fidia italipwa katika maeneo makubwa matatu. Fidia kwenye eneo ambapo litajengwa bwawa, lakini fidia katika eneo ambalo litaenda kuweka hiyo power house, sehemu ya kuzalisha umeme kwa sababu kutoka kwenye bwawa kushuka mpaka sehemu ya kuzalisha umeme kuna kilometa kama saba. Vile vile fidia italipwa kutoka kwenye njia ya kuzalisha umeme mpaka kwenye kituo chetu cha Iganjo ambapo kuna kilometa kama mia moja hamsini kutoka kwenye lile eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maeneo yote hayo kuanzia tarehe Mosi mwezi Juni yataanza kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini kwa ajili ya kuweza kulipa fidia na mradi uweze kuendelea kama ilivyosemwa kufikia mwezi Oktoba.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, aya ya tatu ya jibu lako, kuna sehemu inasomeka hadi kituo cha kupooza umeme cha Iganjo Mkoani Mbeya. Sasa hiki kituo cha kupooza umeme hii Kata hii inayoitwa Iganjo mlipoweka kituo hiki cha kupooza umeme, Mtaa wa Igodima hauna umeme, sasa mmeweka kituo cha kupooza umeme, lakini mtaa hauna umeme. Huo mtaa utapata lini umeme? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na kama tulivyokuwa tukieleza hapo awali ni nia ya Serikali kuhakikisha kila mwananchi wa nchi hii anapata umeme katika eneo lake. Katika eneo hili sasa ni eneo la kipaumbele kwa sababu siyo vema kumpelekea mtu shughuli ambayo wananufaika nayo wengine. Kwa hiyo, nitoe ahadi ya Serikali kwamba, tutahakikisha hicho kituo kinapowekwa pale basi tunaweza kupata umeme wa kuhudumia yale maeneo yote ya jirani kama ambavyo tumefanya hivi karibuni katika Bwawa la Mtera kwa kuongeza pale transformer ya kuhudumiwa wale wananchi wanaoishi katika maeneo yale kwa haraka kabisa.