Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Primary Question

MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:- Je, Serikai haioni umuhimu wa kuajiri Wafamasia angalau katika kila Kituo cha Afya nchini ili kuimarisha usimamizi na mtiririko wa upatikanaji dawa?

Supplementary Question 1

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina swali la nyongeza. Wakati mwingine wananchi wetu wanakwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wanakosa dawa siyo kwa sababu dawa hiyo inakuwa haipo kwenye maghala ya MSD, bali ni matatizo ya uagizaji ambayo yanatokana na vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kutokuwa na hawa watu muhimu wafamasia na wateknolojia dawa ambao wana utaalam wa kuratibu, ku-forecast na kujua kwamba kipindi hiki tuagize dawa gani, kipindi hiki kuna mlipuko wa magonjwa fulani, kuwe na dawa fulani. Sasa ili kuhakikisha kwamba watu hawa muhimu wanakuwepo muda wote katika vituo vya kutolea huduma za afya:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuruhusu Ma-DMO na Wakurugenzi wa Halmashauri zenye uwezo ku-engage watu hawa ili wawepo muda wote hata kwa mtindo wa internship au mikataba ya muda wakati tukisubiri hizi ajira?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kimsingi tunafahamu kwamba katika vituo vyetu vya huduma za afya kama ambavyo nimetangulia kueleza kwenye jibu la msingi, tuna upungufu wa wataalam hawa wa teknolojia wa dawa na wateknolojia wasaidizi wa dawa. Ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge Zedi ameelezea, tunahitaji kuwa na wataalam hawa ili kuhakikisha vituo vyetu vinaweza kuweka maoteo mazuri ya dawa lakini pia uagizaji kulingana na utaalam ili kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na jitihada hizi za Serikali, pia Serikali ilishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi, kwa Halmashauri zile ambazo zina uwezo wa mapato ya ndani ya kuwaajiri kwa mikataba wataalam hawa, waweze kuwaajiri na kuwasimamia kwa karibu chini ya DMO kuhakikisha huduma hizi za upatikanaji wa dawa katika vituo hivyo zinaboreshwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba jambo hilo lishafanyiwa kazi na Serikali na nitoe wito kwa Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kutumia fursa hiyo kwa wale ambao wana uwezo wa kuwaajiri ili tuboreshe huduma za afya kwa wananchi.