Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Primary Question

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuipa fedha Halmashauri ya Temeke ili iweze kujenga Shule mpya za kutosha kutokana na Jimbo la Mbagala kuongoza kuwa na wanafunzi wengi wa Shule za Msingi na Sekondari?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanatia moyo, sasa nataka kujua; kwa kuwa Sera ya Serikali ni kuwa na Sekondari katika kila Kata: Je, ni lini sasa Serikali itajenga Shule za Sekondari katika Kata ya Mbagala, Kilungule na Kibonde Maji ambapo Kata hizo hazina Sekondari kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami kwenda katika Jimbo la Mbagala kujionea hali ya msongamano wa wanafunzi darasani katika Shule ya Mbande, Chamazi, Mianzini, Kilamba, Nzasa, Mbagala, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kilungule na Kijichi? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha baadhi ya Kata hususan Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kibonde Maji ambazo mpaka sasa hivi hazina Sekondari; na Sera ya Serikali ni kwamba kila Kata lazima iwe na Sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Mbagala ambako anawapigania kwamba hizo Kata zote zitapata Sekondari za Kata ambazo zipo katika mpango wetu. Kwa sababu sasa hivi Serikali tuna mpango wa kujenga sekondari 1,000 nchi nzima katika zile Kata zote ambazo hazina sekondari. Kwa hiyo, miongoni mwa Kata tutapeleka Shule za Sekondari ni pamoja na Kata alizoziainisha; Kata ya Mbagala, Kilungule pamoja na Kiponde Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tuongozane tukaone msongamano katika shule ambazo ameziainisha hapa ikiwemo Mbande, Chamazi, Rangi Tatu, Mbagala Kuu, Mzinga, Kijichi na Kilungule; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari, hata akisema baada ya maswali na majibu twende, mimi nitakwenda kwa ajili ya hiyo kazi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuipa fedha Halmashauri ya Temeke ili iweze kujenga Shule mpya za kutosha kutokana na Jimbo la Mbagala kuongoza kuwa na wanafunzi wengi wa Shule za Msingi na Sekondari?

Supplementary Question 2

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami siko mbali sana. Madhara yaliyopo katika Jimbo la Mbagala ni sawa sawa na Jimbo langu la Temeke.

Nimeona hapa Shule nyingi za Sekondari zimeenda kujengwa Mbagala, lakini Temeke bado tuna kiu; kama nilivyosema siku zote, Temeke tunazaliana sana na sasa tuna watoto wengi wa Darasa la Kwanza. Tutakapofika mbali, naamini kabisa sekondari hizi zilizopo haziwezi kutosha hasa kule Vituka, Tandika, Kurasini, Mtoni, Temeke 14, kote tunatamani sekondari hizi ziwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kwamba kama atakwenda naye Mbagala, basi twende pamoja na Temeke tufike. Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge naye kwamba tutakavyopanga safari ya Pamoja, Mbunge wa Mbagala pamoja na Mbunge wa Temeke tutakwenda. Niliainisha Kata za Mbunge wa Mbagala na wewe tutakwenda wote katika maeneo ya Vituka, Tandika, Kurasini, Temeke 14, kuhakikisha tunafanya kazi ya wananchi. Nanyi wote mnafahamu, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuondoa tatizo la Madarasa nchi nzima, ahsante sana. (Makofi)