Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO - K.n.y. MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:- Usambazaji wa umeme vijijini unapaswa kukamilika ifikapo Mwaka 2021/2022:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa usambazaji wa umeme vijijini unakamilika kama ilivyopangwa?

Supplementary Question 1

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ni ahadi ya Chama Tawala na vilevile ahadi ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba mapema mwaka huu wa fedha vijiji hivyo vitakuwa vimekamilishiwa kupata umeme.

Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha kupeleka umeme kwenye vijiji vilivyobaki vya Mkoa wa Tanga hasa Vijiji vya Lushoto na Kilindi ambako kuna hali ngumu zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tatizo kubwa la kukatika kwa umeme kwenye Vijiji vya Handeni, Kilindi na Lushoto linalosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha. Je, ni lini Serikali sasa itamaliza tatizo hilo kwa kubadilisha miundombinu ya umeme hasa katika maeneo ya njia ya umeme kutoka Mombo kwenda Lushoto? (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba vijiji vyote 1,974 ambavyo mpaka sasa havijapata miundombinu ya umeme, vitapata kufikia Desemba, 2022. Hii awamu ya tatu mzunguko wa pili wa REA utahakikisha kwamba unamaliza maeneo yote ambayo yalikuwa hayajapata umeme na hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,268 ambavyo vilikuwa bado havijapata umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yeye na Waheshimiwa wengine wote kwamba ifikapo Desemba mwakani tutakuwa tumefikisha umeme katika vijiji vyote ambavyo havikuwa na umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, kwanza napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Tanga kwa ufuatiliaji mzuri kabisa wa miundombinu ya umeme katika mkoa wao. Mojawapo ya maeneo ambayo yalikuwa yana matatizo makubwa ya umeme ni Tanga. Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO tumehakikisha tunamaliza tatizo la umeme katika Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu niseme tu kidogo kwamba Tanga ina matumizi ya umeme takribani Megawatts 110 na wanapata umeme katika vyanzo viwili pale Hale Megawatts nne na New Pangani Megawatts 68 na umeme mwingine pia unatoka kwenye kituo chetu cha Chalinze kwenda Tanga. Sasa hizo njia zinakuwa ni ndefu kidogo na hivyo umeme mwingine unapotea njiani.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kutoka Chalinze kwenda Tanga, ile njia iliyojengwa pale inashindwa kubeba umeme mkubwa, kwa hiyo, tumeamua kuweka mkakati wa muda mrefu wa kujenga njia ambayo itakuwa ni ya Kilovolt 220 itakayoweza kubeba umeme mkubwa kwa ajili ya kufikisha Tanga bila kukatika. Kwa hiyo, tunajiandaa, tumeshafanya feasibility study, tumeshapata maeneo ya kujenga sub-station ikiwepo eneo la Segera, tutamaliza tatizo hilo. Kwa sasa, Timu yetu ya TANESCO kupitia Shirika lake la ETDCO iko kazini inaendelea kurekebisha miundombinu ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipata takribani shilingi bilioni 4,500 kurekebisha miundombinu ya umeme ya Tanga ikiwemo kurekebisha nguzo, waya na vikombe kwa kilometa zaidi 2,000 na maelekezo ya Wizara ni kwamba ifikapo Mei, 2021 iwe imekamilika. Hivyo timu yao TANESCO kupitia ETDCO ni kubwa na inaendelea kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo, tunawahakikishia wananchi wa Tanga kupitia Wabunge wao kwamba kilio chao tunakifanyika kazi. Vile vile maeneo mengine tutaendelea kuhakikisha tunarekebisha miundombinu ili kuondoa matatizo yaliyopo. (Makofi)

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO - K.n.y. MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:- Usambazaji wa umeme vijijini unapaswa kukamilika ifikapo Mwaka 2021/2022:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa usambazaji wa umeme vijijini unakamilika kama ilivyopangwa?

Supplementary Question 2

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ina vijiji 76, vijiji 34 bado havijapatiwa umeme. Naona uzalishaji wa vijiji vifuatavyo mahitaji ya umeme ni makubwa sana; Kijiji cha Mlembwe, Lilombe, Kikulyungu, Mkutano, Mpigamiti, Ngorongopa, Ngongowele, Kimambi, Nahoro na Ndapata, vijiji hivi kwa sababu ya uzalishaji wake mahitaji ya umeme ni makubwa sana. Je, Serikali ni lini mtatupelekea umeme kwenye vijiji hivi ili kuwatia wananchi hamasa zaidi waweze kuzalisha zaidi mazao ya chakula na biashara?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Kuchauka kwa sababu yeye ni mmojawapo wa Wabunge wanaofuatilia pia maendeleo ya majimbo yao katika maeneo mbalimbali katika likiwepo eneo la umeme. Kama nilivyosema hapo mwanzo ni kwamba vijiji vyote ambavyo havijapata umeme, kufikia Desemba, 2022 vitakuwa vimepatiwa umeme vikiwepo vijiji vyote alivyovitaja vya Jimbo la Liwale. Tunaomba aendelee kutusaidia na kusimamia utekelezaji ambao utafanyika katika maeneo yake.

Name

Dr. Alfred James Kimea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO - K.n.y. MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:- Usambazaji wa umeme vijijini unapaswa kukamilika ifikapo Mwaka 2021/2022:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa usambazaji wa umeme vijijini unakamilika kama ilivyopangwa?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona nami niulize swali dogo la nyongeza. Napenda kuipongeza Serikali kwani ndani ya Kata zangu zote 11 kwenye Jimbo la Korogwe Mjini umeme umefika, lakini changamoto ni kwamba ndani ya Kata hizo ipo Mitaa mingi ambayo umeme haujafika kabisa. Je, Serikali inawaahidi nini wananchi wa Korogwe katika kutatua changamoto hiyo?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kimea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, TANESCO inapeleka umeme katika maeneo mbalimbali kwa program za kila siku za kawaida, kwenye Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Pia zipo program nyingine ambazo zinapeleka umeme kwenye Mitaa na Vijiji vyetu ikiwemo REA yenyewe, densification na peri-urban.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mheshimiwa Dkt. Alfred ambapo tayari Kata zake zote na vijiji vyake vyote vina umeme, yale maeneo machache ambayo hayana umeme, mradi wetu wa densification utapelekea umeme katika maeneo hayo kuanzia mwezi Saba. Pia tunavyo Vitongoji na Mitaa takribani kama 3,000 ambavyo vitapelekewa umeme, kwa hiyo, Vitongoji vyake na Mitaa yake Mheshimiwa Mbunge pia ni sehemu ya maeneo hayo yatakayopelekewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambao densification tu itaanza mwezi wa Saba, Mheshimiwa ataweza kupata umeme katika eneo lake kwa sababu amekuwa akifuatilia sana ofisini kwetu na ni mfuataliaji mzuri wa maendeleo ya wananchi. Kwa hiyo, nawapongeza wananchi kwa kupata Mbunge mfuatiliaji kama wa aina yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO - K.n.y. MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:- Usambazaji wa umeme vijijini unapaswa kukamilika ifikapo Mwaka 2021/2022:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa usambazaji wa umeme vijijini unakamilika kama ilivyopangwa?

Supplementary Question 4

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Kitongoji cha Banawanu katika Kata ya Mseke kiko karibu sana na Mji wa Iringa Mjini na kipo katikati ya Tosamaganga pamoja na Uwachani; na hii ilikuwa ni ahadi ya Mbunge ambaye ndiye mimi kwamba tutawapelekea umeme. Je, ni lini sasa TANESCO itapeleka umeme ili hata kunifichia aibu Mbunge mwenzake?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Kiswaga kwa kutoa ahadi za ukweli kwa wananchi wake kuwaahidi kuwapelekea umeme. Nawaahidi Waheshimiwa Wabunge wote walioahidi kupeleka umeme kwa wananchi wao kwamba ahadi hizo zilikuwa ni za ukweli na Serikali sikivu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kitongoji alichokisema kama nilivyosema, mradi wetu wa densification ambao sasa tupo IIB utapeleka katika Vitongoji ambavyo vilikuwa havijapata umeme, lakini maeneo mengine ambayo hayajapata umeme kwa sasa kwa maana ya vijiji, vitongoji vilivyomo, tulivyovitaja 1,474 vitapata umeme pia katika awamu hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa wananchi kwamba umeme utapelekwa na ahadi ya Mheshimiwa Jackson Kiswaga itakuwa ni ya ukweli kuanzia mwezi Julai.