Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Primary Question

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:- Sehemu kubwa iliyokuwa ikitumika kwa shughuli za uchumi katika Wilaya ya Malinyi imetwaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mwaka 2017 ambapo waliweka mipaka maarufu kama “TUTA LA 2017” bila kushirikisha wananchi. Je, Serikali haioni haja ya kurejea na kufanya upya mapitio shirikishi ya mipaka ya eneo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Februari nilitoa ombi kutokana na majibu hayo kwamba Kijiji cha Ngombo ambacho kinatajwa kihame tuliomba tuko radhi kipunguziwe ukubwa wa mipaka na kupunguza mifugo Zaidi ya 90% ili wananchi waweze kubaki sehemu iliyobaki ichukuliwe kwa ajili ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia eneo kubwa la Jimbo huo mpaka wa 2017 tuliomba tupewe walau mita 700 kama siyo kilomita 1 kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kwa maana umbali sehemu ambayo tunafanya shughuli mpaka mto ni mrefu sana tofauti na ambavyo inasemwa kiujumla. Kwa hiyo, je Serikali iko radhi kuridhia maombi haya?

Mheshimiwa Spika, la pili, majibu ya Naibu Waziri kuhusu wanashughulikia hii Tume ya Mawaziri nane ni tangu mwaka jana wanasema tunashughulikia tutajibu tutajibu watu tuko pending hatufanyi shughuli za kilimo, hatujui hatma yetu. Lini hasa Serikali itatoa msimamo wa mwisho juu ya jambo hili ili tuendelee kuwaza mambo mengine tulimalize?

Mheshimiwa Spika, la tatu, kwa wale ambao tayari wameshalima Wizara inaridhia kipindi hiki tuweze kuvuna? Ahsante

Name

Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ningependa kutoa ufafanuzi kwa Mheshimiwa Antipas kwamba mipaka ya Bonde Tengefu la Kilombero iliwekwa mwaka 1952 kwa GN Namba 107 na ikarejewa mwaka 1997. Mipaka hiyo haijawahi kurekebishwa mpaka sasa kilichofanyika ni wananchi wa maeneo mbalimbali kuvamia maeneo hayo na kutokana na uvamizi huo Serikali ikachukua hatua ya kuunda kamati maalum ya Mawaziri ikiongozwa na Waziri Mwandamizi Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi ambapo taarifa yake imefikia hatua ya mwisho tunaenda kutoa tathimini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo maombi hayo yote tayari Mawaziri walishakwenda kule wamefanya tathmini ripoti iko tayari na watajulishwa wananchi. Kuhusiana na kulima hatuwezi kuendelea mtu kulima ndani ya hifadhi. Kwasababu mpaka unajulikana unaposema unaomba tulime maana yake unataka tulime ndani ya hifadhi madhara ya kulima ndani ya hifadhi hii ni kuhujumu mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, tusubiri maelekezo ya kamati maalum ya Baraza la Mawaziri tutajua hatma ya suala hili.