Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:- Mwaka 2015 wakati wa Kampeni, Mhe. Rais aliahidi kujenga barabara ya kilometa tatu katika Mji wa Kakonko ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya. Je, kwa nini ahadi hiyo haijatekelezwa na ni lini sasa itatekelezwa?

Supplementary Question 1

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ujenzi huu ni ahadi ya muda mrefu, ni miaka sita sasa lakini kama ambavyo ameweza kutoa majibu utekelezaji wake umeanza kwa kuweka kifusi katika Mji ule wa Kakonko. Ni miezi minne sasa shughuli za biashara katika Mji ule hazifanyiki, je, Serikali iko tayari angalau kifusi kiweze kusawazishwa katika maeneo yale ili wananchi waendelee na shughuli zao wakati taratibu hizo nyingine zikifanyika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya Kakonko – Kinonko – Nyakayenze - Muhange na Kasanda - Gwanumpu - Mgunzu ni barabara ambayo iko chini ya TARURA. Barabara hii imeharibika sana pamoja na kwamba ni maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa, wananchi hawawezi kusafirisha mazao yao. Je, nini jibu la Serikali kuhusiana na suala hili? Ahsante. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anaiuliza Serikali kwamba ni kwa nini sasa tusisambaze kile kifusi ili shughuli zingine ziendelee. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi ni kwamba barabara ile inajengwa kwa kiwango cha lami, kwa hiyo, kile kifusi ni sehemu tu ya process za kukamilisha barabara ile. Kama tulivyojibu kwenye jibu la msingi kwamba kufikia mwezi Mei, yaani mwezi ujao ile barabara itakuwa imekamilika kwa kiwango cha lami kwa sababu TARURA wako kazini. Hapa napozungumza wanasikia, nina hakika hilo zoezi litakuwa linaendelea na kazi inafanyika.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ameainisha barabara ambazo zimeharibika sana na kuiomba Serikali iweze kuzifanyia kazi. Nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmini na baada ya hapo nafikiri sisi na TARURA katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko tutakaa pamoja kuhakikisha barabara hiyo inajengwa ili kuondoa hiyo adha ambayo wananchi wanaipata. Ahsante.

Name

Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:- Mwaka 2015 wakati wa Kampeni, Mhe. Rais aliahidi kujenga barabara ya kilometa tatu katika Mji wa Kakonko ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya. Je, kwa nini ahadi hiyo haijatekelezwa na ni lini sasa itatekelezwa?

Supplementary Question 2

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara kule Kakonko inafanana kabisa na ahadi ya Mheshimiwa Rais katika barabara ya Boay – Gidas hadi Getasam, Wilaya ya Hanang, lakini barabara ya Boay –Gidas, barabara ya Babati Vijijini: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huu wa barabara kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, sasa hivi barabara hiyo imekuwa ni chakavu kabisa na haiwezi kupitika: Je, Serikali inatuahidi nini hata kutusaidia kwa kiwango cha changarawe? Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ambacho amejaribu kukiainisha Mheshimiwa Mbunge; ni lini Serikali itaanza kukamilisha ahadi za Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Marais wote waliotangulia na hapa amejaribu kuainisha barabara katika maeneo ya Hanang na Babati Vijijini.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie kwamba mpaka sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Serikali kwa ujumla tumeanza mchakato wa kuziainisha ahadi zote zilizotolewa na viongozi wakubwa nchini. Baada ya hapo tutazifanyia tathmini, tutazitenga katika mipango yetu na kuziwekea bajeti ili kuhakikisha kila ahadi ambayo kiongozi mkubwa aliahidi inatekelezwa na kwa wakati ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi, hususan maeneo yale ambayo yana-involve sana uzalishaji mkubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.