Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, ni lini Kituo cha Afya Kinesi kitapandishwa hadhi na kuwa Hospitali kamili kutokana na kituo hicho kuhudumia wananchi zaidi ya vijiji 27 katika Jimbo la Rorya?

Supplementary Question 1

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nashukuru.

Niseme tu kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri nirudie kumuomba kama kuna uwezekano angalau wa kufika Rorya kuitambua na kuielewa jiografia ya Rorya ilivyokaa. Nimekuwa nikimuomba hii ni mara ya pili tena narudia kumuomba. Imani yangu akifika atagundua hiki Kituo cha Afya ambacho tumekuwa tukikizungumzia kinahudumia kata zaidi ya tano ikiwemo Kata ya Kyang’ombe, Baraki, Komuge, Kisumwa na Rabol. Inahudumia vijiji zaidi ya 27; population wide ambayo inakwenda kupata huduma pale sio chini ya watu 50,000 kulingana na jiografia ilivyokaa. Umbali wa kutoka kituo hiki cha afya mpaka Hospitali hii ya Wilaya inayojengwa ni zaidi ya kilometa 40 ndiyo maana mara ya kwanza nilikuwa namuomba sana tupate daraja la Mto Moli ili kufupisha safari hii.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu la kwanza la nyongeza; Mheshimiwa Waziri haoni sasa kuna umuhimu wa kupandisha hadhi hizi zahanati ambazo ziko kwenye kata zinazozunguka kata hii ya Kinesi ikiwemo Kata ya Kyang’ombe, Banaki, Komuge na Kisumwa ili zile zahanati ziweze kutoa huduma kama vituo vya afya kukisaidia hiki kituo cha afya cha Kinesi population wide inayokwenda pale?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la nyongeza Mheshimiwa Waziri huoni kuna umuhimu sasa kwa muktadha wa majibu haya hiki Kituo cha Kinesi angalau wpaate ambulance ili iweze kuwasaidia kwa umbali huo wa kilometa 40 wanaosafiri hasa tunapopata wagonjwa wa dharura kama akinamama wajawazito na wagonjwa wengine ambao wako serious kwenye matatizo kama haya? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Wambura Chege kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatetea wananchi wa Jimbo la Rorya na kuhakikisha wanapata huduma bora za afya ili tuhakikishe kwamba wananchi wale wanaona matunda mazuri ya Serikali yao.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kituo hiki cha afya kinahudumia wananchi wengi katika vijiji takribani 27 na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza namna ambavyo Serikali imeendelea kutoa fedha zaidi ya shilingi milioni 900 katika kituo hicho; kwanza, kuhakikisha majengo yanakamilika lakini pia kuendelea kukipanua kituo kile ili kiendelee kutoa huduma bora kwa hao wananchi wengi ambao kituo kinawahudumia. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tutaendelea kukiboresha kituo kile cha afya, lakini pia zahanati zinazozunguka kituo cha afya, sera na mpango wa maendeleo ya afya msingi tunahitaji kituo cha afya katika kila kata na kila zahanati katika kila Kijiji. Kwa hiyo, kama kuna zahanati ambazo ziko nje ya kata ilipo Kituo cha Afya cha Kinesi tunaweza kupanddisha hadhi zahanati hizo zikawa Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ambulance, ni kweli tunahitaji kuwa na magari ya wagonjwa kwa ajili ya dharura na tutakwenda kuweka mpango wa kuhakikisha kituo hiki cha Kinesi kinapata gari la wagonjwa ili kiweze kurahisisha huduma za rufaa.