Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha Ujenzi wa Chuo cha VETA Shaurimoyo – Ludewa ili kuzalisha Wataalam watakaosaidia kutekeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma utakapoanza?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ina uhaba mkubwa wa walimu kwenye shule zake za msingi, jambo linalosababisha wazazi kuchangishwa kati ya 15,000 mpaka 20,000 kwa ajili ya kuajiri walimu wa kujitolea kwenye Kata ya Mlangali, Mavanga na Lugarawa. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha kwenye shule za msingi za Wilaya ya Ludewa ikiwa ni pamoja na kuwaajiri wale walimu waliojitolea kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, shule 23 za sekondari zilizopo Jimboni Ludewa hazijafanyiwa ukaguzi muda mrefu. Je, ni lini Wizara itatoa maelekezo kwa wadhibiti ubora wa elimu walioko pale Ludewa waweze kufanya ukaguzi huo kuliko kuendelea kusubiri wakaguzi kutoka kanda? Ahsante.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto ya uhaba wa walimu katika maeneo mbalimbali nchini. Na kama mnavyofahamu hivi punde tu Mheshimiwa Rais aliagiza kwamba, wale walimu 6,000 ambao wa kuziba nafasi utaratibu wake uweze kufanyika mapema. Lakini kama mnavyofahamu mwaka jana mwezi wa Novemba Serikali ilitoa kibali cha kuajiri walimu zaidi ya 13,000. Tunaamini kati ya wale 13,000 walimu karibu elfu nane walikuwa tayari wameshasambazwa shuleni na walimu 5,000 walikuwa wanaendelea na mchakato.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika magawanyo huu sasa na hawa 6,000 watakaopatikana hivi punde watakwenda kutatua tatizo lile la upungufu wa walimu katika Halmashauri zetu ikiwemo na Halmashauri au Wilaya ya Ludewa.

Mheshimiwa Spika, hili la wazazi kuchangishwa, naomba tulibebe. Tutashirikana na wenzetu wa TAMISEMI tuweze kuangalia namna gani jambo hii linaweza likachukuliwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amezungumzia suala la ukaguzi wa shule, Wizara inaendelea na kuimarisha Kitengo hiki cha Wadhibiti Ubora, ambapo hatua tofauti zimeweza kuchukuliwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018/2019 mpaka hii 2020/2021. Wizara imeweza kufanya mambo yafuatayo; kwanza, tumeweza kusambaza Wadhibiti Ubora 400 katika Halmashauri zote nchini.

Pia katika kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2020/ 2021 jumla ya ofisi za Wadhibiti Ubora 100 katika Halmashauri zetu zimeweza kujengwa na mpaka hivi navyozungumza tunaendelea na ujenzi wa ofisi 55 na ukarabati wa ofisi 31. Sambamba na hilo, Wizara yangu tumeweza kununua na kusambaza magari 83 kwenye Halmashauri tofauti tofauti.

Mheshimiwa Spika, lengo la kufanya hayo yote ni ili kuimarisha Kitengo chetu hiki cha Udhibiti Ubora hasa katika Halmashauri zetu. Kwa kufanya hivyo, tunaamini kutokana na ongezeko la shule nyingi ambazo zinahitaji kukaguliwa za msingi na sekondari tutaweza sasa kuzifikia shule hizo kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sasa Wadhibiti wetu wa Ubora hawa wa Wilaya watakwenda kufanya ukaguzi katika shule hizi za msingi na sekondari katika maeneo waliopo badala ya kutumia wale Wadhibiti Ubora wa Kanda ambao walikuwa wanakagua hizi shule katika kipindi kilichopita. Ahsante.

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha Ujenzi wa Chuo cha VETA Shaurimoyo – Ludewa ili kuzalisha Wataalam watakaosaidia kutekeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma utakapoanza?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Hitaji ya chuo cha VETA katika Jimbo la Ludewa linafanana sana na hitaji ya chuo cha VETA katika Jimbo la Manyoni Mashariki.

Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango wa kuhakikisha kwamba Jimbo la Manyoni Mashariki hususan Wilaya ya Manyoni inakwenda kujengewa chuo cha VETA? Ahsante sana.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mbunge wa Manyoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimeeleza mara kadhaa katika Bunge lako hili Tukufu kwamba hivi sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo 29 katika Halmashauri mbalimbali nchini, ambapo jumla ya shilingi bilioni 48.6 zimeweza kutengwa na zinaendelea kutumika kwa ajili ya ujenzi huo. Serikali inaendelea na utaratibu wa kutafuta fedha kwa sababu lengo kuu ni kuhakikisha kwamba katika kila Wilaya na Mkoa tunakuwa na VETA.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge mara tu fedha zitakapopatikana tutahakikisha kwamba tunakwenda kujenga VETA katika Halmashauri ya Manyoni lakini na Halmashauri zote ambazo bado hazijafikiwa na VETA nchini. Ahsante.