Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Primary Question

MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:- Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ya ujenzi wa bwawa la maji katika Kata ya Mikangaula Wilayani Nanyumbu itatekelezwa?

Supplementary Question 1

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na andiko la huu mradi pamoja na kujenga bwawa, ni kuhakikisha kunakuwa na mtandao wa maji kutoka kwenye bwawa kuelekea Vijiji vya Lipupu, Maratani, Mchangani A na Malema na baadhi ya Vijiji vya Kata ya Mnanje:-

Swali je, ni lini utekelezaji wa uwekaji wa miundombinu ya maji utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ahadi hii ya kujenga bwawa katika Kata ya Mikangaula ilitolewa tarehe 28/07/2011 na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Mrisho Jakaya Kikwete. Swali langu; ni miaka 11 ndiyo mradi huu unatakiwa kutekelezwa:-

Je, Wizara haioni wakati umefika ahadi ya viongozi wa juu hasa Marais wetu ikachukuliwa kama ni agizo na ikatekelezwa haraka iwezekanavyo, badala ya kusubiri miaka 11 ndiyo itekelezwe? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mtandao wa maji tunaelekea sasa kwenda kuutekeleza. Katika kutengeneza mabwawa, tunaanza kuhakikisha uhakika wa chanzo cha maji ambapo sasa bwawa limeshafika asilimia 95 na sasa hivi kazi zitakazofuata ni kuukamilisha. Hii 5% iliyobaki kufikia mwisho wa mwezi wa Tano au kabla ya kumaliza mwaka huu wa fedha ni kuona kwamba tunakwenda kusambaza mitandao ya mabomba kuelekea kwa watumiaji wetu wote wa Nanyumbu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, amesema mradi umeanza tarehe 28/07/2011. Kama wote tunavyokumbuka, miradi hii kwa kipindi hicho ilikuwa chini ya Halmashauri zetu za Wilaya. Kwa hiyo, wale wenzetu kidogo walishindwa kumaliza miradi hii na ndiyo maana RUWASA ikaanzishwa. Sote tunafahamu RUWASA sasa hivi ina mwaka mmoja na miradi korofi yote kama huu imekuwa ikifanikiwa kwa kuweza kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge napenda tu kukuhakikishia kwamba tunakwenda kutimiza ahadi hii kwa kutumia RUWASA na wote tunafahamu namna RUWASA ambavyo wamekuwa wakikamilisha miradi chechefu, kwa hiyo, na mabwawa haya pia yanakwenda kukamilika. (Makofi)