Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA G. MWANDABILA Aliuliza:- (a) Je, ni lini mahabusu wataruhusiwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali wakiwa Gerezani? (b) Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuwezesha Magereza kwa chakula kwa kuwa mkakati wa kila Gereza kujitegemea kwa chakula umeshindwa kutekelezeka?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza japo majibu walionipa angalau yanaridisha.

Swali la kwanza, natamani kufahamu; kwa kuwa magereza wao wamekiri bado uwezo wa kulisha mahabusu na wafungwa ni mgumu, upo kwa asilimia 54. Je, hawaoni sasa ipo haja ya hawa mahabusu kuweza kushirikishwa kuzalisha chakula chao tu kwa sababu maandiko yanasema kila mtu atakula kwa jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili natamani kufahamu; tunafahamu kabisa Magereza changamoto ya magodoro ni kubwa sana. Katika changamoto hiyo, Serikali inawajibika kuhakikisha magodoro yanakuwepo kule, lakini hali bado ni ngumu; na tunafahamu kuna taasisi nyingi sana zinazokuwa zinahitaji magodoro kama shule na Serikali haiwapatii:-

Je, Serikali haioni iko haja sasa ya mahabusu au wafungwa wote wanaokuwa wanafungwa wakawa na kigezo cha kwenda na magodoro yao ili kuweza kupunguza changamoto ile kwa sababu sio wote wanashindwa kuwa na godoro hilo kuliko kuiongezea Serikali mzigo? Ahsante. (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kanuni au Sheria, hakuna eneo ambalo linakataza kwamba watu kuingia na vitu wanavyovitaka katika Magereza, lakini sasa sababu mbili ndizo ambazo zinatufanya mpaka tufike hatua ya kusema kwamba haiwezekani kila mtu aingie na kitu chake Gerezani. Sababu ya kwanza, moja ni busara ya Jeshi la Magereza kama Jeshi la Magereza. La pili, ni sababu za kiusalama.

Mheshimiwa Spika, unapochukua kitu ukakiingiza kwenye Magereza, maana yake kinaweza kikachomekwa kitu kingine ndani yake ambacho kinaweza kikaja kuwadhuru wengine. Ndiyo maana hata ukifika wakati ukitaka kuleta chakula au dawa au kitu kingine, lazima tukithibitishe tukihakikishe na tujue kwamba hiki kina usalama kwako, kwetu tunaokipokea na kwa yule ambaye anakwenda kukitumia. Kwa hiyo, suala la kila mtu aingie na godoro lake, pazito kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine tunaweza tukajikuta tunatengeza tabaka kwamba kuna mtu anaweza kuingia na godoro lake na mwingine akashindwa. Kwa nini sasa na mahabusu nao wasishiriki katika shughuli za uzalishaji? Mahabusu na wafungwa wote ni binadamu, lakini hata akiitwa mfungwa, maana yake kesi yake imeshakuwa held, kwa maana ya kwamba imeshahukumiwa aende jela miaka mingapi? Kwa hiyo, yule tunayo sababu ya kumwambia sasa nenda kalime, nenda kazalishe kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya gereza. Sasa huyu mahabusu bado kesi yake haijahukumiwa kwa hiyo, yupo pale. Kusema tumchukue tukamfanyishe kazi, tukamlimishe bado kidogo busara hiyo hatujafikia. Nakushukuru. (Makofi)

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA G. MWANDABILA Aliuliza:- (a) Je, ni lini mahabusu wataruhusiwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali wakiwa Gerezani? (b) Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuwezesha Magereza kwa chakula kwa kuwa mkakati wa kila Gereza kujitegemea kwa chakula umeshindwa kutekelezeka?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kufuatana na majibu ya Naibu Waziri anasema kwamba mahabusu wana hiari ya kufanya shughuli mbalimbali; kwa sababu mahabusu wengi wanakaa muda mrefu Gerezani; miaka mitatu, nane, wengine mpaka tisa, wengine mpaka 12: Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kupeleka vifaa mbalimbali ambavyo watakuwa wanajiendeleza mle ndani kama ni kushona cherehani; yaani ujuzi mbalimbali wakiwa mle mle ndani, siyo kwenda kufanya kazi nje, kwa kipindi ambacho wanasubiria kesi zao kama zimemalizika wameachiwa huru au kama wamefungwa. Kwa kipindi hiki, kwa nini msipeleke waendeleze ujuzi wao wakiwa mle gerezani? (Makofi)

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, Mheshimiwa Hamza Chilo, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mahabusu hawapaswi kufanya kazi kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa na pia sheria za nchi yetu. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kwamba katika maeneo ambayo tumepita na kuangalia, wengine wanapenda kufanya zile shughuli za hiari yao kabisa na wanapenda kufanya kazi. Nakubaliana na Mheshimiwa Matiko kwamba katika maeneo ambako tumekuwa na shughuli ambazo haziwaruhusu kutoka nje, kwa sababu mahabusu wanategemeana na aina ya kosa alilolikosa.

Mheshimwia Spika, kwa makosa ya kawaida unaweza kumruhusu hata kutoka kidogo, lakini kwa makosa yale magumu, makubwa, siyo rahisi kumruhusu. Sasa katika maeneo ambayo tumefungua bakeries kwenye maeneo ya Magereza na Shule za Kushona ambazo ziko ndani ya Magereza, kwa kweli wanazifurahia na wanafanya.

Mheshimiwa Spika, tunachukua maoni yake hapa kwamba hicho anachokisema ndicho kinachofanyika hata kwa sasa. Tutajitahidi tu kuongeza uwekezaji kuhakikisha kwamba tunapeleka mashine hizo za kushona au zinazofanana na shughuli za kawaida zinazoweza kufanyika ndani ya Magereza ili waweze kujishughulisha kwa sababu kusema ukweli mtu kukaa bila kufanya shughuli yoyote kwa muda mrefu inakuwa siyo jambo ambalo kibinadamu linakubalika. Hata wao unaona kabisa nimesema nao, wanasema tuleteeni shughuli za kawaida tufanye. Kwa hiyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge. Ahsante. (Makofi)