Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka miundombinu mizuri ya barabara katika Mbuga ya Ibanda na Rumanyika ili kuvutia watalii?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kinipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa juhudi zinazoendelea kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Ibanda na Rumayika.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwenye awamu iliyopita ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, alitoa maelekezo kuwekwa mipaka maeneo ambayo yalikuwa yamevamiwa na wananchi na akaelekeza maeneo haya yawekewe mipaka ili wananchi wasiendelee kuvamia yale maeneo, na Serikali ilileta wataalam wakaja kupitia maeneo yale. Baada ya kupitia, Serikali bado haijaweka mipaka kwenye maeneo hayo ya hifadhi na wananchi wameendelea kubugudhiwa. Je, ni lini Serikali itaweka mipaka inayotambulika ili wananchi hawa wasiendelee kusumbuliwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye hifadhi hizi pamoja na kutengwa sisi tunashukuru sana Serikali, lakini bado hatujaona juhudi za Serikali za kuweka vivutio ambavyo vitawavutia watalii. Ni lini Serikali italeta vivutio katika Hifadhi ya Ibanda na Rumanyika ili kuvutia watalii waje katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Swali lako la pili halijaeleweka Mheshimiwa Bilakwate; Serikali ilete vivutio tena wakati hifadhi zenyewe ndiyo vivutio?

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, samahani, kwenye hizo hifadhi hakuna wanyama, yaani hakuna vile vivutio ambavyo vinaweza kuwavutia watalii kuja kuangalia.

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye kipengele (a) na (b), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze na mipaka. Ni kweli Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikiainisha maeneo mbalimbali yanayohusiana na hifadhi kwa kuweka mipaka katika maeneo ambayo yanahusiana na uhifadhi. Katika Hifadhi ya Ibanda – Kyerwa na Rumanyika tulifanya tathmini baada ya wataalam wetu kwenda kuainisha mipaka na utekelezaji wake tunaendelea kuandaa mazingira ya kupeleka wataalam kwa ajili ya gharama za uthamini ikiwemo kuainisha maeneo yenye changamoto hizi za uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, lakini tunatoa maelekezo kwenye upande wa maeneo haya ambayo tayari yamesha ainishwa, kwamba wananchi ambao wanazunguka maeneo haya wasiendelee kubugudhiwa mpaka pale ambapo wataonyeshwa eneo ambalo linahitajika kwaajili ya uhifadhi na maeneo ambayo wataachiwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upande wa vivutio. Serikali inatambua kwenye hifadhi hizi ambazo ni mpya ambazo tayari zimeshatangazwa, zina wanyama lakini baadhi hawapo, hasa vivutio vya wanyama wakali kama simba na tembo. Serikali ina mpango wa kupeleka mbegu za wanyama hawa ili kuimarisha maeneo yenye uhifadhi katika maeneo hayo ili kuendelea kuongeza idadi ya Wanyama katika hifadhi hizi, lakini pia vivutio mbalimbali vinavyohusiana na mambo ya mali kale na mambo mengine ambayo yanahusiana na vivutio. Naomba kuwasilisha.