Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. HASSAN S. MTENGA Aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza ruzuku katika mpango wa utoaji bure Elimu ya Sekondari na Msingi?

Supplementary Question 1

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya kutoa Elimumsingi Bila Malipo kwa miaka mitano mfululizo, kuna changamoto ambazo zimejitokeza kutokana na zoezi hili. Moja ya eneo kubwa ni kwamba vigezo vinavyotumika kupeleka fedha kidogo vinasumbua, hasa kwa shule ambazo zina wanafunzi wachache wakati baadhi ya mahitaji hasa ya utawala yanafana. Je, Serikali haioni umefika wakati wa kupitia upya vigezo hivi na kuona namna bora ya kupeleka fedha hasa kwenye eneo la utawala ili kutatua tatizo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Elimumsingi kwa definition ambayo imekuwa ikitolewa ni kuanzia Chekechea mpaka Kidato cha Nne. Hapa pana Kidato cha Tano na cha Sita ambapo hakuna facility na Elimu ya Juu kuna mikopo.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuhusisha kidato cha tano na cha sita kwenye elimumsingi ili nao wapate elimu hii ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli alichoeleza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina vigezo vyake ikiwemo idadi ya wanafunzi na ndiyo mfumo ambao tunautumia kupeleka hiyo ruzuku ya fedha katika shule zote nchini. Bahati mbaya sana kwenye zile shule ambazo wanafunzi wake ni wachache tumekuwa tukipeleka fedha kulingana na mahitaji ama kulingana na idadi yao ambayo ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na nia njema na ndiyo maana moja ya nia njema yake ni kuanzisha Elimu Bila Malipo. Kutokana na hiyo nia njema, sasa hivi nafikiri ninyi nyote mmejua, moja ya jitihada kubwa ya Serikali ilikuwa ni kuboresha miundombinu hususan katika yale maeneo ambayo shule nyingi zimekosa uhitaji na Wabunge wote ni mashuhuda sasa hivi, Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, mabwalo pamoja na maabara. Ndiyo maana nimeeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba, kulingana na bajeti na mahitaji tutaendelea kutenga fedha. Hata hivyo, hiyo changamoto anayoielezea Mheshimiwa Mbunge tunaipokea na kutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita ambao Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba hawahusiki na Elimu Bila Malipo. Moja nipokee, lakini hili ni suala la kisera; na kwa sababu Serikali ipo hapa ndani, tumelipokea hilo na tutalifanyia kazi tuone mahitaji yake kulingana na mazingira tuliyonayo. Ahsante sana.