Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Primary Question

MHE. JUMANNE A. SAGINI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itazipatia umeme kaya na vitongoji ambavyo havijapatiwa umeme Wilayani Butiama?

Supplementary Question 1

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Jimbo la Butiama lina vitongoji 370, katika awamu zote mbili nilizopita za REA ni vitongoji 147 tu vilipata umeme sawa na asilimia 40. Sasa Naibu Waziri ananihakikishiaje kwamba pia kama njia ya kumwenzi baba wa Taifa, vitongoji 223 vilivyosalia vitapata umeme katika awamu ijayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; sera ya Wizara ni kwamba unapopita umeme taasisi za elimu au afya zilizoko katika maeneo hayo zinapaswa pia kuhakikisha kwamba zinafungiwa umeme, lakini ninazo taarifa katika Jimbo la Butiama zipo shule za sekondari, vituo vya afya na zahanati ambavyo havijapata umeme. Je, Waziri atanihakikishiaje kwamba vituo hivyo vinapata umeme, orodha ninayo ndefu lakini atuhakikishie kwamba TANESCO walioko kule wanaweza wakashusha umeme kabla ya utekelezaji ya awamu ijayo anayosema inayoanza mwezi Julai?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Sagini, Mbunge wa Butiama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Butiama ni mojawapo ya Wilaya ambayo tayari zimepata umeme katika vijiji vyote vilivyoko na kweli kuna baadhi ya vitongoji ambavyo havijapata umeme. Upelekaji wa umeme kwenye vitongoji ni zoezi endelevu na ni kwa awamu na tunapeleka umeme katika maeneo haya kupitia TANESCO kufanya kazi zao za kila siku lakini pia kupitia katika miradi tuliyokuwa nayo ambayo ilikuwepo densification I, densification IIA, IIB na sasa mwezi wa Saba tutaanza densification IIC ambapo kama tulivyosema tutapeleka vitongoji 648.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vitongoji vyote vilivyoko katika Wilaya ya Butiama, awamu kwa awamu vitapelekewa umeme na vyote vitapatiwa umeme vyote kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, nipende kusema kwamba ni kweli zipo baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikiachwa bila kupelekewa umeme, lakini wakati wa kuzindua mradi wa REA, awamu ya tatu, mzunguko wa pili, maelekezo ya Wizara ambayo yalitolewa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati, yalisema kwamba katika kupeleka umeme katika awamu hii ya tatu, kisiachwe kijiji au eneo lolote ambalo lina taasisi ya umma ambayo haitapelekewa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu nirudie maelekezo yake kwamba wakandarasi wote wanaopeleka umeme katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili, wasiache kupeleka umeme katika taasisi zote za umma ambazo ziko katika maeneo yetu. Vile vile, uniruhusu nisisitize maelekezo mengine mawili ambayo Mheshimiwa Waziri aliyatoa, mojawapo ikiwa ni kwamba watakapokwenda Wakandarasi kupeleka umeme katika maeneo yetu, pamoja na watu wengine na taasisi nyingine watakazoenda, wahakikishe wanapiga hodi kwa Waheshimiwa Wabunge ili Waheshimiwa Wabunge waweze kuwaonyesha maeneo ambayo yana changamoto zikiwa ni pamoja na hizo ambazo ni taasisi zetu za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, agizo la mwisho, alilolitoa ni kwamba ni lazima upelekaji wa umeme ukamilike ndani ya muda ambayo ni kufikia Disemba, 2022.

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. JUMANNE A. SAGINI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itazipatia umeme kaya na vitongoji ambavyo havijapatiwa umeme Wilayani Butiama?

Supplementary Question 2

MHE. FLATEI I. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Butiama ni majimbo ya zamani kama ilivyo Mbulu Vijijini na changamoto ya umeme karibu zinafanana. Zipo Kata za Masieda, Eda Chini, Eshkesh ambazo Mheshimiwa Waziri naye alikuja akaziona. Je, ni lini sasa maeneo hayo niliyoyataja yatapata umeme?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa REA, unapeleka umeme katika vijiji vyote vilivyokuwa vimebakia katika awamu zilizotangulia bila kupelekewa umeme.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba katika awamu hii inayoanza ambayo pengine imeshaanza kwenye maeneo mengine na kufikia Disemba, 2022 vijiji vyote vilivyo katika eneo lake vitapata umeme na vitongoji vitapata umeme kupitia utaratibu huo huo kwa sababu mkandarasi anapopeleka umeme kwenye Kijiji kimsingi anaunganisha wateja kwenye vitongoji na kuunganisha wateja kwenye kaya na mteja mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwa ujumla kwamba vijiji vyote Tanzania Bara vilivyokuwa havina umeme, vitapelekewa umeme katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa REA bila kukosa.

Name

Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Primary Question

MHE. JUMANNE A. SAGINI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itazipatia umeme kaya na vitongoji ambavyo havijapatiwa umeme Wilayani Butiama?

Supplementary Question 3

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itatusaidia kupeleka umeme katika Kata ya Kasokola na Mwamkulu?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian, Mbunge wa Mpanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyote vilivyokuwa havijapelekewa umeme katika awamu zilizotangulia zitapelekewa umeme katika awamu hii ya tatu, mzunguko wa pili na vijiji kwa kuwa viko kwenye kata, kata hizo pia zitakuwa ni sehemu ya kupata umeme huo ambao Serikali imejipanga vyema kabisa kuhakikisha kwamba umeme unawafikia wananchi katika kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi Aprili.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JUMANNE A. SAGINI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itazipatia umeme kaya na vitongoji ambavyo havijapatiwa umeme Wilayani Butiama?

Supplementary Question 4

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Matatizo yaliyopo katika Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara yanaonyesha uhalisia wa Wilaya zote ndani ya Mkoa wa Mara kwenye kadhia ya umeme na kwa sababu umeme unaweza kuimarisha usalama na kuweza kukuza uchumi kwa maana kupitia uanzishwaji wa viwanda na vitu vingine. Ningependa kujua ni lini sasa Serikali itahakikisha umeme unapatikana katika wilaya zote ndani ya Mkoa wa Mara?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wilaya zote Tanzania Bara zina umeme, maeneo machache katika wilaya hizo ndiyo hayajafikiwa na umeme, kwa hiyo nimhakikishie kwamba maeneo hayo machache ambayo bado hayajafikiwa na umeme kwa maana ya vijiji yatakuwa yamepatiwa umeme katika miezi 18 ijayo. Kama ni umeme wa uhakika kama nilivyotangulia kujibu maswali yaliyotangulia ya msingi, Serikali inaendelea kuwa na jitihada za kuhakikisha inatenga bajeti kuhakikisha inawawezesha TANESCO kuendelea kurekebisha miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, pia Serikali inatekeleza miradi mikubwa sana ya ufuaji wa umeme Tanzania bara ikiwemo ya Mwalimu Nyerere itakayozalisha megawatt 2,115, Rusumo megawatt 80, Kagati megawatt 14, Ruhudji megawatt 358 na Rumakali megawatt 222. Miradi yote hiyo ikikamilika tutaweka umeme mwingi sana kwenye grid yetu ya Taifa na kuweza kumpatia kila mmoja umeme wa kutosha. Kwa hiyo tunawahakikishieni Wabunge wote kwamba umeme upo na utaendelea kuongezwa, tutarekebisha miundombinu yetu ili kila moja aweze kufikiwa na umeme ili Tanzania ya viwanda iweze kuwa ya kweli.

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. JUMANNE A. SAGINI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itazipatia umeme kaya na vitongoji ambavyo havijapatiwa umeme Wilayani Butiama?

Supplementary Question 5

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo la Manyoni Magharibi ambako mimi natoka kwa maana ya Halmashauri ya Itigi kuna vijiji 15 na vitongoji kadhaa bado havijafikiwa umeme. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje juu ya vijiji vyangu ni lini vitapata umeme?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa ambayo imejengewa kituo kikubwa kabisa cha kupoza umeme na kipo kingine kinachoongezwa kikubwa pia kwa ajili ya kupitisha umeme kutoka Iringa kupita Singida kwenda Arusha kwa ajili ya kwenda nje ya nchi ambapo ni Arusha kwenda Kenya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida ni mkoa ambao hauna matatizo ya umeme na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo machache ambayo kwake bado hayajapata umeme, yataendelea kupelekewa umeme kwa kupitia taasisi yetu ya TANESCO, lakini kwa kupitia awamu mbalimbali ikiwemo REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili, ambao kwa sasa unaendelea kwa sababu umeme tunao wa kutosha na tunao uwezo wa kupeleka lakini ni kwa awamu kwa awamu kama nilivyotangulia kusema.

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. JUMANNE A. SAGINI Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itazipatia umeme kaya na vitongoji ambavyo havijapatiwa umeme Wilayani Butiama?

Supplementary Question 6

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Meatu liko nyuma katika utekelezaji wa umeme wa REA, kwa kuwa ni asilimia 46 tu ndiyo iliyotekelezwa. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka kwanza kwenye kata saba ambazo hazijafikiwa kabisa ambazo ni Kata ya Mwamalole, Mwamanongu, Mwabuzo, Imalaseko, Kimali na Mbushi? (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika maswali mengine yaliyotangulia, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TANESCO na REA tunapeleka umeme na tumejipanga kupeleka umeme katika maeneo ya vitongoji na vitongoji hivyo ndimo kata zinapopatikana, ndimo vijiji vinapopatikana na wilaya inahudumia maeneo hayo hayo. Kwa hiyo katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili, hatujabaguwa nani aanze na nani afuate tutakwenda kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme katika awamu hii ya tatu, mzunguko wa pili, tumefanya mambo mawili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na uhakika wa kupeleka umeme katika maeneo yote kwa wakati mmoja. Jambo la kwanza tulilolifanya tumegawa kazi kidogo kwa wakandarasi wachache wachache kuhakikisha kwamba basi mkandarasi anakuwa hana kazi kubwa za kufanya na hivyo kushindwa kumaliza kazi yake kwa wakati katika eneo alilopewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili tulilolifanya, tumehakikisha kwamba tunapeleka wasimamizi katika maeneo hayo ya kanda na kwenye mikoa ambayo yatakuwa yanatokea REA kwenda kuhakikisha kwamba wale wakandarasi tuliowapeleka wanafanya kazi.

Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Leah kwamba katika kipindi hiki cha REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili, ataona matunda makubwa na mafanikio makubwa ya upelekaji wa umeme katika maeneo yote ya vijiji na vitongoji tuliyokuwa nayo.