Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA Aliuliza:- (a) Je, Serikali inasemaje kuhusiana na ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto nchini? (b) Je, kwa nini Serikali haifanyi tafiti kujua sababu za kesi nyingi kushindwa kuwatia hatiani wabakaji na kuja na mpango mpya wa kudhibiti vitendo hivyo?

Supplementary Question 1

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza niipongeze Serikali kwa jitihada inazochukua katika kupiga vita ukatili wa watoto kwa suala la ubakaji. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza litalenga kwenye majibu ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na tafiti ambyao amefanya na kututaka sisi sasa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla kuweza kusaidia katika kutatua changamoto hizi.

Swali langu liko kwamba, je, ninyi kama Serikali mmejipangaje kuhakikisha kwamba vitengo vyote vinavyoshughulikia masuala ya sheria na kutoa haki vinashirikiana kikamilifu ili kuweza kutokomeza masuala haya ambayo mmeyatafiti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na Sheria Namba 21 ya Mtoto ya mwaka 2009. Sheria hii imeweka wajibu na jukumu la wazazi ama walezi kuweza kuwalinda watoto dhidi ya ukatili ikiwemo hili la ubakaji.

Je, mmekwama wapi katika kutekeleza sheria hii kiasi kwamba tunaona hakuna mzazi au mlezi anayeweza kuchukuliwa hatua pale ambapo mtoto anapatikana na makosa haya tukizingatia ndoa zinavunjika kwa wingi na watoto wanatelekezwa na inasababisha kufanyiwa vitendo hivyo vya ukatili, lakini pia wale wazazi ambao wanabaki, akina baba wanaweza kufanya vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto wao wenyewe. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na hilo? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mbunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza lilikuwa linasema kwamba, je, Serikali ina mpango gani au je, kuna jitihada gani nyingine ambazo zimechukuliwa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba, tunatokomeza vitendo hivi. Kama Serikali tumechukua jitihada nyingi na tumechukua jitihada mbalimbali, lakini bado tunaendelea kuchukua jitihada ya kwanza ikiwemo ya kuendeleza kutoa elimu kwa jamii kwa sababu, tunaamini jamii ikipata elimu ya kutosha kwenye masuala haya maana yake masuala haya yanapungua au yatamalizika moja kwa moja. kwa hiyo, kama Serikali tumeanza kutoa taaluma kwanza kupitia kwenye madawati ya kijinsia ambayo mara nyingi yapo katika Jeshi la Polisi, tunayatumia yale kutoa taaluma hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tunao hawa para legals, wasaidizi wetu wa sheria ambao wako huko, wanatusaidia kuipa jamii taaluma. Pia tunavitumia vyombo vya habari kuhakikisha kwamba, taaluma inafika kwa jamii, lakini kizuri zaidi tunaenda kutengeneza mazingira ya kuipa nguvu sheria hii Namba 21 ya mwaka 2009 ili kuhakikisha kwamba, sheria inafuatwa na wananchi kwa kiasi kikubwa jamii inapungukiwa na matendo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine la pili ameuliza kwamba, sheria hii inakwama wapi? Naomba pia kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakati tunaipitia sheria hii tumegundua kwamba, sheria hii ipo kimadai zaidi rather than kijinai. Sasa ukitazama unakuta kwamba, watu wanaweza wakafanya vitendo hivi wakitegemea kwamba, wao watafunguliwa kesi zaidi za madai na kwa sababu, madai si analipa. Kwa hiyo, sasa unakuta haiko kijinai zaidi. Kwa hiyo, unakuta sheria ndio maana unafika wakati utendaji wake wa kazi unakuwa haupo vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni ugumu wa wananchi kwenda kutoa ushahidi, ugumu wa mashahidi. Ukimchukua mtu akitoa ushahidi huko nyumbani ukikaa naye atatoa ushahidi vizuri tu, tena atatoa ushahidi maana yake ambao uko evident, lakini kesho twende mahakamani ndio inakuwa ngumu. Sasa na mahakama nayo ikiwa siku mbili, tatu, mara nne tano umeitwa hujaenda kutoa ushahidi maana yake mahakama inatoa uamuzi kwa upande mmoja. Kwa hiyo, upo ugumu kwenye utoaji wa ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine sasa wanafamilia, wanamalizana tu kienyeji. Jambo limetokea kwa sababu, baba mkubwa, baba mdogo wanamalizana huko mwisho wa siku huku sheria inakuwa haipewi nguvu. Nakushukuru.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA Aliuliza:- (a) Je, Serikali inasemaje kuhusiana na ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto nchini? (b) Je, kwa nini Serikali haifanyi tafiti kujua sababu za kesi nyingi kushindwa kuwatia hatiani wabakaji na kuja na mpango mpya wa kudhibiti vitendo hivyo?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la ubakaji katika Mkoa wetu wa Iringa limekithiri sana; na kwa kuwa, tunaona kwamba, wanaobaka mara nyingi wamekuwa wakiweka Mawakili tena wasomi kwa ajili ya kutetea hizo kesi, matokeo yake wanashinda; na wale wanaobakwa kwa sababu, hawana uwezo walio wengi tumeona mara nyingi hata kesi zikienda wanashindwa. Je, Serikali inasaidiaje kuhakikisha wale watu wanapata haki zao, na hasa watoto wetu wanaobakwa?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu maswali ya kwanza kwa ufasaha sana. Jambo kubwa ambalo Serikali tumeendelea kusisitiza ni watu wetu kutokuyamaliza haya masuala kwa namna ya kindugu ama kirafiki na kuficha ushahidi, lakini kwa kile kipengele alichosema kwa wale watu ambao hawana uwezo wa kutafuta Mawakili tumetengeneza ule utaratibu wa msaada wa kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuko kwenye hatua za mwisho za kuzungumza kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ili kuweza kuanza kuwatumia Wanasheria popote pale walipo hapa nchini, wale walioko chini ya halmashauri, wale walioko chini ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, waweze kuwasaidia wananchi wale wasioweza kupata Mawakili kuwapatia msaada wa kisheria kama ambavyo viongozi wetu wakuu wamekuwa wakionesha mfano punde wanapofika katika eneo ambako kuna wananchi wana kilio, wamekuwa wakiingilia kati kuweza kuwasaidia, ili waweze kupata msaada huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshajaribisha sehemu mojawapo tulipokuwa na suala moja la mwananchi mmoja ambaye hakuweza kupata suala la wakili, lakini pia hakuweza kujua masuala ya kisheria, kuweza kusaidiwa na Wanasheria waliopo Ofisi za Mkuu wa Wilaya ama Ofisi za Mkurugenzi kwa maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye Wanasheria wote Mawakili wako chini yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la muuliza swali ni la msingi kwa sababu kwa wakati mwingine hata mwananchi akiwa na Wakili kumekuwa na utaratibu wakati mwingine Mawakili wanazungukwa na wale watenda maovu, I mean wale Wanasheria, kama mlalamikaji hana fedha wanaweza wakazungukwa na wale wenye fedha ikatokea wakashindwa kupata haki yao. Kwa hiyo, tutakapokamilisha hili, tangazo rasmi litatoka ili wananchi waweze kupata haki zao.

Name

Rose Cyprian Tweve

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA Aliuliza:- (a) Je, Serikali inasemaje kuhusiana na ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto nchini? (b) Je, kwa nini Serikali haifanyi tafiti kujua sababu za kesi nyingi kushindwa kuwatia hatiani wabakaji na kuja na mpango mpya wa kudhibiti vitendo hivyo?

Supplementary Question 3

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri na mikakati mingi ambayo wameweka kuhakikisha tunapambana na hali hii, bado kuna mianya mingi hasa kwenye sheria yetu ambayo inaenda kuchochea hii changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu nitoe mfano, kuna binti Iringa wa miaka 13, alibakwa na kijana wa miaka 18, akakiri kuwa amembaka binti huyu na adhabu yake ilikuwa ni viboko na akaachiwa. Huyu kijana anaruhusiwa kupiga kura, lakini sheria inapokuja kwenye kumbaka mtoto inamlinda kuwa bado ni minor. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na mikakati hiyo inabidi waangalie upungufu mkubwa wa kisheria ambao unakwenda kuchochea changamoto hii ya watoto kubakwa na kulawitiwa katika mikoa yetu. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea na tuko kwenye hatua tunaziangalia hizo sheria, Sheria ya Ndoa, Sheria ya Mtoto pamoja na Sheria za Mirathi ambazo kimsingi ni sheria zinazogusa jamii moja kwa moja ili tuone pale ambapo patakuwa na upungufu tuweze kurekebisha, ili kuweza kulinda jamii yetu na ustawi wa jamii wa nchi yetu.