Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Primary Question

MHE. ABUBAKAR D. ASENGA Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaongeza uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Kilombero ili kunusuru miwa ambayo haijavunwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa?

Supplementary Question 1

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watu waliofika Jimboni kwetu na kuona namna ambavyo tunalima miwa kwa bidii kwa kufuata kauli ya Mheshimiwa Rais ya nchi kujitegemea katika suala zima la sukari; na kwa kuwa hao wenye viwanda ndio waliopewa vibali vya kuingiza sukari inayopungua katika nchi yetu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mwekezaji mwingine wa kiwanda ili kuondoa monopolism ya kiwanda ambacho kipo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri na Mawaziri husika katika sekta hii ya kilimo na viwanda na biashara, watakuwa tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda kuwasikiliza wananchi hasa wakulima wa miwa Jimboni kwangu?

Name

Mwanaidi Ali Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, Serikali inaona umuhimu wa kuongeza uwekezaji wa viwanda vya sukari nchini hasa katika Kiwanda cha Kilombero ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini. Kwa upande wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Serikali na mbia mwenza, iko katika majadiliano ya kupanua kiwanda hiki na hatimaye kuongeza uzalishaji wa sukari ili miwa yote inayolimwa iweze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, napenda kumwahidi Mheshimiwa Abubakari kwamba niko tayari kuongozana naye pamoja na wataalam wangu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kujionea hali halisi ya uzalishaji katika kiwanda hicho, pale tutakapopata nafasi mara baada ya mkutano huu wa Bunge kuahirishwa. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuongezea majibu kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali iko kwenye mazungumzo na wawekezaji kadhaa angalau watatu ambao wana nia ya kuwekeza katika kujenga viwanda vipya vya sukari. Naamini kwa mazungumzo hayo, tukiwapata tutapunguza sana tatizo la sukari na nia ya Serikali ni kuona kwamba katika mwaka mmoja ujao tunajitosheleza kwa mahitaji ya sukari hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba, wiki ijayo baada ya Bunge hili mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tuna ziara katika Mkoa wa Morogoro na tutajitahidi tufike pia jimboni kwa Mheshimiwa ili kuweza kuona changamoto. Ahsante sana. (Makofi)