Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:- Je, ni lini ahadi ya Serikali ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Lushoto – Muyanta hadi Mlalo itaanza kutekelezwa?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ni muhimu sana kwa shughuli za uchumi wa wananchi wa Lushoto, hasa ukizingatia kwamba, mazao tunayozalisha kule ni mbogamboga na matunda ambayo ni rahisi kuharibika. Kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, angalau sasa barabara hii ijengwe japo kwa kiwango cha kilometa 10 kwa mwaka. Je, tunapoelekea kutengeneza bajeti Serikali haioni ni muhimu kutenga kiwango hicho cha kilometa 10 kwa kila mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hii imeendelea kutia hasara wananchi wa Mlalo, hasa nyakati za mvua. Je, Serikali sasa iko tayari kuwalipa fidia mara ambapo wananchi wanapata hasara ya mazao yao kuoza barabarani?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ambako kunazalishwa sana matunda na mbogamboga. Kwa kutambua umuhimu huo ndio maana Serikali tayari imeshakuwa na mpango wa kujenga hii barabara. Tunatambua pia kwamba, Serikali ilitoa ahadi kwamba, itaendela kujenga hii barabara walao kwa kilometa 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza kama kwenye bajeti ijayo je, tutajenga. Itategemea pia na upatikanaji wa fedha na kama itapatikana si tu kilometa 10 bali inawezekana ikawa ni kukamilisha kabisa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; endapo kama tutatoa fidia kwa wale wanaopata matatizo hasa pale ambapo mazao yao yanaharibika. Tumeshaongea na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, ili badala ya kuendelea kutengeneza kile kipande wanachokiendeleza, basi atengeneze yale maeneo ambayo ni korofi, ili yaweze kuimarika na kusitokee tatizo kama hilo. Kama kuna changamoto nyingine basi namwomba Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, anipatie. Nimwahidi Mheshimiwa kwamba, nitafika kuona hizo changamoto ambazo anazisema. Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:- Je, ni lini ahadi ya Serikali ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Lushoto – Muyanta hadi Mlalo itaanza kutekelezwa?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona, nilitaka kunyosha mikono miwili. Naomba niulize swali moja. Kwa vile Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuwa kwenye kampeni kule Vunjo aliahidi kujenga barabara ya Kilema a.k.a barabara ya Nyerere ambayo ni kilometa tisa; barabara ya Uchira kwenda Kisomachi kilometa nane tu na Mabogini – Kahe na Chekereni ambayo na yenyewe ni kilometa 22 tu kwa kiwango cha lami. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuhakikishia kwamba, barabara hizo zimeingizwa kwenye mpango wa 2021/2022? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kimei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi alizosema ni ahadi za Rais na ni ahadi katika kipindi cha uchaguzi wa 2020. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Kimei avute subira kwa sababu, bajeti ndio inaenda kwa hiyo, tutaangalia. Siwezi nikasema kwa sasa kwa sababu, hiyo bajeti bado haijapitishwa, lakini kama ni ahadi ya Rais, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kimei kwamba, ahadi za Rais zitazingatiwa katika kutekelezwa kwa bajeti zinazokuja kuanzia 2021/2022. Ahsante. (Makofi)