Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI Aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kunakuwepo na Mwongozo kwa Tour Operators wanaopandisha watalii Mlima Kilimanjaro wanaoajiri Wapagazi, Wapishi na Waongoza Misafara kwa kuwalipa ujira stahiki?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili mafupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nashukuru sana kwamba nimepewa jibu la kina na naamini tutaendelea kulifuatilia suala hili. Zaidi ni kwamba hawa operators wanakuja na watu kutoka sehemu nyingine ambao hawajui hii mikataba. Kwa hiyo, hawaajiri wale vijana ambao wanatoka kwenye vijiji karibu na ule mlima, wao hawaelewi mikataba hiyo hivyo wanalipwa kidogo sana. Je, hatuwezi kuweka uwiano fulani hasa kwa zile shughuli ambazo hazihitaji taaluma kwamba hawa operators waweze kuajiri au kuchukua vijana kutoka kwenye kundi la wale ambao wanatoka karibu na mlima kwa sababu hiyo ni njia mojawapo ya kuwapa motosha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni nyeti kidogo ni hili suala la nusu mile. Kwa vile tunajua kwamba watu wanaolinda ule mlima ni wale wanavijiji walio karibu na hifadhi ya mlima ule inakuwaje sasa suala la nusu mile. Nusu mile ni suala nimezungumza na Mheshimiwa Waziri na ni nyeti kidogo lakini nafikiri kwamba tusiliangalie kama watu wanaomba kuingia msituni isipokuwa ni ku-review ile mipaka ya msitu na kuongeza sehemu ndogo ambayo inaweza ikasaidia wale wananchi wanaoishi karibu kuweza kupata kuni na kupata malisho ya wanyama bila kuathiri miti. Siyo suala la kuingia isipokuwa ni suala la kupanua…

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya wageni kupata ajira kwenye maeneo ya hifadhi hasa kwenye Mlima Kilimanjaro. Hata hivyo, katika mwongozo wa waongoza utalii kuna kiwango ambacho wamewekewa waongoza utalii ambapo hawa watumishi kwa maana ya wanaoomba ajira wanaomba kwa kuzingatia mwongozo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto pia kwenye upande wa kiwango kwamba mtu anapokuwa anahitaji ajira basi anapunguza kiwango kinakuwa chini ya mwongozo uliopo. Waongoza utalii (tour operators) wao wanazingatia zaidi kupata faida kwenye biashara zao. Kwa hiyo, huyu mtumishi anapokuwa akiomba ajira na kwa kuzingatia kwamba waombaji wa ajira wanakuwa ni wengi basi anapunguza kiwango ili aweze kupata ajira. Kwa hiyo, kumekuwa na changamoto hii lakini tunawashauri watumishi wanaokutana na changamoto hizi waende kwenye Tume ya Usuluhishi (Mahakama ya Kazi) ambayo inasimamia haki za mtumishi yeyote anapokuwa amedhulumiwa haki yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine ni kuhusu nusu mile, naomba itambulike kwamba maeneo ya hifadhi yanapokuwa yametangazwa kuwa hifadhi hairuhusiwi kufanya kitu chochote zaidi ya uhifadhi. Nimuombe sana Mheshimiwa Dkt. Kimei, sisi kama Serikali tunapokuwa tunahifadhi maeneo haya tunatunza ili yawe kivutio na kwa ajili ya kutuletea mapato.

Kwa hiyo, tunapokuwa tunatunza, hairuhusiwi kufanya kitu chochote ndani ya eneo la hifadhi, hata kama ni kuokota kuni hairuhusiwi. Kuna maeneo mengine ambayo huwa tunawatengea wananchi kwa ajili ya kuendelea na shughuli zingine kama ufugaji, uvuvi pamoja na kilimo lakini maeneo yanayotunzwa kama hifadhi hairuhusiwi kufanya kitu chochote.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi sana kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kwa kweli nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ambayo imeletwa na Mheshimiwa Dkt. Kimei inahusika pia na masuala ya mikataba ya ajira na stahiki za wafanyakazi na mfumo mzima wa uratibu wa ajira katika eneo la Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Waziri ameliweka vizuri, tayari Wizara ya Maliasili na Wizara yetu tumeweka ule mwongozo. Tunawaomba sana wafanyakazi wote wanapokutana na changamoto zozote ambazo pia zinahusiana na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, 2004, wajitahidi kuwa wanatoa taarifa mapema sana kwenye ofisi zetu za Idara ya Kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sasa imeamua kufungua kliniki maalum. Kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi wafanyakazi wote ambao wanaona wana changamoto zinazohusiana na sheria za kazi watakuwa wanaripoti kwenye ofisi zetu za kazi ili wakaeleze zile changamoto wanazozipata kama ni za mishahara, mikataba na mambo mengine yoyote ili ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu iweze kuchukua hatua haraka ili kuondoa migogoro katika maeneo ya kazi kati ya mfanyakazi na mwajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamuomba sana Mheshimiwa Kimei kama ana mambo ya ziada aonane pia na ofisi yetu na tutaweza kulifanyia kazi na tutaagiza utaratibu na mwongozo usimamiwe vizuri. (Makofi)