Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Silvestry Fransis Koka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Mjini

Primary Question

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:- Mji wa Kibaha unakua kwa kasi hivyo mahitaji ya Watumishi yameongezeka ikiwemo Watendaji wa Mitaa, Maofisa Mifugo, Walimu pamoja na Watumishi:- Je, ni lini Serikali itatoa kibali cha ajira na kuajiri Watumishi pungufu ili kuleta ufanisi zaidi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha?

Supplementary Question 1

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kuipongeza Serikali yetu kwanza katika suala la afya ambapo tayari ilitupatia milioni 500 kwa upanuzi wa Kituo chetu cha Afya Mkoani na imetekelezwa, lakini vilevile bilioni moja na laki tano kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mradi ambao unaendelea, sambamba na hilo nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ikama ya Watumishi wa Afya ni 360 na tulio nao ni 255 tunao upungufu wa Watumishi 105 katika Idara yetu ya Afya jambo ambalo linasababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wanapokwenda kupata huduma na tukizingatia kwamba sasa Hospitali ya Wilaya inakwenda kukamilika mapema; je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ajira kwa upungufu huu ili kusudio la kutoa huduma hii liweze kukamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vilevile ikama ya Watendaji wa Mitaa ni 73 na tunao 50 na tuna upungufu wa Watendaji 23 na tunapata malalamiko sana hasa tunapofanya ziara katika mitaa yetu kwa wananchi wetu na ikizingatia kwamba tunakwenda sasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa; je, ni lini sasa Serikali itajazia upungufu wa watumishi hawa ili huduma hii iweze kuwafikia wananchi na tusiwe na malalamiko?

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Silvestry Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunamshukuru sana kwa pongezi zake kwa kazi nzuri ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi Awamu ya Tano. Swali lake la kwanza ametaka kujua ni lini tutapata Watumishi kwenye Sekta ya Afya.

Tulizungumza mara kadhaa, turudie tu kwamba tumeshaangalia changamoto hii katika maeneo mbalimbali pamoja na Kibaha, lakini tumeshaomba Kibali Utumishi kupata Watumishi wa Sekta ya Afya 12,000. Kwa wakati huo tukipata kibali hiki na kuajiri tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba watumishi hawa watapelekwa katika eneo hilo wakatoe huduma kwa watu wetu ili waendelee kufurahia maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anasema kuna upungufu katika Watendaji wa Mitaa na Vijiji na kwa sababu kuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ni kweli kwamba kuna baadhi ya maeneo katika mitaa yetu na vijiji hatuna watendaji, lakini jambo hili la uchaguzi naomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na Watanzania wengine wote, hao hao wanaosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni Watumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kupata Watendaji wa kila siku kutoa huduma kwa watu wetu, lakini wakati wa uchaguzi kama itatokea kuna kijiji au mtaa ambao hauna Mtendaji wa Kijiji, basi wale Watumishi wa Umma waliopo pale watafanya kazi hiyo kwa niaba ya Serikali na tunahakikisha kwamba jambo hilo litaenda vizuri bila tatizo. Ahsante.