Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Jimbo la Kibiti lina Kata 5 na Vijiji 17, sawa na Vitongoji 72 ambavyo vipo kwenye maeneo ya Delta lakini havina umeme:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme kwenye Visiwa hivyo? (b) Je, utapelekwa umeme wa aina gani?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY SEIF UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, nina maswali mawili ya nyongeza, moja kwa kuwa sasa wananchi hawa wa Delta wamesubiri sana kwa muda mrefu umeme wa solar; Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapelekea hata taa katika wakati huu mfupi ili waweze kujipatia huduma kwenye vituo vya afya na shule?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa wananchi wa Lungungu, Nyamatanga, Lwaluke, Kikale, Mtunda, kuna laini kubwa ambayo imepita na tayari kazi imekamilika. Je, lini umeme utakwenda kuwashwa kwenye maeneo hayo?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Ungando hii ni mara ya tatu anawaulizia wananchi wa Visiwa vya Delta, kwa kuwa ni Mbunge wa Mkoa wa Pwani natambua Visiwa hivyo na nimefanya ziara kimoja hadi kimoja vyote pamoja naye Mheshimiwa Mbunge Ally Seif Ungando.

Mheshimiwa Naibu Spika, atakubaliana na mimi kwamba kwa kuwa Serikali yetu ina nia ya kufikisha umeme vijiji vyote nchini, na kwa kuzingatia yapo maeneo kama 89 hivi ambayo yako Visiwani na wao lakini wana haki ya kupata umeme. Ndiyo maana kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Serikali iliamua kufanya upembuzi yakinifu kuainisha mahitaji na kumpata mzabuni mkandarasi ambaye atafanya kazi hiyo na mchakato huo unakamilika tarehe 26 Juni, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameainisha kwa kuwa huu muda wa mchakato mpaka mkandarasi, inawezekana ikachukua muda mrefu anauliza namna gani Serikali inaweza ikatumia mkakati wa muda mfupi wa kuwezesha hususan taasisi za umma ikiwemo kituo cha afya cha Mbwera. Tunaishukuru sana Serikali kwa mara ya kwanza kutupatia fedha za kujenga kituo cha afya Mbwera, kinapatiwa umeme mara baada ya kuanza shughuli zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge hilo tumelipokea na Wakala wa Nishati Vijijini katika maeneo ya Kiongoroni, Kiechuru, Kiasi na Mbwera itafanya kupeleka mfumo wa taa kwa ajili ya taasisi za umma ili zitoe huduma kabla mradi huu wa kupeleka nishati ya solar katika maeneo hayo kwa ajili ya matumizi ya wananchi na wa taasisi za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ameyaulizia maeneo ya Lungungu, maeneo ya Rwaluke, maeneo ya Nyamatanga, maeneo ya Mtunda. Maeneo haya kulikuwa na mradi wa REA Awamu ya Pili na mkandarasi hakufanya vizuri lakini Serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli iliamua kuanza tena mchakato na maeneo yale ambayo kazi haikukamilika ilipewa TANESCO na baada ya kupewa TANESCO wameendelea na kazi. Nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge ajiandae ili twende tukazindue kuwasha umeme kuanzia Jumatano wiki ijayo mara baada ya kuhitimisha bajeti yetu ya Serikali. Tutafanya sherehe kubwa sana katika maeneo haya kwa kuwa wamesubiri muda mrefu. Kwa hiyo, niwataarifu wakati wa Kibiti kwamba maeneo haya ambayo mmesubiri Serikali imefanya kazi na tutawasha umeme kwa kishindo. Ahsante sana.