Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 50 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 431 2019-06-21

Name

Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-

Jimbo la Kibiti lina Kata 5 na Vijiji 17, sawa na Vitongoji 72 ambavyo vipo kwenye maeneo ya Delta lakini havina umeme:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme kwenye Visiwa hivyo?

(b) Je, utapelekwa umeme wa aina gani?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwapatia huduma wananchi wake Serikali kupitia TANESCO ilifanya upembezi yakinifu kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijiji vya Pombwe, Kiongoroni, Mbuchi, Mbwera Mashariki, Mbwera Magharibi, Maporoni, Kiechuru, Msala, Kiasi, Kiomboni, Mchinga na Mfisini vilivyo katika Delta ya Mto Rufiji. Aidha, katika hatua hiyo imesaidia kupata mahitaji halisi na kubaini changamoto zilizopo katika kutekeleza mradi wa kufikisha umeme katika vijiji hivyo. Mradi wa kupeleka umeme katika maeneo hayo tajwa unatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Desemba, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya upembuzi yakinifu kufanyika vijiji vya Mbuchi, Mbwera Mashariki na Mbwera Magharibi vitaunganishiwa na umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Muhoro umbali wa kilomita 40. Ujenzi wa njia ya umeme itatumia nguzo za zege kwa kuwa maeneo mengi ni chepechepe na oevu. Vijiji vingine vilivyobaki vitapelekewa umeme wa solar kwa kuwa ujenzi wa laini ya umeme wa Gridi kupeleka katika vijiji hivyo umekuwa na changamoto kutokana na jiografia ya maeneo hayo, ahsante.