Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Augustino Manyanda Masele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:- Kampuni ya Mabangu ina leseni ya utafiti wa madini katika maeneo ya Nyakafuru, Bukandwe na Kanegere Wilayani Mbogwe; kampuni hiyo inafanya utafiti kwa kushirikiana na kampuni nyingine ya Resolute lakini utafiti huo umechukua muda mrefu. (a) Je, ni lini kampuni hizo zitafungua mgodi katika eneo lao la utafiti? (b) Kama kampuni hizo zimeshindwa kuanzisha mgodi; je, Serikali iko tayari kuona uwezekano wa kuligawa eneo hilo kwa wachimbaji wadogo wa Wilaya ya Mbogwe?

Supplementary Question 1

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika,asante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba leseni ya utafiti ya hao watu wa Mabangu imeisha muda wake na imerudishwa Serikalini. Sasa je, Serikali ipo tayari kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Mbogwe ili kusudi na wao waweze kufaidika na madini yanayopatikana katika eneo lao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, endapo Serikali itakuwa tayari kugawa hayo maeneo, je, Serikali itakuwa tayari pia kuwapatia vifaa na utaalam ili wananchi waweze kuchimba kwa kufuata kanuni na taratibu za uchimbaji wa kisasa? Ahsante. (Makofi)

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunavyoongea sasa hivi ni kwamba tayari kuna wachimbaji wadogo wapo katika leseni hiyo wanachimba na Mheshimiwa Mbunge hilo unalifahamu. Lakini tu nipende kusema kwamba kampuni hii iliomba leseni ya kufanya utafiti na wamefanya utafiti na kawaida mtu ukimpa leseni ya kufanya utafiti, hatua inayofuata kama ameridhika na utafiti huo na akaona kwamba anaweza akafanya biashara au kwa maana anaweza akachimba kibiashara, katika hali ya kawaida ni kwamba akishafanya upembuzi yakinifu, anaomba tunampatia leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu leseni hiyo imesharudishwa Serikalini na tunadhani kwamba huyu mwekezaji atakuja na maombi yake sasa baada ya kufanya upembuzi yakinifu, hatuoni haja ya kumnyima leseni hiyo kwa sababu tayari ameshaingia gharama ya kufanya upembuzi yakinifu. Lakini kama atasema kwamba hakuna biashara, haiwezekani akachimba kibiashara, basi sisi Serikali hatusiti na tumekwishakuanza kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo mbalimbali ili waweze kuendesha shughuli zao na hilo tunalifanya kwa kweli na wachimbaji wengi wamepata maeneo mengi ya kuchimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, Mbunge ametaka kujua kama Serikali tukishawapa hilo eneo basi na vifaa tutawapa? Mimi nipende tu kusema kwamba Wizara yetu hapo awali ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo ili waweze kununua vifaa, kufanya tafiti, lakini vilevile katika ruzuku hiyo tuliona kabisa kulikuwa kuna ubadhilifu unafanyika, watu walikuwa wakipewa fedha hizo wanazitumia katika matumizi mengine, tumesitisha na sasa hivi tunaangalia namna bora ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, lakini ikiwa ni pamoja na kuwafanyia tafiti ndogo ndogo kwa maana ya kufanya drilling kwenye maeneo ambayo yanaashiria uwepo wa dhahabu. Tumeshanunua rig machine kupitia STAMICO imekwisha kuanza kutoa huduma hiyo kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kama ana wachimbaji wadogo ambao wanataka kupata huduma ya hiyo rig machine basi aje STAMICO anaweza akapata huduma hiyo.