Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yussuf Haji Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Nungwi

Primary Question

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:- Upimaji wa Afya za Wanamichezo ni jambo muhimu kwa ajili ya kulinda na kuhakikisha afya zao kabla ya kushiriki michezoni kwani kumekuwa na matokeo mbalimbali ya Wanamichezo kupoteza maisha wakiwa uwanjani. Mathalani, Ismael Mirisho wa Timu ya Mbao FC, Marc Vivien Foe wa Cameroon na Cheikh Tiote wa Ivory Coast:- Je, Serikali kupitia Vyama vya Michezo vimeweka utaratibu gani kuhakikisha upimaji wa afya za wanamichezo ni jambo linalopewa kipaumbele?

Supplementary Question 1

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba ruhusa yako kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza, niwapongeze Simba Sports Club kwa kuchukua ubingwa wa Tanzania mara mbili mfululizo. (Makofi)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mnajuana eeh! (Makofi)

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, mimi nina wasiwasi kwamba agizo analolitoa Mheshimiwa Waziri kwamba linafanyiwa kazi na vilabu na hili tatizo ni kubwa linajitokeza mara kwa mara: Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuleta sheria hapa Bungeni kuvibana vilabu angalau vile vya daraja la kwanza na vile vinavyocheza Club Bingwa ya Tanzania kupima kwa lazima? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali langu ya pili, hili suala la upimaji wa afya, basi Bunge tungekuwa mfano mzuri sana, kwa sababu tuna vilabu mbalimbali vya michezo hapa Bungeni, mfano Club ya Mpira wa Miguu Ndugai Boys na michezo hii inashirikisha Viongozi Mashuhuri. Mfano mzuri Waziri Mkuu amekuwa mchezaji, pia amekuwa Kocha ambaye ameleta ufanisi mkubwa katika timu ya Bunge hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kujua, ni lini wamewahi kupima afya zao wakicheza michezo ya ndani? Au ile wanayotushirikisha katika Mabunge ya East Africa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante? (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Nikianza na swali lake la kwanza ambalo amezungumzia kwamba agizo hili huwa halifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kusema kwamba suala la kupima afya kwa wachezaji ni agizo ambalo sisi kama Wizara tunalisimamia. Ukiacha kwamba ni suala la kisera, ukiangalia kwenye kanuni za FIFA, vilevile kwenye kanuni za TFF imeelekeza wazi kwamba vilabu vyote na mashiriko yote ya mpira wa miguu yahakikishe kwamba yanapima afya ya wachezaji wao, siyo tu kipindi ambacho vilabu vinajiandaa kuingia kwenye mashindano, vilevile kabla ya usajili wowote kuweza kufanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo ni agizo, nasi kama Wizara tunalisimamia, lakini kwa ushauri ambao Mheshimiwa Mbunge ameutoa, kwamba sisi kama Wizara tulete sheria hapa Bungeni, niseme kwamba ushauri huo tumeupokea kwa sababu sisi Wabunge ndiyo ambao tunatunga sheria; na kama Mbunge ameona kwamba kuna haja ya kuwa na hiyo sheria, basi sisi kama Wizara tutakaa na kuangalia namna gani ambavyo tutaleta hiyo sheria ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili amezungumzia kuhusiana na timu ya Wabunge. Ni kweli kwamba tunayo timu ya Wabunge na timu yetu imekuwa ikifanya vizuri sana katika mashindano mbalimbali ya East Africa. Kwa hiyo, kama ambavyo nimezungumza, suala la kupima afya kwa wachezaji siyo tu kwa timu ambazo zinashiriki ligi kuu, ni jukumu la timu zote ambazo zinashiriki mashindano mbalimbali, iwe ni timu ambazo zinashiriki ligi daraja la kwanza, daraja la pili, vilevile hata kwenye michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA wanatakiwa kupima afya kwa wachezaji wao kabla ya kuanza kwa mashindano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kwa sisi Wabunge, ni jukumu letu la kuhakikisha kwamba wanapima afya zao kabla ya kuweza kushiriki mashindano yoyote au kabla ya kwenda kushiriki kwenye mashindano ambayo huwa yanafanyika nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:- Upimaji wa Afya za Wanamichezo ni jambo muhimu kwa ajili ya kulinda na kuhakikisha afya zao kabla ya kushiriki michezoni kwani kumekuwa na matokeo mbalimbali ya Wanamichezo kupoteza maisha wakiwa uwanjani. Mathalani, Ismael Mirisho wa Timu ya Mbao FC, Marc Vivien Foe wa Cameroon na Cheikh Tiote wa Ivory Coast:- Je, Serikali kupitia Vyama vya Michezo vimeweka utaratibu gani kuhakikisha upimaji wa afya za wanamichezo ni jambo linalopewa kipaumbele?

Supplementary Question 2

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika mchezo wa ngumi, asilimia 99 ya wachezaji wanapata maumivu. Je, ni lini Serikali italazimisha ma- promoter kuwakatia bima hasa mabondoa wanawake hapa nchini Tanzania? Ahsante. (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza kwa sababu Mheshimiwa Sophia Mwakagenda ni promoter pekee mwanamke ambaye anashiriki kwenye michezo ya ngumi. Nikija kwenye swali lake la msingi ambalo ametaka kujua kwamba ni lini sasa Serikali tutasimamia hawa wanaocheza michezo ya ngumi kuweza kukatiwa bima; nikiri kwamba imekuwa ni changamoto ya muda mrefu kwamba wachezaji wengi ambao wanacheza michezo ya ngumi wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu ikiwepo kutokuwa na Bima za Afya.

Mheshimiwa Spika, kwenye hivi vyama ambavyo vinashiriki mchezo huu ndondi kumekuwa kuna migogoro ya muda mrefu sana na ndiyo maana wachezaji hawa wakawa hawapati ile haki yao ya kuweza kupata Bima ya Afya. Kwa sasa hivi kama Wizara, tumeshaunda shirikisho la kuweza kusimamia mchezo huu wa ngumi nchini Tanzania. Lengo mojawapo kwenye vile vipengele ambavyo tumeviweka, ni kuhakikisha kwamba ni lazima kwa Ma- promoter kuwakatia Bima za Afya wachezaji wao.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)