Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA) aliuliza:- Shamba la uzalishaji wa Mitamba Kibaha lipo katikati ya Mji wa Kibaha na limezungukwa na makazi ya watu:- Je, Serikali ina mpango gani juu ya matumizi ya eneo hili kwa ufanisi zaidi?

Supplementary Question 1

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na juhudi za Serikali kuhakikisha kunakuwa na kituo maalum cha kuzalisha mitamba, nina maswali yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo hilo ni kubwa, na kwa kuwa eneo hilo tayari limeshakuwa na wakazi zaidi ya 300 kwenye sehemu inayoitwa Vingunguti na wakazi hao wako kwa muda mrefu sana, na wanajiendeleza na wamejiendeleza kwa muda mrefu. Je, haioni sasa ni wakati wa Serikali kulitoa eneo hilo na kuwapa wananchi hao ili waweze kuishi kwa usalama na amani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa suala hili linahusu mambo ya mifugo na ardhi, hii Tanzania ni nchi ya amani, upendo na ushikamano, na Tanzania yetu ina wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na wafanyakazi sehemu mbalimbali. Kumekuwa na tatizo la migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Je, Serikali haioni sasa ikatafuta mbinu mbalimbali mbadala za kuepukana na migogoro hiyo kwa kuwapatia maeneo wafugaji wakakaa wakaweka mifugo yao na wakulima na wananchi wengine wakaishi kwa amani na utulivu?

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo hili lilikuwa na hekta zaidi ya 1,000 na baada ya Serikali kugundua kwamba wananchi wameshaingia eneo hili, wamejenga, wamejiendeleza, tumefanya tathmini, tumewaachia wananchi zaidi ya hecta 2,900 ili waendelee kufanya shughuli zao za maendeleo.

Sasa naomba tupokee pia hoja ya Mheshimiwa Mbunge ya kwenda kufanya tathmini tuangalie kazi ya kuzalisha mitambo ambayo inafanyika eneo hili, faida yake, lakini pia na huduma za jamii za wananchi halafu tutaona busara tunafanye ili tuweze kuamua, ama tuwaachie au tuendelee kuweka mifugo pale ya kuzalisha mitambo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili anazungumzia migogoro ya ardhi; muda mfupi uliopita Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoka kuzungumza hapa namna ambavyo Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla wamepokea jambo hili la migogoro na kwamba haipaswi kuendelea. Mheshimiwa Waziri umefanya kazi hiyo, lakini pia wakuu wa mikoa na wilaya wamepewa maelekezo, lakini Wizara ya Ardhi inafanya pia mpango mahususi wa matumizi bora ya ardhi, sasa hili nalo kama kuna mgogoro pale unaendelea naomba tulipokee tuwasiliane na wenzetu mamlaka katika eneo lile tulifanyie kazi. Nia ya Serikali ni kwamba migogoro isiwepo, tunahitaji wakulima, tunahitaji wafugaji na wananchi na shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo biashara ili waendelee kufanya kwa amani na waweze kuchangia pato ikiwa ni pamoja na kulipa kodi. Ahsante.