Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA (K.n.y. MHE. DEVOTHA M. MINJA) aliuliza:- Timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars imefanya vizuri na kuliletea Taifa heshima miaka iliyopita hivi karibuni:- Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhamasisha soka kwa wanawake katika ngazi za wilaya na mikoa kuwa na timu za soka za wanawake kama ilivyo kwa wanaume?

Supplementary Question 1

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu hii ya Twiga Stars ni timu ambayo imeweza kushinda michezo mingi nje ya nchi na ni timu ambayo kwa kweli ina makombe mengi kushinda hata makombe mengine ambayo yapo ya timu zingine za wanaume zilizopo hapa Tanzania. Sasa Serikali haioni haja sasa ya kuwatambua, kuwathamini na kuwekeza katika timu hii ya wanawake ili hawa wanawake waweze kupata ajira ndani na nje ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, michezo ni ajira na soka hili la wanawake limekuwa ni ajira sasa hivi. Tunaona watoto wengi wa kike wamependa michezo. Kule Kalenga sasa hivi nikienda badala ya watoto wa kiume kuomba mipira ni wasichana wanaomba mipira kwa ajili ya kucheza soka la wanawake na tunaona nchi za Ujerumani, Japan na West Africa nchi zao zimewekeza na timu za wanawake zimeweza kushinda katika soka kombe la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali ina mkakati gani wa muda mrefu wa kujenga academy za soka la wanawake hata kwa kila kanda ili kuwawezesha hawa wanawake wakajengewa vipaji na kwa sababu michezo ni ajira. (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri lakini nikianza na swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kwamba mpango wa Serikali ni nini katika kuwekeza kwenye Timu ya Twiga Stars?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba ni kweli Timu ya Twiga Stars imekuwa ikifanya vizuri sana kwa miaka mingi na kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge umesema, kufanya vizuri kwa Timu ya Twiga Stars maana yake Serikali imefanya uwekezaji mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nikuhakikishie kwamba kama ambavyo tumekuwa tukifanya uwekezaji katika Timu ya Twiga Stars, tunaahidi kwamba tutaendelea kufanya uwekezaji zaidi ili timu hii ifanye vizuri lakini si Timu ya Twiga Stars peke yake ni pamoja na timu nyingine kwa sababu tunazo timu nyingi sana ambazo zinafanya vizuri na ni timu za wanawake ikiwemo timu ya Kilimanjaro Queens inafanya vizuri lakini pia tunayo timu nyingine ya Mlandizi Queens pamoja na timu zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uwekezaji ni mpango ambao kama Serikali tunao na tunaendelea kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lako la pili ambalo umetaka kujua kwamba Serikali tuna mpango gani katika kujenga academy. Nikuhakikishie kwamba sisi kama Serikali tumekuwa tukihamasisha sana kwa sababu tunatambua kwamba hatuwezi kuwa na timu kubwa za kitaifa kama hatujawekeza kwenye kujenga academy ambazo zitalea vijana. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tumekuwa tukitoa hamasa kwanza kwa wadau kwa mashirikisho lakini vilevile hata kwa Waheshimiwa Wabunge tuweze kushirikiana katika kuhakikisha kwamba tunajenga academy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie fursa hii kuwapongeza wadau wote ambao wameshirikiana na Serikali lakini wameunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga academy ikiwepo academy ya kule Kaitaba lakini tunayo academy ya pale Filbert Bayi pamoja na wadau wengine ambao wanafanya kazi vizuri katika kuhakikisha kwamba tunawekeza katika kuwakuza vijana wetu ili siku moja tuweze kuja kuwa na timu ambazo ni bora zaidi. (Makofi)