Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:- Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwahi kupewa jukumu la nyongeza la kusimamia kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba kwa Sheria iliyotungwa na Bunge kwa kutumia Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba ya Nchi:- (a) Je, ni kwa nini Ibara ya 74(6)(e) isitumike ili Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa Mwaka 2019 usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI)? (b) Je, ni kwa nini Serikali haijatekeleza makubaliano na Vyama ya mwaka 2014 ya kuwezesha Uchaguzi wa Vitongoji na Mitaa kutumia Daftari la Wapiga Kura lililoboreshwa badala ya Orodha ya Wakazi? (c) Je, ni hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 unakuwa huru na wa haki?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali imekwepa kujibu msingi wa swali kwa sababu msingi wa swali langu ni kwamba Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba imesema Bunge linaweza kutunga sheria ya kuipa tume jukumu la kusimamia suala lingine lolote na Ibara hiyo ya Katiba pamoja na kuwa kwenye majukumu ya Tume kulikuwa hakuna jukumu la kusimamia kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba, sheria ikatungwa na Bunge ya kura ya maoni…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnyika uliza swali.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Sasa ndio najenga msingi wa swali kwa sababu amejibu tofauti kabisa. ni kwa nini Serikali imeogopa kuleta Bungeni Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo ingeondoa mamlaka kwa Waziri wa TAMISEMI ingeweka daftari la kudumu kutumika na ingepeleka majukumu yote kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili uchaguzi usimamiwe na Tume ya Uchaguzi badala ya kusimamiwa na Serikali yenyewe kwa maana ya Waziri wa TAMISEMI ambaye ni interested part ndio alazimike kutunga kanuni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye sehemu ya mwisho ya majibu amesema kwamba kanuni zimeandaliwa kushirikisha wadau, bahati nzuri nilikuwepo kwenye kikao kilichofanyika mwezi Aprili cha kujadili kanuni. Tumekaa kikao kama vyama, anasema vyama vimeshirikishwa; tumekaa kikao Aprili, Aprili hiyohiyo tarehe
25 mwezi wa nne, Waziri akatoa Kanuni kwa siri zilizochapishwa, zimekuja kutolewa hadharani mwezi Agosti na Kanuni zile hazijazingatia maoni ya vyama, wadau na tayari Kanuni hizo zimeanza kutumika vibaya, tunaona Wakuu wa Mikoa ambao ni viongozi wa kisiasa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tarafa sasa ndio wanapewa jukumu la kusimamia uchaguzi wakati ni makada wa Chama cha Mapinduzi, kutakuwa na uchaguzi wa uhuru na haki katika mazingira kama hayo? (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, majibu ya Serikali ni sahihi kulingana na swali ambalo ameliuliza. Nikirejea swali la Mheshimiwa Mbunge anasema je, ni kwa nini Ibara ya 74(6)(e) isitumike ili kusimamia uchaguzi wa Vitongoji na Vijiji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja anayosema swali la kwanza kwamba kwa nini Serikali isilete mabadiliko ya Katiba, Serikali inaweza ikaleta Muswada wa kubadilisha Katiba lakini pia Mheshimiwa Mbunge ana nafasi hiyo na hajafanya hivyo. Kwa hiyo, angeleta mabadiliko hayo tungeyajadili lakini kwa sasa tunazungumza uchaguzi wa Serikali za Mitaa as by now kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria zilizopo utasimamiwa na Waziri mwenye dhamana, hakuna mabadiliko ya Katiba ambayo yamekwishafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; Mheshimiwa Mbunge ananiuliza kwamba kanuni hizi hazikuzingatia miongozo, sio kweli na yeye mwenyewe bahati nzuri amethibitisha kwamba alihudhuria, sasa mkiitwa kwenye kikao kujadili na kutoa maoni siyo lazima Serikali ichukue kila kitu mnachokisema, maoni yakitolewa wataalam wanakaa, wanaangalia katiba, sheria, miongozo mbalimbali na practice ya kawaida halafu tunaamua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni hizo sasa hivi wala hazikumpa dhamana yoyote Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya kwamba wakasimamie uchaguzi, muongozo huu hapa. Mheshimiwa Mnyika Naibu Katibu Mkuu wa chama chake cha CHADEMA alikuwepo siku hiyo Mheshimiwa Waziri anatangaza kanuni, amepewa kanuni za uchaguzi, mwongozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Mwongozo wa Mpiga kura. Na kanuni inasema pia asasi za kiraia na mtu yeyote yule anaweza akapewa hii akasoma na akaomba miongozo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mnyika asiwe ana hofu, Mheshimiwa Mnyika uchaguzi huu utakuwa ni huru na haki na kanuni imeeleza vizuri nani anapaswa kusimamia uchaguzi huu. Tujipange, tukutane kazini, ahsante. (Makofi)

Name

Freeman Aikaeli Mbowe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:- Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwahi kupewa jukumu la nyongeza la kusimamia kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba kwa Sheria iliyotungwa na Bunge kwa kutumia Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba ya Nchi:- (a) Je, ni kwa nini Ibara ya 74(6)(e) isitumike ili Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa Mwaka 2019 usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI)? (b) Je, ni kwa nini Serikali haijatekeleza makubaliano na Vyama ya mwaka 2014 ya kuwezesha Uchaguzi wa Vitongoji na Mitaa kutumia Daftari la Wapiga Kura lililoboreshwa badala ya Orodha ya Wakazi? (c) Je, ni hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 unakuwa huru na wa haki?

Supplementary Question 2

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tukaona mambo haya ya uchaguzi ni mepesi lakini amani ya Taifa hili itapotea ama itaathirika kama tukipuuza masuala ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, subsidiary legislation zozote zinazotungwa katika nchi hii leo, lazima kwa njia moja au nyingine ziwe ratified na Bunge. Sheria ndogondogo tunazozitunga kabla hazijaanza kutumika kimsingi zinastahili kuletwa kuwa ratified na Bunge. Vikao vya wadau vinavyokaa ni maoni wala vikao vya wadau vinavyokaa kujadili subsidiary legislation ama legislation yote haviwezi kuwa mbadala wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge haijawahi kuona kabisa au kupitia na kuthibitisha ama kuzi-accept ama kutoa maoni kanuni hizi zilizotungwa na TAMISEMI. Ninachouliza Mheshimiwa Waziri atueleze katika utamaduni huo ambako tayari kanuni zimeshaingizwa kazini, Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge haikuzipitia kwa kisingizo kwamba wadau walizipitia ambao sio Bunge. Je, jambo hili ni sahihi? (Makofi)

Name

Dr. Adelardus Lubango Kilangi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Answer

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelezo kidogo kuhusu suala ambalo ameliibua Mheshimiwa Mbowe, amesema kwamba sheria ndogondogo zinapotungwa lazima kuletwa Bungeni kabla ya kuanza kutumika, hiyo kwa mujibu wa utaratibu siyo sahihi na bahati nzuri Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo yupo hapa ataeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo huwa zikishatayarishwa zinapelekwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchambuzi yaani vetting na baada ya hapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali humrudishia Waziri husika na Waziri yule anazi-gazette halafu baada ya hapo zinapelekwa kwenye kikao kinachofuata cha Bunge kwenye Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo kwa ajili ya kuchambuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kusema mtu anaweza kusema labda mchakato huo hautoi nafasi ya kuweza kuziangalia vizuri zile sheria ndogo, kimsingi sheria ndogo zote zinatungwa chini ya sheria mama na ipo misingi ya kisheria inayoelekeza namna gani sheria ndogo zitungwe na mojawapo ya misingi hiyo ni kwamba isipingane kimsingi na sheria mama. Na inapotokea kuna changamoto moja au mbili ile Kamati ya Bunge kuhusu sheria ndogo kutoa maoni na maelekezo yake na kama kuna changamoto yoyote inarekebishwa, kwa hiyo, hakuna tatizo kabisa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)

Name

Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:- Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwahi kupewa jukumu la nyongeza la kusimamia kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba kwa Sheria iliyotungwa na Bunge kwa kutumia Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba ya Nchi:- (a) Je, ni kwa nini Ibara ya 74(6)(e) isitumike ili Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa Mwaka 2019 usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI)? (b) Je, ni kwa nini Serikali haijatekeleza makubaliano na Vyama ya mwaka 2014 ya kuwezesha Uchaguzi wa Vitongoji na Mitaa kutumia Daftari la Wapiga Kura lililoboreshwa badala ya Orodha ya Wakazi? (c) Je, ni hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 unakuwa huru na wa haki?

Supplementary Question 3

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupigania afya yangu, sasa hivi naendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na upotoshwaji mkubwa sana kwa watu wasioitakia mema nchi hii, wamekuwa wakiweka dosari ambazo hazipo kwenye suala hili la uchaguzi. Je, Serikali imejipangaje kuwaelimisha zaidi Watanzania ukweli ambao wamekuwa wakifanya hivyo na uchaguzi umekuwa ni huru na ndio maana wapinzani ni wengi ndani ya Bunge, Madiwani, Wenyeviti na kadhalika. Mmejipangaje kuwaelimisha Watanzania hawa wanaopenda amani katika nchi yao? Ahsante. (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nampongeza na kumpa pole sana kwa kupata shida ya afya na Mungu amemjalia na aendelee kuimarika Mbunge mwenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni swali muhimu sana, nasema ni muhimu kwa sababu ni kweli kwamba hata swali la msingi la leo utaona ni swali ambalo limejaa tu hofu bila sababu yoyote ile kwa sababu uchaguzi wa Serikali za Mitaa si kwamba unaanza kufanyika kwa mara ya kwanza Tanzania leo mwaka huu, ni uchaguzi ambao tumefanya awamu kadhaa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na bahati nzuri niliyesimama hapa pia nimekuwa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa kupitia chama cha upinzani CHADEMA kama ingekuwa uchaguzi sio huru mwenyewe mwaka 2014 nisingekuwa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa pale Kivule, nilishinda uchaguzi na nikawa Mwenyekiti wa Mtaa kupitia chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; uchaguzi wa nchi hii ni huru, nilikuwa Mbunge kupitia CHADEMA, nilishinda kwa kanuni hizihizi na Katiba hiihii iliyopo na leo nimesimama mbele yako kama Mbunge kupitia Chama cha Mapinduzi. Hii yenyewe inaonesha kwamba uchaguzi wa Tanzania ni huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Serikali za Mitaa, mchakato wa uchaguzi huu kanuni zimeandaliwa na wadau waliitwa wakatoa maoni yao, tukachakata na wataalam wakashauri kanuni hii hapa imeshatolewa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi ameshatoa nakala hizi kwa Wakuu wa Mikoa wote na vyama vya siasa wanazo hizi kanuni. Hakuna mtu ambaye amekuja mbele ya Watanzania akakosoa kifungu chochote kwenye kanuni kwamba kimekinzana na Katiba kina mapungufu, wamepokea na wameridhia, tunaendelea na mchakato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda mbali zaidi, tumetoa mwongozo kwa wapiga kura, hapa inaeleza nani ana sifa za kugombea, mchakato ndani ya chama namna mbalimbali za michakato na usimamizi na imetaja nani anapaswa kusimamia uchaguzi na imewakataa mpaka Watendaji wa Kata ukisoma vizuri. Kwa hiyo, nitashangaa sana watu ambao wanakuja hapa wana hofu ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tarafa, Watendaji na watumishi wa Serikali lakini kanuni imeeleza ni nani ambaye anapasa kusimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu cha tatu ambacho kimetolewa ni Mwongozo kwa Mpiga Kura na kanuni imeeleza kama mtu yeyote ama asasi za kiraia anataka kutoa elimu ya uraia, kuchunguza ndani na nje kanuni imetoa mwongozo kuna utaratibu wa kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba Serikali imejipanga vizuri sana kuendesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa na utasimamiwa na Waziri mwenye dhamana na Watanzania wapo tayari sana kufanya uchaguzi huru na haki, wapate viongozi wao, wazingatie maelekezo ya Serikali ili tupate viongozi ambao watatuwakilisha. Wananchi wasiwe na hofu, uchaguzi utasimamiwa na vyombo vipo na kama kuna mtu yeyote ambaye ana jambo lolote ambalo anadhani kwamba linataka maelezo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ipo wazi, tunawakaribisha tupate maoni tujadiliane kwa maana ya kuboresha,

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.