Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:- Bado kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu hasa maeneo ya vijijini:- Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kupunguza au kumaliza tatizo hilo kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Misungwi?

Supplementary Question 1

MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mradi wa kutoka Nyahiti umekamilika, siyo kweli, nilikuwa huko juzi. Mradi huo hautoi maji na Mkandarasi hayuko site na hili lilikuwa ni agizo la Mheshimiwa Rais kwamba miradi kama hii yote ikamilike na ifanye kazi. Sasa atuambie, Wizara imekaidi agizo la Mheshimiwa Rais? Je, ni lini wananchi wa Misungwi watapata maji ya uhakika ? Ukizingatia wako karibu kabisa na Ziwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mwishoni mwa mwaka 2019 Serikali iliweka miundmbinu katika Kata ya Shibula na Bugogwa katika Jimbo la Ilemela, lakini maji hayatoki na yakitoka yanakuwa yanatoka kwa kusuasua na pia yanatoka machafu sana…

SPIKA: Mheshimiwa Susanne unahutubia badala ya kuuliza swali.

MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Spika, najenga hoja.

SPIKA: Aaah, uliza swali.

MHE. SUSANNE P. MASELE: Mheshimiwa Spika, ni lini sasa wananchi wa maeneo hayo watapata maji ya uhakika ili waweze kufaidi miradi hiyo? Ahsante.

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, kwanza napenda kumfahamisha ndani ya wiki mbili nilikuwa katika Jimbo la Misungwi, nilikuwa na Mheshimiwa Mbunge na tumefanya kazi kubwa. Changamoto iliyokuwepo pale ilikuwa ni Mkurugenzi wetu wa Maji. Tumemwondoa na mradi huu mkubwa utasimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira MWAWASA katika kuongeza utendaji. Mradi umekamilika kwa zaidi ya shilingi bilioni 12 katika kuhakikisha wananchi wa Misungwi wanapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Ilemela pamoja na Nyamagana yake tuna mradi zaidi ya bilioni 38 tunatekeleza katika kuhakikisha wananchi wa Nyamagana pamoja na Ilemela wanapata huduma ya maji na nilikuwepo na Waheshimiwa Wabunge na wanafanya kubwa na nzuri na tumemwagiza Mkandarasi, kabla ya mwezi wa Tatu mradi uwe umekamilika na tutakwenda kuuzindua katika wiki ya maji. Kama tulivyosema, wiki ya maji haitokuwa wiki ya mapambio, wiki ya maji itakuwa ni kazi ya kuzindua miradi mbalimbali ya maji ikiwemo na Nyamagana. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:- Bado kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu hasa maeneo ya vijijini:- Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kupunguza au kumaliza tatizo hilo kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Misungwi?

Supplementary Question 2

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza, naipongeza sana Serikali kwa miradi mikubwa ya maji ambayo inatekelezwa kwenye Mkoa wa Mwanza likiwemo Jimbo la Nyamagana na hakika ikikamilika miradi hii itakuwa suluhisho kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, tunao mradi kwenye Kata ya Lwanima wa ujenzi wa tenki la karibia lita 450,000. Ni takribani miaka mitatu sasa na changamoto ni malipo ya certificate ya mwisho hayajalipwa mpaka leo. Ni nini kauli ya Serikali kwa watu wa Lwanima ambao mradi huu na tenki hili lenye matoleo zaidi ya 17 katika kila Mtaa? Ni lini fedha hizi zitatoka ili wakazi wa Lwanima waweze kupata maji ya uhakika na salama?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji kwanza nipende kumpongeza na nithaminishe kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake la Nyamagana, lakini kikubwa maji ni uhai. Ninachotaka kumhakikishia, sisi kama Viongozi wa Wizara hatutakuwa kikwazo kwa Wakandarasi ambao wamefanya kazi yao thabiti kabisa na yenye weledi kuhakikisha kwamba tunawalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie, katika mfuko huu tutalipa ili mradi ule ukamilike na wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu ya maji. (Makofi)

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:- Bado kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu hasa maeneo ya vijijini:- Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kupunguza au kumaliza tatizo hilo kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Misungwi?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Hanang ni moja yenye Wilaya yenye taabu sana ya maji, lakini naishukuru Serikali kwa kazi ambayo tayari imefanyika, lakini bado taabu iko pale pale.

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Visima alikuja kule na mashine ndogo akashindwa kuchimba visima. Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje? Wakala huyu atarudi lini ili achimbe vile visima ambavyo tulikuwa tunajua watavichimba? Ahsante tena. (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kiufupi tu nimwambie mama yangu kwamba, tutawatuma haraka ili kuhakikisha wanakwenda kuchimba visima hivi ili wananchi waweze kupata huduma ya maji, hususan Gehandu.