Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Primary Question

MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:- Katika Jimbo la Ngara wapo wachimbaji wadogo wa madini ya Manganese katika Kata ya Murusagamba, Kijiji cha Magamba na tayari wamepata soko la madini hayo nje ya nchi ikiwemo India, Afrika Kusini na Uturuki:- Je, Serikal iko tayari kutoa kibali kwa wachimbaji hao kuuza madini hayo yakiwa ghafi kutokana na kwamba hakuna mitambo ya uchenguaji hapa nchini?

Supplementary Question 1

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, napongeza viongozi wote wa Wizara hii ya Madini, Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya na matokeo yake tunayaona.

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia kwamba tayari katika mchakato huu na katika ombi hili wameshatekeleza kwa sehemu kwa kuwapa kibali wachimbaji hawa kwa kuanza na tani 500, nashukuru na kuipongeza Serikali kupitia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa lipo soko kubwa la madini haya ya manganese nje ya nchi; Uturuki, India, Afrika Kusini na tayari wachimbaji hawa wadogo wameunganishwa kwenye masoko hayo lakini uchimbaji wa madini hayo unahitaji mtaji mkubwa kwa maana mitambo pia ya kisasa, Serikali iko tayari kuwawezesha wachimbaji hawa wadogo wadogo ili waweze kupata mitambo kama excavator, tipping trucks ili waweze ku-meet uhitaji wa soko na kuongeza kipato kwa Serikali yetu na kwao binafsi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa vile miongoni mwa madini yanayopatikana katika Jimbo la Ngara ni pamoja na Nickel na kwa muda mrefu tumekuwa tukisubiria kuona mradi huu wa Kabanga Nickel unaanza ili kutoa ajira, kuongeza kipato kwa wananchi wa Jimbo la Ngara na Watanzania kwa ujumla, ni lini mgodi huu utaanza ili kuweza kuleta tija kwa wananchi na kwa Taifa pia? (Makofi)

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli soko la Manganese lipo ndani ya nchi na lipo nje ya nchi, na wachimbaji wadogo wamekutana sana na changamoto ya kuwa na upungufu wa mitaji kwa maana ya kununua vifaa vya uchimbaji, Serikali kupitia ule mradi wa SMRP ambao ulikuwa unafadhiliwa na World Bank kupitia katika Wizara yetu ya Madini ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo, lakini ruzuku hizo hazikutumika vema inavyostahili ndipo tuliposimamisha utoaji wa ruzuku hizo na sasa hivi tunatoa elimu kwa wachimbaji, tunatoa taarifa za uchimbaji kwa maana ya geological information na hizi taarifa tunazipendekeza kuzipeleka, au tunazipeleka na kuwashauri watu wa mabenki mbalimbali waweze kuzitambua taarifa hizi na kuweza kuwapatia mikopo wachimbaji wadogo ili wachimbaji hao waweze kukopa na kununua vifaa mbalimbali ambavyo vinaweza vikatumika katika uchimbaji na kuongeza tija katika uchimbaji huo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana na mgodi wa Kabanga Nickel ni kweli kabisa nickel hapo kipindi cha nyuma katika soko la dunia ilikuwa na bei ya chini sana ambapo uchimbaji wake ulikuwa hauna tija, kwa sababu bei ya nickel katika soko la Dunia ilikuwa chini ya dola 3.5 kwa pawn moja, lakini sasa hivi, bei ya pawn moja ya nickel imepanda kwenda hadi dola Sita katika soko la Dunia ambapo Wawekezaji sasa wameanza kuona kwamba wakiwekeza kwenye nickel itaweza kuwa na faida, katika ule mradi wa Kabanga moja ya leseni ambayo ilikuwa ni retention license ilifutwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya mabadiliko ya sheria mwaka 2017 hapa tulipo ni kwamba ile retention license ipo na sasa hivi tunaifanyia mchakato wa kutafuta Mwekezaji ambaye tunaona yuko serious anaweza akawekeza, sasa hivi tuko tayari kutoa leseni hiyo kwa mtu yeyote ambaye tunaona anaweza akafanya shughuli hiyo, mpaka sasa hivi tuna mchakato unaoendelea ndani ya Wizara yetu kuona namna ya kuweza kumpa Mwekezaji ambaye tunaona anaweza akawekeza kwa faida na mradi huo uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni wakati wowote watu wa Kabanga wataona mradi huo unaanza na ninapongeza Serikali kwa juhudi zake za kupeleka umeme eneo hilo pamoja na miundombinu ya reli na barabara ambayo sasa itakuwa ni miundombinu muhimu katika utekelezaji wa mradi huu wa Kabanga Nickel.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.