Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE Aliuliza:- Halmashauri ya Mbulu haina Hospitali ya Wilaya hivyo wananchi wa Kata za Gidhim, Yayeda, Ampatumat hutembea umbali mrefu kufuata huduma katika kituo cha Afya Dongobeshi. (a) Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya Dongobesh ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Mbulu Vijijini na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Hydom? (b) Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya, dawa na vifaa tiba katika kituo hicho cha afya?

Supplementary Question 1

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pia niipongeze Serikali kwa kutuletea fedha hizo shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya unaoendelea hivi sasa, lakini pamoja na majibu haya mazuri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwanza kabisa kuna msongamano mkubwa bado katika Kituo hiki cha Afya cha Dongobesh kwa sababu ya huduma ambayo si nzuri sana kwenye zahanati zetu. Je, ni nini kauli ya Serikali wakati tukisubiri kukamilika kwa ujenzi ambao ndio kwanza umeanza wa Hospitali ya Wilaya ambao utapunguza msongamano kwenye kituo hicho cha afya kupeleka huduma ya vifaa tiba pamoja na watumishi kwenye zahanati zinazozunguka Kituo hiki cha Afya cha Dongobesh?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Tarafa ya Yaeda Chini haina kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itapeleka Kituo cha Afya katika tarafa ya Yaeda Chini ambayo mioundombinu yake migumu na huko ndiko wanakoishi wenzetu Wahadzabe? Ahsante sana.

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ester Mahawe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, tupokee pongezi za kutoka kwa Mheshimiwa Esther. Nilipata fursa ya kwenda Kituo cha Afya Dongobesh na pia nikapata fursa ya kushiriki kuzindua ujenzi wa Hospitali ya Dongobesh kwa maana ya Hospitali ya Wilaya. Kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Mahawe pamoja na Mheshimiwa Flatey Massay kwa ushirikiano mkubwa pamoja na wananchi wao katika kuhakikisha kwamba, huduma za afya zinaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake anaongelea juu ya suala zima la kupeleka watumishi katika zahanati ili kusiwe na msongamano. Wewe ni shuhuda. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumepeleka maombi ya ajira elfu 15 kwa ajili ya watumishi wa Kada ya Afya kwa kadri kibali kitakavyopatikana, naomba nimhakikishie Mbunge na huko nako hatutawaacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, anaongelea juu ya suala zima la kujenga Kituo cha Afya katika Tarafa ya jirani ambako wanaishi jamii ya Wahadzabe ambao wanauhitaji mkubwa. Naomba aendelee kuiamini Serikali tumeahidi tunatekeleza na naamini na yeye anaridhika na mwendo ambao tunaufanya katika kujenga vituo vya afya.

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE Aliuliza:- Halmashauri ya Mbulu haina Hospitali ya Wilaya hivyo wananchi wa Kata za Gidhim, Yayeda, Ampatumat hutembea umbali mrefu kufuata huduma katika kituo cha Afya Dongobeshi. (a) Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya Dongobesh ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Mbulu Vijijini na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Hydom? (b) Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya, dawa na vifaa tiba katika kituo hicho cha afya?

Supplementary Question 2

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri amefika na Serikali imetupa fedha ya kujenga hospitali ya wilaya, lakini Mheshimiwa Waziri atakumbuka tulimsimika kama Mzee wa Mbulu Vijijini na akatuahidi atatupatia Kituo cha Afya kile cha Maretadu na maombi yako kwake. Ndugu yangu awaambie watu wa Maretadu je, kituo cha afya kitaletewa fedha lini? Ahsante sana.

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muungwana ahadi ni deni. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali kama ambavyo tumepeleka fedha katika Kituo cha kwanza cha Dongobesh, tukapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, halikadhalika tutahakikisha kwamba, pale nafasi inapopatikana hatutasahau kwa sababu tumeahidi.

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE Aliuliza:- Halmashauri ya Mbulu haina Hospitali ya Wilaya hivyo wananchi wa Kata za Gidhim, Yayeda, Ampatumat hutembea umbali mrefu kufuata huduma katika kituo cha Afya Dongobeshi. (a) Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya Dongobesh ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Mbulu Vijijini na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Hydom? (b) Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya, dawa na vifaa tiba katika kituo hicho cha afya?

Supplementary Question 3

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Mgombezi ina zahanati na Kata ya Mtonga ina zahanati ambayo ina wakazi wengi, hasa ikizingatiwa kwamba, kuna mashamba ya mkonge. Je, watakuwa tayari sasa kutusaidia kupandisha hadhi Zahanati ya Mtonga pamoja na Zahanati ya Mgombezi ili viwe vituo vya afya, hasa ikizingatiwa kwamba, kuna watu wengi sana ambao wana shughuli za mkonge kule? Nashukuru sana.

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mary Chatanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba, tunajenga vituo vya afya vyenye ramani na hadhi ya kufanana na vituo vya afya. Pale ambapo zahanati ambayo imejengwa ina hadhi ya kulingana na vituo vya afya hatusiti kufanya hivyo, lakini tunafanya kwa kuzingatia kwamba, ramani ile ambayo vituo vya afya vinajengwa na zahanati hiyo ifanane na ramani hizo, lakini pia hata ukubwa wa eneo; inahitaji eneo lisilopungua ekari 15 kuwa na kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sina uhakika katika zahanati ambazo Mheshimiwa Mbunge anaongelea zina maeneo na ramani ya kufanana na vituo vyetu vya afya? Tutafanya vile baada ya kujiridhisha kwamba, vigezo vyote vimetosheleza, kama ambavyo kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama kuna zahanati ambazo tumezipandisha hadhi kuwa vituo vya afya baada ya kuridhika kwamba, matakwa yote ya kituo cha afya yanakamilishwa.

Name

Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE Aliuliza:- Halmashauri ya Mbulu haina Hospitali ya Wilaya hivyo wananchi wa Kata za Gidhim, Yayeda, Ampatumat hutembea umbali mrefu kufuata huduma katika kituo cha Afya Dongobeshi. (a) Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya Dongobesh ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Mbulu Vijijini na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Hydom? (b) Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya, dawa na vifaa tiba katika kituo hicho cha afya?

Supplementary Question 4

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambayo inahudumia wagonjwa 500 kwa siku, hospitali hii kwa miezi minne hivi sasa haina kipimo cha full blood picture, hospitali hii kwa miezi minne haina oxygen, hospitali hii kwa miezi minne haina film, wagonjwa wakienda kupima x-ray wanapewa CD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu Serikali ina mpango gani wa haraka wa kusaidia hospitali hii iweze kutoa huduma kwa wagonjwa?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Minja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina taarifa ya hili ambalo analolisema sasa hivi, lakini nimwombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki tuweze kulifuatilia na kuhakikisha kwamba, hiyo huduma ambayo ni ya msingi kwa wagonjwa iweze kupatikana katika Hospitali hii ya Rufaa ya Morogoro.